Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli leo amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman J.A. Al Thani, Ikulu Jijini DSM.
Viongozi hao wamezungumzia uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Qatar na dhamira yao ya kuhakikisha uhusiano na ushirikiano huo unaendelezwa na kukuzwa zaidi hususani katika masuala ya uwekezaji katika gesi, madini, utalii na miundombinu ya barabara, bandari, nishati, reli na huduma za kijamii.
Rais Magufuli amemshukuru Sheikh Mohammed kwa kuja kwake hapa nchini pamoja ujumbe wa wawekezaji wenye dhamira ya kuwekeza nchini Tanzania na amemuomba ampelekee salamu za shukrani kwa Mtawala wa Taifa la Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani kwa kuendeleza uhusiano na Tanzania.
Rais Magufuli amesema Tanzania inazo fursa nyingi za uwekezaji zikiwemo uchakataji wa gesi, madini, utalii na usafiri wa anga hivyo amemuomba Sheikh Mohammed kuwahamasisha wafanyabiashara wa Qatar kushirikiana na Tanzania kuwekeza katika maeneo hayo.
“Natambua kuwa Qatar mna utalaamu wa kuchakata gesi na sisi tunayo gesi nyingi, kwa hivyo nawakaribisha mje tushirikiane kuwekeza katika sekta ya gesi, na pia natambua kuwa nyie ni wanunuzi wakubwa wa dhahabu, sisi tunayo dhahabu nyingi na hivi sasa tumeanzisha vituo vya ununuzi wa dhahabu, nawakaribisha mje mnunue dhahabu na tutawapa ushirikiano wote mtaouhitaji” Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli ameiomba Qatar kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo uzalishaji wa nishati ya umeme, ujenzi wa reli, barabara na madaraja na pia amemualika Mtawala wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani kufanya ziara hapa Tanzania.
Kwa upande wake Naibu Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed amemshukuru Rais Magufuli na Serikali yake kwa kuendelea kushirikiana na Qatar katika masuala mbalimbali na kubainisha kuwa Qatar inathamini uhusiano huo.
Sheikh Mohammed ameahidi kuwa Qatar ipo tayari kufanyia kazi maombi yaliyotolewa na Mhe. Rais Magufuli na pia kuzileta kampuni za nchi hiyo kuja kuwekeza katika maeneo yenye fursa zenye manufaa kwa pande zote mbili.
Nae Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi amesema baada ya kukutana na Mhe. Rais Magufuli, yeye na Sheikh Mohammed watakua na mazungumzo ya kina kuhusu maeneo ya ushirikiano.
Mazungumzo ya viongozi hao yamehudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Qatar Mhe. Fatma Rajab na Balozi wa Qatar nchini Tanzania Abdullah Jassim Mohammed Al Medadi.
LIVE: MKURUGENZI MKUU TCRA AKIZUNGUMZA MBELE YA KAMATI YA PAC