Mfanyabiashara Hamis Said (38), anayekabiliwa na kesi ya kumuua Mkewe, Naomi Marijani ameieleza Mahakama ya Hakimu Kisutu kuwa anaomba apatiwe Line zake mbili za simu zenye zaidi ya Milioni 5 kwa ajili ya matumizi ya nyumbani kwake pamoja na kumlipia ada mwanae.
Said ambaye hivi karibuni alitoa vitisho kwa Waandishi wa Habari kwamba atawafanya kitu mbaya ametoa maombi hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Salum Ally.
Kabla ya kueleza hayo, Wakili wa Serikali Wankyo Simon amemueleza Hakimu Ally kwamba shauri hilo limeitishwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi haujakamilika, hivyo anaomba ahirisho.
Baada ya kueleza hayo, Said alinyoosha mkono na kumueleza Hakimu kwamba ana mambo mawili muhimu ikiwemo nakala yake ya Hati ya Mashitaka na Line zake za simu zilizopo Central Police.
Amedai kuwa anaomba apatiwe line zake mbili zenye zaidi ya Mil. 5 ili ziweze kutumika kwa matumizi madogo madogo pamoja na kumlipia ada ya mwanae.
Said amedai kuwa ana simu nne zipo Central Police kati hizo mbili ndio zina zaidi ya Sh.Milioni 5.
“Sitaki simu ila nipatiwe line ambazo nimpatie ndugu yangu atoe hizo hela kwa ajili ya matumizi, ikiwezekana zitolewe hata Polisi wakiwepo,” Said
Baada ya kueleza hayo, Wakili Wankyo ameeleza kuwa simu hizo ni sehemu ya upelelezi hivyo kwa sasa itakuwa ngumu kumpatia kwa sababu hawawezi kuamini moja kwa moja kama kweli anahitaji kutoa hizo hela.
Pia ameeleza kuwa kesi hiyo ni ya mauaji na maombi hayo alipaswa kuyawasilisha katika Mahakama husika yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Pia kama anahitaji fedha hizo basi atumie njia ya kumuandikia barua Mkurugenzi wa Mashitaka.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Ally alimshauri Said kutumia mbinu ya kuandika barua ambapo ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 10, 2019.
Mshtakiwa anakabiliwa na kosa la mauaji ambapo adaiwa alilitenda Mei 15, 2019 katika oneo la Geza Ulole Kigamboni Dar es Salaam ambapo alimuua mtu anayeitwa Naomi Marajani.
Inakumbukwa kuwa Hamis anadaiwa kumuua mke wake Naomi kisha kumchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya Mkaa ambapo alichukua majivu ya marehemu na kwenda kuyafukia shambani kwake.