Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kutafuta njia mbadala ambazo zitapunguza gharama ya maisha kwa Watanzania kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.
“Nawaomba Watanzania waendelee kuwa watulivu na waiamini Serikali yao kuwa tunaendelea kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha tunapunguza gharama za maisha kwa Wananchi”
Waziri Mkuu ametoa wito huo leo Alhamisi, Mei 5, 2022 katika kikao kilichofanyika usiku wa kuamkia leo kwenye ofisi ndogo ya Waziri Mkuu iliyoko Oysterbay, jijini Dar es Salaam ili kufanya tathmini ya bei ya mafuta na kuangalia namna gani Serikali inaweza kufanya ili kupunguza athari ya bei ya mafuta na kuleta unafuu wa gharama za maisha kwa Watanzania.
Waziri Mkuu amesema kikao hicho kimefanyika ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia ambaye ameagiza viongozi wa sekta husika wahakikishe wanatafuta suluhisho la kupanda kwa bei ya mafuta hata kama bei hiyo inaendelea kupanda duniani.
“Rais ameona changamoto wanayopitia Watanzania kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, hivyo kikao hiki ni matokeo ya maagizo yake ya kuhakikisha sisi kama viongozi tunatafuta suluhisho la muda mfupi na la muda mrefu ili kukabiliana na changamoto hii”