Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wito kwa Mataifa ya Afrika kutafsiri vizuri dhana ya uhuru na kujiepusha na masalia ya fikra za kikoloni za kuamini kuwa watawala wa zamani wa Mataifa ya Afrika ndio wenye uwezo wa kusaidia kusimamia na kuendeleza rasilimali zilipo katika Bara la Afrika.
Rais Magufuli ametoa wito huo leo Ikulu alipohutubia Mkutano wa 6 wa Jukwaa la Uongozi Afrika unaohudhuriwa na Marais Wastaafu Benjamin William Mkapa (Tanzania), Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (Tanzania), Thabo Mbeki (Afrika Kusini), Hassan Mohamud (Somalia), Hery Rajaonarimampianina (Madagascar), Mabalozi, Wawakilishi wa Kimataifa na washiriki wa Jukwaa la Uongozi Afrika.
“Maana hasa ya kupigania uhuru ilikuwa ni kurejesha rasilimali na hasa maliasili zetu lakini pia kuwa na maamuzi kamili kuhusu namna ya kuzisimamia na kuzitumia kwa manufaa yetu ili kuleta ukombozi wa kiuchumi, na hii ndio maana pekee ya kulinda uhuru wa kisiasa” Rais Magufuli
Tusijidanganye watawala wetu wa zamani hawawezi kugeuka kwa usiku mmoja na kuwa wajomba zetu au wakombozi wetu kiuchumi, utegemezi huu ndio umeimarisha mizizi na misingi ya ukoloni mamboleo, ni lazima tuamke” Rais Magufuli.