Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ina jukumu la kusimamia na kutathmini sera na miongozo mbalimbali ikiwemo ya rasilimali watu katika Sekta ya Afya nchini. Wizara inatambua umuhimu wa rasilimali watu yenye weledi na umahiri kwa ajili ya usalama wa afya za wananchi.
Mitihani ya muhula wa pili kwa mwaka wa masomo 2020/2021 ilifanyika kitaifa kuanzia tarehe 16 Agosti, 2021 hadi 30 Septemba, 2021. Wizara ilipokea taarifa ya kuwepo kwa viashiria vya kuvuja kwa mitihani hiyo siku ya mwisho ya ufanyikaji wa mitihani ya nadharia (theory examinations), na hivyo kulazimika kuunda Kamati ya uchunguzi iliyojumuisha wataalamu kutoka kwenye vyombo vya ulinzi na usalama.
Kamati hiyo imefanya uchunguzi kuanzia Septemba 6, 2021 hadi tarehe Novemba 30, 2021 na kukabidhi taarifa hiyo kwa Katibu Mkuu (Afya) mnamo tarehe 03 Disemba, 2021. Katika uchunguzi huo kamati imebaini kwamba mitihani ya mwaka wa pili (NTA level 5) ya programu ya Utabibu (Clinical Medicine) ilivuja. Mitihani ya programu zingine zote haikuvuja.
Chanzo cha kuvuja kwa mitihani hiyo kimebainika na vyombo vya ulinzi na usalama vinakamilisha taratibu za kumfungulia mashtaka Mkufunzi aliyethibitika kufungua mitihani, kupiga picha na kuisambaza kwenye mitandao ya kijamii. Vile vile, chuo kilichohusika na kuvuja kwa mitihani hiyo kitachukuliwa hatua kulingana na sheria, kanuni na taratibu zilizopo ili iwe fundisho kwa vyuo au taasisi zingine.
Aidha, kupitia taarifa hiyo, Kamati ya uchunguzi imetoa mapendekezo mbalimbali kwa Wizara ya Afya na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) yatakayosaidia kuimarisha usalama wa mitihani. Napenda kuwajulisha kuwa Wizara ya Afya inakamilisha maandalizi ya mitihani ya wanafunzi wa utabibu wa ngazi ya tano (mwaka wa pili) ambayo ilifutwa baada ya kuthibitika kuwa ilivuja.
Mitihani hiyo itafanyika kuanzia tarehe 13 Disemba, 2021 pamoja mitihani ya marudio kwa wanafunzi ambao hawakufanya vizuri katika mitihani ya awali. Ratiba za mitihani kwa kozi zote za afya zimetumwa vyuoni. Wizara inawaelekeza wanafunzi kuwa watulivu na kuendelea kujiandaa na mitihani hiyo. Aidha, Wizara inawaagiza wakuu wa vyuo pamoja na wasimamizi watakaoteuliwa kuhakikisha kuwa mitihani inafanyika kwa mujibu wa taratibu na miongozo iliyopo ili kuhakikisha usalama wa mitihani.