Wakulima wa Wilaya tatu za Mtwara, Nanyumbu na Masasi ambao wanasimamiwa na chama kikuu cha ushirika cha MAMCU, licha ya kukukubali kuuza Korosho zao, wamesikitishwa na kitendo cha Kampuni moja pekee ya Korosho Africa, kujitokeza mnadani kununua korosho, huku kati ya zaidi ya Tani Elfu 9 kampuni hiyo ikinunua Tani 200 tu, kwa bei ya Tsh.3001 kwa kila kilo.
Mnada huo wa kwanza tangu kauli ya Rais Magufuli kuwataka wanunuzi kutonunua chini ya Shilingi Elfu tatu, umefanyika Chiwale wilayani Masasi ambapo mara baada ya mnunuzi mmoja pekee kutangazwa uliibuka mvutano mkali wa wakulima wengine wakitaka korosho zisiuzwe kufuatia idadi ndogo ya Tani zilizonunuliwa, lakini baadaye walikubaliana kuuza kwa matumaini ya kusubiri mnada unaofuatia .
Katika hatua nyingine leo pia umefanyika mnada mwingine ambao umewahusisha wakulima wa Wilaya za Newala na Tandahimba chini ya chama kikuu cha ushirika TANECU, ambao pia wamekubali kuuza korosho zao kwa bei ya juu ya Tsh.3016 huku Bei ya chini ikiwa Tsh 3000.
Katika mnada huu uliofanyika Mdimba wilayani Tandahimba na kushuhudiwa na Waziri wa Kilimo Dr.Charles Tizeba ambaye alikuwa mgeni, rasmi jumla ya tani 2141 zimeuzwa kati ya Tani 7000 zilizopigwa mnada na TANECU.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mnada huo, Waziri Tizeba amesema matokeo ya mnada si mabaya ukilinganisha na minada iliyotangulia na kuwapongeza wanunuzi kwa kutekeleza agizo la Rais la kununua kwa bei isiyopungua Elfu tatu na kusema ni mwanzo mzuri na pengine bei inaweza kupanda kwenye minada ijayo.
Kaduguda alivyowakataa Waandishi baada ya matokeo ya Uchaguzi Simba SC