Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amempongeza Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe Emmerson Mnangagwa kwa hatua madhubuti za kufanya mageuzi ya kiuchumi katika nchi hiyo na ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuondoa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Zimbabwe.
Rais Magufuli amesema hayo wakati akitoa hotuba katika Dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa na Rais Mnangagwa kwa heshima yake na kufanyika Ikulu Jijini Harare.
Rais Magufuli amesema katika kipindi kifupi cha tangu Rais Mnangagwa aingie madarakani hali ya uchumi imeanza kuimarika ambapo kwa sasa uchumi wa Zimbabwe unakua kwa wastani wa asilimia 3.5, mwaka ujao unatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 4.2 na mwaka unaofuata kuongeza hadi wastani wa asilimi 4.4.
Kufuatia hali hiyo ameisihi Jumuiya ya Kimataifa kuondoa vikwazo mbalimbali vilivyowekwa dhidi ya Zimbabwe kwa kuwa vikwazo hivyo vinawaumiza wananchi wa Zimbabwe wakiwemo watoto na wanawake.
Katika hotuba hiyo, Rais Magufuli kwa mara nyingine amewapa pole Rais na wananchi wote wa Zimbabwe kwa kupoteza watu takribani 400 waliofariki dunia katika mafuriko yaliyosababishwa na Kimbunga Idai kilichoikumba Zimbabwe Machi 2019. Amesema Watanzania wanaungana na ndugu zao Wazimbabwe katika majonzi ya kuondokewa na jamaa zao na wanawaombea kwa Mwenyezi Mungu aziweke roho zao mahali pema peponi, Amina.
Kuhusu uhusiano wa Tanzania na Zimbabwe ulioasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Mzee Robert Mugabe, Rais Magufuli amesema Tanzania inatambua na inathamini uhusiano huu wa kihistoria na kidugu na amebainisha kuwa jukumu lililopo sasa ni kuelekeza nguvu nyingi zaidi katika uhusiano na ushirikiano wa kiuchumi utakaoziwezesha Tanzania na Zimbabwe kuongeza biashara na uwekezaji.
Rais Magufuli amebainisha kuwa katika mazungumzo yake ya faragha na Rais Mnangagwa leo mchana wamekubaliana kusimamia ipasavyo makubaliano yaliyopo katika Kamati ya Pamoja ya Kudumu (Joint Permanent Commission – JPC) kwa manufaa ya nchi zote mbili.
“Rais Mnangagwa ujio wangu hapa Zimbabwe ni kuthibitisha kuwa urafiki wetu bado upo imara na sisi Tanzania tumejipanga kuuimarisha zaidi, tunataka tufanye biashara zaidi na nyinyi ndugu zetu wa Zimbabwe ili tukuze uchumi wa nchi zetu na kuongeza kipato cha wananchi wetu” amesisitiza Rais Magufuli.
Kwa upande wake, Rais Mnangagwa amemshukuru Rais Magufuli kwa kukubali mwaliko wake, na amemthibitishia kuwa yeye na wananchi wa Zimbabwe wanatambua kuwa Watanzania ni ndugu zao waliojitolea kwa dhati katika ukombozi wao wakiongozwa na dhamira ya dhati ya Hayati Mwl. Nyerere.
Amemshukuru Rais Magufuli kwa kuwa kiongozi wa kwanza katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kutoa msaada wa chakula, dawa na vifaa vya kujihifadhi wakati Zimbabwe alipokumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na Kimbunga Idai mwezi Machi 2019.
Rais Mnangagwa amesema msaada huo uliwagusa Wazimbabwe wengi na kuwakumbusha umuhimu wa kuchukua tahadhari dhidi ya majanga na mabadiliko ya tabia nchi.
Amesisitiza kuwa daima Zimbabwe itabaki kuwa rafiki na ndugu wa kweli wa Tanzania na hivyo amemhakikishia Rais Magufuli kuwa nchi hiyo ipo tayari kukuza zaidi ushirikiano wa kiuchumi kwa kuongeza biashara na uwekezaji pamoja na kushirikiana katika usafiri wa anga.
Amemshukuru Rais Magufuli kwa kumpa mbinu mbalimbali za kiuongozi ikiwemo kuondoa watumishi hewa ambao wamekuwa mzigo mkubwa kwa Serikali na ameahidi kudumisha ushirikiano kati ya chama chake ZANU-PF na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
RAIS MAGUFULI NA RAIS WA ZIMBABWE WAKICHEZA WIMBO WA ‘SHAURI YAKO’