Mawaziri wawili wa Afrika Kusini wamelazwa hospitalini siku chache baada ya kubainika kuwa wameambukizwa ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na maambukizi ya virusi vya corona.
Habari hizo zilithibitishwa na Ofisi ya Rais wa nchi hiyo juzi Jumanne ambayo ilisema katika taarifa kuwa, wawili hao waliokumbwa na Covid-19 ni Waziri wa Ajira na Kazi, Thembelani Nxesi, na mwenzake wa Madini, Gwede Mantashe.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa, wawili hao walipelekwa hospitalini siku ya Jumatatu kwa ajili ya matibabu zaidi. Inaarifiwa kuwa, mawaziri hao walikuwa wamejitenga nyumbani, baada ya kugundulika kuwa wameambukizwa maradhi hayo ya kuambukiza karibu wiki moja iliyopita.
Hii ni katika hali ambayo, Afrika Kusini inaonekana kuwa kitovu cha maambukizi ya virusi vya corona barani Afrika kwa sasa, ambapo kufikia jana Jumanne, idadi ya visa vya ugonjwa huo vilivyosajiliwa nchini humo ni 372,628, na ile ya waliopoteza maisha kwa maradhi hayo ikiwa ni 5,173.
Kwa mujibu wa Waziri wa Afya wa Afrika Kusini, Zweli Mkhize, kiwango cha wanaopona ugonjwa huo nchini humo kwa wastani ni asilimia 50 ya kesi zote, na kwamba hadi sasa wagonjwa 195,000 wa corona wamepata afueni.