Uingereza imeihakikishia Tanzania kuwa itaendelea kuwa mshirika wake katika masuala mbalimbali ya ubia wa maendeleo ikiwa ni pamoja na kuhamasisha Wawekezaji kuwekeza Tanzania kama moja ya hatua za kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano ili iweze kufikia azma yake ya kuwa nchi ya uchumi wa kati na viwanda ifikapo 2025.
Waziri wa Masuala ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza katika Idara ya Ushirikiano wa Maendeleo, Harriett Baldwin ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi, Jijini London, Uingereza kwa nia ya kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo na ushirikiano baina ya Tanzania na Uingereza.
Katika mazungumzo hayo Waziri Harriett na Prof. Kabudi wamezungumzia kuhusu hali ya ushirikiano wa ubia wa maendeleo uliopo hivi sasa na kuonesha kuridhishwa na Serikali ya Tanzania inavyosimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Serikali ya Uingereza katika sekta za elimu, afya, maji, kilimo pamoja na miundombinu ya barabara hususani vijijini ikiwemo maboresho ya mifumo ya fedha, utumishi wa umma, serikali za mitaa miongoni mwa miradi mingine mingi.
Pia, Waziri Harriett ameipongeza Serikali ya Rais Magufuli katika kupambana na rushwa, kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma katika sekta ya umma, kuongeza uwajibikaji na utawala bora mambo aliyoyataja kama hatua muhimu ya kufikia malengo ya haraka na kuondoa umasikini.
Kwa upande wake, Waziri Kabudi ameishukuru Serikali ya Uingereza kwa kuwa mbia mkubwa wa maendeleo na kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa uwekezaji,biashara na utalii nchini Tanzania.
Aidha, Prof Kabudi amemhakikishia Waziri Harriett nia thabiti ya Serikali ya Rais Magufuli ya kufanya mageuzi muhimu ya kiuchumi na kiutawala yanayolenga kuifikisha Tanzania katika mojawapo ya nchi za uchumi wa kati.
Miongoni mwa maboresho hayo, Waziri Kabudi ameyataja kuwa ni pamoja na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara,maboresho katika usimamizi wa utendaji wa Serikali katika kuwahudumia wananchi na utoaji huduma za kijamii hususani sekta zinazowagusa wananchi wengi hususani wa kipato cha chini.