Aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Jamal Malinzi amedai katika utawala wake walikuwepo watu walioikopesha TFF, lakini yeye amekuwa Rais wa Kwanza kufikishwa mahakamani licha ya kuikopesha TFF mwaka 2014 na 2016 kiasi cha Sh. Milioni 320.
Malinzi ameyaeleza hayo mahakamani wakati akiendelea kutoa utetezi wake katika kesi inayomkabili ya utakatishaji fedha,baada ya kukutwa na kesi ya kujibu.
Malinzi amedai kuwa katika kipindi chake walikuwepo watu mbalimbali ambao walikuwa wakiikopesha TFF, lakini yeye ndiye Rais wa kwanza kukamatwa na kufikishwa mahakamani.
Akiongozwa na Wakili wake Richard Rweyongeza mbele ya Hakimu Mkazi Maira Kasonde , Malinzi amedai kuwa fedha hizo alikuwa akiikopesha TFF bila masharti yoyote wala kudai riba na kuongeza kuwa alikuwa akilipwa kadiri ambavyo hali ya kifedha ilivyokuwa inaruhusu katika shirikisho hilo.