Mwandishi wa habari za uchunguzi Erick Kabendere amepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka matatu ikiwemo kuongoza genge la Uhalifu, kukwepa kodi na kutakatisha zaidi ya Sh. Milioni 100.
Hati ya mashtaka dhidi ya mshtakiwa Kabendera imesomwa na Mawakili wawili wa Wakuu wa Serikali na mmoja Mwandamizi mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Augustine Rwizile.
Mshtakiwa Kabendera anatetewa na Mawakili wa kujitegemea, Jebra Kambore, John Mallya na Benedict.
Akisoma shtaka la kwanza, Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi amedai, mshtakiwa anadaiwa katika siku tofauti tofauti kati ya Januari 2015 na Julai 2019 katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam, mshtakiwa Kabendera alitoa msaada katika genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia faida.
Katika shtaka la pili lililosomwa na Wakili Wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi imedaiwa, siku na mahali hapo mshtakiwa bila kuwa na sababu za msingi kisheria alishindwa kulipa kodi ya sh. 173, 247,047.02 ambayo ilitakiwa ilipwe kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
Katika shtaka la utakatishaji fedha lililosomwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon imedaiwa, kati ya Januari 2015 na Julai 2019 ndani ya Jiji na Mkoa wa DSM mshtakiwa alijipatia kiasi hicho cha sh. Milioni 173.2 wakati akizipokea alijua kuwa fedha hizo ni mazao ya makosa tangulizi ya kukwepa kodi na kujihusisha na genge la uhalifu.
Hata hivyo, mshtakiwa Kabendera hakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo isipokuwa kwa kupata kibali kutoka kwa DPP.
Mawakili wa utetezi wakiongozwa na wakili Kambore, wameomba upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi haraka kwani kesi dhidi ya mteja wao haina dhamana.
Hivyo katika tarehe itakayokuja wangependa kujua upelelezi umefikia wapi.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 19 Mwaka huu, mshtakiwa amepelekwa rumande.
Katika hatua nyingine Wakili wa upande utetezi Jebrah Kambole ameiomba mahakama kuondoa maombi yao ya awali ya kutaka mshitakiwa afikishwe mahakamani na kupatiwa dhamana lakini kwa sababu kwa sababu mshtakiwa ameishafikishwa mahakamani na mashtaka yake hayana dhamana hivyo wanaomba kuondoa maombi yao.
Hakimu Rwizile aliyaondoa maombi hayo kama walivyoomba upande wa utetezi utetezi.