Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo August, 2018 amewaapisha Wakuu wa Mikoa 4, Makatibu Wakuu 2, Makatibu Tawala wa Mikoa 13 na Naibu Makatibu Wakuu 2 aliowateua July 28, 2018.
Wakuu wa Mikoa walioapishwa ni Brig. Jen. Nicodemus Elias Mwangela (Songwe), Brig. Jen. Marco Elisha Gaguti (Kagera), Ali Salum Hapi (Iringa) na Albert John Chalamila (Mbeya), wakati Makatibu Wakuu walioapishwa ni Prof. Joseph Rwegasira Buchweishaija (Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji) na Andrew Wilson Massawe (Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu).
Makatibu Tawala wa Mikoa walioapishwa ni Eric Katemansimba Shitindi (Njombe), Maduka Paul Kessy (Dodoma), Dr. Jilly Elibariki Maleko (Mtwara), Abubakar Mussa Kunenge (Dar es Salaam), Happiness William Seneda (Iringa), Karolina Albert Mthapula (Mara) na David Zacharia Kafulila (Songwe),
Wengine ni Denis Isidory Bandisa (Geita), Abdalla Mohamed Malela (Katavi), Rashid Kassim Mchatta (Kigoma), Missaile Raymond Musa (Manyara), Christopher Derek Kadio (Mwanza) na Prof. Riziki Silas Shemdoe (Ruvuma).
Naibu Makatibu Wakuu walioapishwa ni Dkt. Jim James Yonazi (Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano {Mawasiliano}) na Edwin Paul Mhede (Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji).
Akizungumza baada ya kuwaapisha Rais Magufuli amewataka viongozi hao kwenda kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa katika maeneo waliyopangiwa kwa kushirikiana na viongozi na wafanyakazi wengine waliopo katika maeneo hayo.
Rais Magufuli amesema amechukua muda mrefu kufanya uteuzi wa viongozi hao pamoja na Wakuu wa Wilaya ambao wanaapishwa na Wakuu wa Mikoa katika mikoa waliyopangiwa, ili kujiridhisha juu ya uwezo wao na kwamba anaamini aliowateua watafanya kazi ya kutatua kero za wananchi na kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.
Aidha, Rais Magufuli amewataka Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa kwenda kusimamia ipasavyo ukusanyaji wa mapato ya halmashauri na ameelezea kutoridhishwa na ukusanyaji wa kiwango cha chini wa mapato hasa katika Majiji ya DSM na Mbeya ambayo yana vyanzo vingi na vikubwa lakini yanakusanya kiasi kidogo huku yakizidiwa na Jiji jipya la Dodoma.
“Mkuu wa Mkoa wewe ndio Rais wa mkoa huo, sasa mkoa wako unapokuwa haukusanyi mapato huwa najiuliza sana kuna sababu gani ya kuendelea na Mkuu wa Mkoa ambaye hasimamii ukusanyaji wa mapato?” amesisitiza Rais Magufuli.
Halikadhalika Rais Magufuli amewaonya viongozi wa mikoa wasiokuwa na uhusiano mzuri miongoni mwao na amewataka viongozi hao kuwajibika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015, inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano.
Mapema kabla ya hotuba ya Rais, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa wamempongeza Rais Magufuli kwa kufanya uteuzi wa viongozi hao na wamewataka viongozi hao kuzingatia viapo vyao, kujifunza kwa umakini yaliyopo katika ofisi zao na kusimamia kwa tija shughuli za Serikali.
Maagizo kumi aliyotoa JPM akiwaapisha Makatibu wa wakuu, Ma-RC na Makatibu Tawala