Leo December 9, 2020 Haya ni maneno kutoka kwenye ukurasa wa instagram wa Mbunge wa Nzega Vijijini Hamis Kigwangalla ambaye alikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii
“Awali ya yote namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai, miaka mitano iliyopita haikuwa rahisi kwangu, ilikuwa miaka ya kupanda na kushuka ya kusimama na kuanguka ya kujaribu na kufanya, kukosea na kupatia” Kingwangalla
“Ni kipindi kilichojaa furaha na maumivu, uhai na umauti, ni kipindi nilichonusa kifo na kufufuka, ni kipindi nilichoshangilia na nilicholia machozi, ni kipindi nilichopata ulemavu wa milele na maumivu yasiyoisha wala kusahaulika” Kigwangalla
“Siwezi kumlalamikia Mungu kwa lolote lile zaidi namshukuru kwa kuwa hai na kwa nyakati zote nilizopitia za kiza totoro na za mwangaza, kipindi hiki nilipewa heshima ya kuwa msaidizi wa Rais kwa nafasi nyeti Serikalini (Afya na Maliasili na Utalii)” Kigwangalla
“Naomba nitumie fursa hii kumshukuru Rais, Dr. John Pombe Magufuli, kwa imani yake kubwa kwangu, kwa maelekezo na usimamizi wake, si tu alikuwa Kiongozi wangu mkuu bali pia alikuwa Mwalimu na Baba, sintosahau huruma na upendo alionionesha nilipopata ajali na msiba wa mwanangu” Kigwangalla
“Rais alipokea machela yangu huku akilia machozi, alihakikisha usalama na matibabu yangu wakati wote, ninawashukuru pia Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwa uongozi na usimamizi wao wa karibu, kipekee ninawashukuru sana watumishi wote wa sekta za Afya na Maliasili niliohudumu nao kipindi nikiwa serikalini” Kigwangalla
“Tumepata mafanikio makubwa sana kwa uwezo wao na kwa kujitoa kwao, mara zote walinipa ushirikiano wa dhati kama moja ya viongozi wakuu wa sekta hizo, ninawashukuru sana wadau wote wa sekta nilizohudumu” Kigwangalla
“Mara zote nilipokutana nao niliwasikiliza kwa umakini na kushughulikia changamoto walizokuwa nazo, kimsingi walikuwa dira ya kazi zangu, hata hivyo, mimi ni binadamu dhaifu, sijakamilika, naomba radhi kwa kila niliyemkwaza ama kumuumiza” Kigwangalla
“Haijawahi kuwa lengo langu bali ni jitihada za kujaribu kufanya mambo yafanikiwe, kazi ya kufanya jambo liwe zuri na timilifu siyo rahisi, Mimi sina kinyongo na mtu na naomba sana niliowakwaza wanisamehe” Kigwangalla
“Nimempongeza Dr. Damas Ndumbaro, Waziri wa Maliasili na Utalii na nakusudia kesho kwenda kumkabidhi rasmi ofisi, nawapongeza Mawaziri wote na nawaahidi ushirikiano wangu wakati wote” Kigwangalla