October 30, 2018 Mkuu wa Mkoa wa Pwani Engineer Evarist Ndikilo ameipongeza TIC kwa jitihada zake katika kukuza na kuvutia uwekezaji nchini na namna inavyowahudumia wawekezaji kupitia huduma za mahala pamoja zinazotolewa na taasisi mbalimbali zilizopo ndani ya ofis za TIC.
Engineer Ndikilo ametoa pongezi hizo wakati alipotembelea banda la TIC katika Maonesho ya wiki ya Viwanda Mkoa wa Pwani amesema mkoa huo ni miongoni mwa Mikoa inayopokea wawekezaji wengi na hivyo nguvu ya kuwahudumia lazima iimarishwe.
Aidha ameshauri TIC kuhakikisha inapata taarifa zote muhimu zinazohusiana na uwekezaji ndani ya mkoa wa Pwani kwa kuwasiliana na ofisi za Halmashauri. Kwani kwa kufanya hivyo kutarahisisha uratibu na huduma kwa wawekezaji nchini.
RC Ndikilo ameisisitiza TIC iwe na taarifa za maeneo ya uwekezaji yaliyotengwa, takwimu za miradi ya uwekezaji. Katika kuhakikisha Pwani unaendelea kuvutia uwekezaji RC atawasilisha TIC maeneo ambayo tayari yametengwa kwa ajili ya uwekezaji ili yaweze kutafutiwa wawekezaji.
Akizungumza na Waandishi wa habari Meneja wa Kanda ya Mashariki Venance Mashiba amesema kuwa katika kuharakisha utatuzi wa changamoto zinazowakabili wawekezaji, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimeunda Kamati Maalum ya kitaifa inayojumuisha Wakuu wa Taasisi za Serikali ambazo ni wadau katika kuhudumia uwekezaji.
Mashiba “Kamati hii hukutana chini ya Mwenyekiti wa muda ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa TIC na kujadili changamoto mbalimbali za uwekezaji na kuzitafutia ufumbuzi na inajadili changamoto mbalimbali ikiwa ni sehemu yake ya mpango kazi wa kuhakikisha huduma za wawekezaji zinaboreshwa.”
Kamati hiyo ilianza kufanya kazi Mwishoni mwa mwaka jana ikiwa na wajumbe wanaounda kituo cha huduma za mahala pamoja inayoundwa na taasisi 11 zikijumuisha Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni BRELA, Uhamiaji, Shirika la Viwango Tanzania TBS, Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania TFDA, Wizara ya Ardhi,
Kazi na Ajira, Wakala wa Usalama mahala pa Kazi OSHA, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa NIDA na Shirika la Umeme Tanzania TANESCO, NEMC
“Sisi TIC tunataka kuhakikisha wawekezaji wanapata urahisi wa kuendesha miradi yao na tunahakikisha kila mara tunaboresha mazingira ya uwekezaji, hatutaki Mwekezaji akij ahangaike kutafuta vibali au leseni zinazohitajika, au achelewe kutatua changamoto zinazomkabili” Mashiba.
Aidha Kituo kinawakaribisha watu wote, Jumuiya ya wafanyabiashara na wawekezaji wote kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kwenye maonesho hayo ili wajionee bidhaa zinazozalishwa mkoa wa Pwani na huduma nyingine zinazotolewa na taasisi mbalimbali zinazoshiriki maonesho haya.
Maonesho ya Wiki ya Viwanda Mkoa wa Pwani yanaendelea katika viwanja vya Sabasaba vilivyopo Picha ya Ndege Wilayani Kibaha Mkoani Pwani.