Afisa Usalama wa Shirika la Posta, George Mwamgabe (44) na Dereva Abraham Msimu (54) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na makosa mawili ikiwemo kusafarisha dawa za kulevya aina ya Bangi gramu 125.
Washitakiwa hao wamesomewa mashitaka yao na Wakili wa Serikali, Adolf Lema mbele ya Hakimu Mkazi, Augustina Mbando.
Katika shitaka la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Bangi zenye uzito wa gramu 125, wanadaiwa wamelitenda Agosti 25, 2018 katika eneo la Posta Ilala Dar es Salaam.
Pia kosa jingine la kusafirisa dawa za kulevya aina Heroine Hydrochloride zenye uzito wa gramu 1.55 wanadaiwa walilitenda Agosti 25, 2018 katika jiji la Dar es Salaam.
Washitakiwa hao wamekana makosa hayo na upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Washitakiwa hao wameomba wapatiwe dhamana ambapo wamepewa masharti ya kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh.Mil 5 kila mmoja na mmoja wa wadhamini atoke Ofisi ya Umma.
Hata hivyo wameshindwa kutimiza masharti hayo, hivyo wamerudishwa rumande na kesi imeahirishwa hadi Oktoba 16, 2019.