Leo May 20, 2019 Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) umetenga shilingi Bilioni 127.3 kwa ajili ya kufadhili miradi ya kilimo nchini Tanzania kwa kipindi cha miaka 3 kuanzia mwaka 2020.
Rais wa IFAD, Gilbert Fossoun Houngbo amesema hayo leo Ikulu Jijini DSM alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.
Pamoja na kutenga fedha hizo, Houngbo ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Togo amempongeza Rais Magufuli na Serikali anayoiongoza kwa juhudi kubwa anazozifanya katika kukuza uchumi ikiwemo utekelezaji mzuri wa miradi inayofadhiliwa na IFAD, kutilia mkazo umuhimu wa uwekezaji usiokuwa tegemezi, unaolinda utu, unaozalisha kipato kwa wananchi na unaojenga misingi endelevu ya kujitegemea.
Amebainisha kuwa baada ya kutenga fedha hizo, IFAD inasubiri upande wa Tanzania kuainisha maeneo mahususi ya miradi ya kilimo ambako fedha zitaelekezwa na ameeleza kuwa ana matumaini miradi hiyo itafanikiwa kwa kuzingatia kuwa Tanzania ni nchi yenye amani na namna Serikali ilivyo na dhamira ya maendeleo.
Rais Magufuli ameishukuru IFAD kwa ushirikiano wake mzuri na Tanzania na amemhakikishia Mhe. Houngbo kuwa ushirikiano na uhusiano huo ulioanza mwaka 1978 utadumishwa kwa maslahi ya Watanzania.
Rais Magufuli amesema fedha zilizotengwa katika mpango huo wa miaka 3 zitaelekezwa katika maeneo yenye maslahi mapana ya sekta ya kilimo ikiwemo kuwezesha matumizi ya zana bora za kilimo katika uzalishaji, kuzalisha mbegu bora za mazao, kutatua changamoto ya masoko ya mazao, kuboresha ufugaji na ameipongeza IFAD kwa kutoa fedha pasipo kuweka masharti ya maeneo zinakopaswa kuelekezwa.
Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Kilimo kuharakisha mchakato wa kuainisha maeneo yatakayopokea fedha hizo ili utekelezaji wa mpango huo uanze.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa wa Sweden, Peter Eriksson.
Baada ya mazungumzo hayo, Peter Eriksson amempongeza Rais Magufuli na Serikali yake kwa mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya rushwa na ameeleza dhamira ya Sweden kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Balozi wa Sweden hapa nchini Mhe. Anders Sjöberg na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Prof. Palamagamba Kabudi.