Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi mkoa wa Mbeya imeamuru kutolewa katika chumba cha kuhifadhia maiti na kwenda kuzikw mwili wa marehemu Frank Kapange aliyefariki dunia katika mazingira ya kutatanisha zaidi ya miezi miwili iliyopita na ndugu kususia mwili huo.
Akitoa hukumu juu ya maombi ya mzazi wa marehemu Julias Kapange kupitia wakili wake Moris Mwamwenda ambaye hakuwepo mahakamani kwakuwa uamuzi huo ulipangwa kutolewa Septemba 4 mwaka huu hakimu mkazi Mfawidhi Michael Mteite amekataa kufanyiwa uchunguzi mwili wa marehemu kama walivyoomba ndugu hao wa marehemu.
Hakimu Mteite amesema sio kawaida kwa tamaduni za Kitanzania kuona mwili wa marehemu unakaa zaidi ya miezi miwili na nusu Mochwari hivyo ameelekeza hospitali ya rufaa Mbeya kuruhusu ndugu wa marehemu kuchukua mwili huo kwenda kuzika.
Hakimu amegoma kuruhusu kufanyiwa uchunguzi mwili wa Amarehemu kama ilivyoombwa kwa madai kuwa wakili wa ndugu hao alichelewa kuwasilisha majumuisho ya maombi yao iliyokuwa yatolewe Agosti 14 mwaka huu pamoja na kuandaa majumuisho hayo badala ya mzazi aliyekuwa anajua hali ya mtoto hadi anakutwa na umauti.
Hakimu huyo amesema ni dhahiri kuwa wakili wa walalamikaji hakuwa na maslahi na kesi hiyo hivyo akaamuru kutolewa na kwenda kuzikwa mwili wa marehemu na kwamba endapo ndugu wataendelea kususia mwili huo basi Mkurugenzi wa hospitali ya rufaa Mbeya kwa kushirikiana na maofisa wa idara ya afya jiji la Mbeya watalazimika kwenda kuzika mwili huo.
Akizungumza nje ya Mahakama baba mkubwa wa marehemu Julius Kapange amesema atawasiliana na wakili wake na kukata rufaa mapema iwezekanavyo kwa kuwa hawajaridhika na mwenendo wa kesi hiyo sanjari na hukumu yake.
Haya yalikuwa maombi namba 2/2018 ambayo mtoa maombi baba mkubwa wa marehemu Julius Godwin Kapange aliomba kufanyiwa uchunguzi mwili wa mtoto wake Frank Kapange (21) mkazi wa Airport ya zamani anayedaiwa kufariki dunia katika mazingira ya kutatanisha Juni 04 mwaka huu hivyo ni siku 80 tangu marehemu afariki na mwili bado uko mochwari katika hospitali ya rufaa kanda ya Mbeya.