Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli leo ameendelea na ziara yake Mkoani Ruvuma kwa kutembelea shamba la Gereza la Kitai lililopo Wilayani Mbinga na kuzindua kiwanda cha kuchakata mahindi cha Kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) 842KJ – Mlale Wilayani Songea.
Akiwa Gereza la Kitai, Rais Magufuli ametembelea shamba la mahindi lenye ukubwa wa ekari 650 linalolimwa kwa kutumia wafungwa wa gereza hilo na ambalo linatarajiwa kuzalisha tani 780 za mahindi katika msimu huu.
Kamishna Jenerali wa Magereza Faustine Kasike amemueleza Rais Magufuli kuwa mahindi yatakayovunwa katika shamba hilo yatatumika kulisha Magereza ya Mikoa 3 (Ruvuma, Lindi na Mtwara) yenye wafungwa 2,000 na kubainisha kuwa kupitia mkakati wake wa uzalishaji wa mazao katika Magereza 10 Jeshi hilo linatarajia kuvuna tani 15,135.75 za mahindi, mpunga na maharage msimu huu baada ya kupanua mashamba yanayolimwa kutoka ekari 1,950 hadi kufikia ekari 5,395.
Akizungumza na Askari, Maafisa wa Magereza na wananchi wa Kitai, Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Magereza kwa kuitikia wito wake wa kuhakikisha linawatumia wafungwa ipasavyo katika uzalishaji na ametoa matrekta 2 kwa Gereza la Kitai ili yasaidie kupanua mashamba ya mazao katika eneo la ekari zaidi ya 7,000 zilizopo katika gereza hilo.
Hata hivyo Rais Magufuli amelitaka Jeshi la Magereza kuwahamisha wafungwa waliopo katika magereza yasiyokuwa na shughuli za uzalishaji na kuwapeleka katika magereza yenye shughuli za uzalishaji mali likiwemo gereza la Kitai ambalo lina wafungwa 233 ikilinganishwa na uwezo wake wa kuchukua wafungwa 370 ilihali baadhi ya Mikoa hapa nchini ina idadi kubwa ya wafungwa kupita uwezo wake na hawafanyi kazi zozote za uzalishaji mali.
“Nimeambiwa katika Magereza yetu wapo wafungwa kama 18,000 na Mahabusu 19,000 nataka wafungwa hawa watumike kuzalisha mali badala ya kukaa Magerezani halafu Serikali iwe inatoa fedha kwa ajili ya kuwalisha, Magereza mengine yaige mfano wa Gereza la Kitai.
Nataka wafungwa watumike kwelikweli na kama kuna suala la kisheria, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ipeleke mapendekezo ya mabadiliko ya sheria Bungeni” Rais Magufuli.
Rais Magufuli amelielekeza Jeshi la Magereza liwatumie wafungwa kujenga makazi ya askari pamoja na miundombinu ya huduma za kijamii katika maeneo hayo, pia baada ya kuelezwa na wanafunzi wa Shule ya Msingi Kitai kuwa shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa matundu ya vyoo amechangia shilingi Milioni 5.
Baada ya kutoka Gereza la Kitai, Rais Magufuli amezindua kiwanda cha kuchakata mahindi cha Jeshi la Kujenga Taifa (842KJ) Mlale Wilayani Songea ambacho kina uwezo wa kuchakata tani 5,280 kwa mwaka na amepokea gawio la Serikali kutoka Shirika la Suma-JKT la shilingi Milioni 700.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jen. Venance Mabeyo amesema ujenzi wa kiwanda hicho pamoja na viwanda vingine vilivyo chini ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) vinajengwa ili kuunga mkono sera ya viwanda na kutekeleza majukumu ya jeshi hilo wakati wa amani na kwamba pamoja na kutekeleza wajibu huo JWTZ inaendelea kuhakikisha mipaka ya nchi ipo salama.
Waziri wa Ulinzi na JKT Dkt. Hussein Mwinyi amesema katika kuongeza uzalishaji wa mazao Serikali imejipanga kuhakikisha wanafunzi wanaojiunga na JKT wanatumika ipasavyo kuzalisha mali ikiwemo mazao yatakayotumika kwa chakula cha Majeshi na kuuza ili kupata fedha.
Akizungumza baada ya kuzindua kiwanda hicho Rais Magufuli amempongeza Mkuu wa Majeshi Mabeyo na Mkuu wa JKT vBusungu kwa kazi nzuri zinazofanywa na Jeshi hilo na ameelezea kufurahishwa kwake na namna Jeshi linavyotekeleza maagizo linayopewa ikiwemo ujenzi wa viwanda, ujenzi wa ukuta Mererani, ujenzi wa nyumba Dodoma, uinuaji wa kivuko cha MV Nyerere katika ziwa Victoria na ukusanyaji wa korosho za wakulima na ametaka Majeshi mengine yaige mfano huo.
“Najisikia raha sana kuwa na Jeshi la namna hii, najisikia raha kuongoza vikosi vya ulinzi kama nyinyi, na mimi nawaahidi kuwa Serikali itahakikisha Jeshi linakuwa imara na maslahi yenu yanaboreshwa” amesisitiza Rais Magufuli.
LIVE: ZIARA YA RAIS MAGUFULI RUVUMA ANAZINDUA KIWANDA