Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu Raia wawili wa China, Li Ling na Chen Guo kulipa faini ya Sh.Mil 70 baada ya kukiri makosa yao ikiwemo la kusafirisha Kucha 25 za Simba.
Pamoja na kuachiwa huru, mahakama hiyo imetaifisha gari aina ya Toyota Prado T 982 CDH na mashine mbili za washtakiwa hao na kuwa mali ya Serikali huku ikimtaka mshtakiwa Chen Guo kulipa faini ya Sh. Milioni 1 kwa kosa la kuishi nchini bila kibali.
Hatua hiyo, imekuja baada ya upande wa mashtaka kuwafutia washtakiwa hao mashtaka ya uhujumu uchumi na kuwasomea mashtaka mawili ya kujihusisha na nyara za serikali na kuishi nchini bila kibali.
Hata hivyo washtakiwa wengine wanne waliokuwa katika kesi hiyo ambao ni raia wa China wamegoma kukiri mashtaka yao yanayowakabili hivyo wamerudishwa rumande.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi ambapo amesema mshtakiwa Li Ling anapaswa kulipa fidia ya Sh. Mil 45 na mshtakiwa Chen Guo atalipa Sh. Mil 25 na faini ya Sh. Milioni 1 au kwenda jela mwaka mmoja.
Pia amesema, gari aina ya Toyota Prado na mashine mbili zinataifishwa na kuwa mali ya Serikali na amewataka washtakiwa hao kuondoka nchini mara moja kwa kuwa sio raia wa Tanzania. .
Kabla ya kutolewa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali, Salim Msemo amedai hawana kumbukumbu ya nyuma ya makosa kwa washtakiwa hivyo, anaiomba mahakama itoe adhabu kulingana na makubaliano ili iwe fundisho kwao na wengine.
Mapema, akisoma makubaliano hayo, Wakili Msemo amedai kuwa wameingia makubaliano na washtakiwa hao baada ya kukiri kosa la kujihusisha na nyara za serikali na kuishi nchini bila kibali, hivyo wameamua kuondoa mashtaka ya uhujumu uchumi.
Baada ya kusoma makubaliano hayo, Hakimu Shaidi aliwaapisha washtakiwa na kuwauliza kama walisaini kwa hiari yao na kudai alifanya hivyo kwa hiari yao.
Miongoni mwa mashtaka mapya, inadaiwa Julai 5, 2015 katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) mshtakiwa Li Ling Ling alisafirisha nje ya nchi kucha 25 za simba zenye thamani ya Sh. 22, 500,000 bila kuwa na kibali.
Pia kosa jingine inadaiwa Julai 5, 2015 katika uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere mshtakiwa Cheng Guo alisafirisha nje ya nchi meno 21 ya simba yenye thamani ya Sh. 12, 500,000 bila ya kuwa na kibali.