Moja ya habari ya Kimataifa inayoshika headlines ni ya Rais wa zamani wa Argentina Cristina Fernandez de Kirchner ambaye amefunguliwa mashtaka ya rushwa, siku tatu baada ya kutangaza kuwania nafasi ya Makamu wa Rais katika uchaguzi wa October.
Kirchner anatuhumiwa kwa kumpendelea Mfanyabiashara Lazaro Baez ili kupatiwa zabuni za umma zenye thamani ya Mamilioni ya dola wakati akiwa Rais mwaka 2007-2015.
Mfanyabiashara huyo anaetokea Jimbo la Santa Cruz ambako ni ngome ya Kirchner, anahisiwa kuanza kupata upendeleo wa aina hiyo wakati Nestor Kirchner ambae ni Mume wa Cristina alipokuwa Rais kati ya mwaka 2003 hadi 2007.
Waendesha mashtaka wamesema zabuni zilitolewa kwa gharama ya juu mno na kusababisha miradi mingine kukwama. Kirchner pia anakabiliwa na mlolongo wa uchunguzi wa madai ya ufisadi, lakini haya ni ya kwanza kufikishwa mahakamani.