Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma inatarajia kuanza kusikiliza kesi inayomkabili Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyantole, Jason Rwekaza (42) anayetuhumiwa kubaka na kumpa ujauzito Mwanafunze wake wa Darasa la Tano.
Kesi hiyo ambayo ipo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Flora Mtalania inatarajiwa kuanza kusikilizwa Agosti 26, 2019.
Hatua hiyo inatokana na kukamilika kwa upelelezi ambapo Wakili wa Serikali, Clement Masua ameieleza Mahakama kwamba wameandaa mashahidi 10, vielelezo viwili ikiwemo daftari la mahudhurio na PF3.
Naye Wakili wa utetezi, Thomas Msasa aliiomba mahakama kutoa ruhusa mteja wake kupima vinasaba (DNA), pindi mwanafunzi huyo atakapojifungua ili haki iweze kutendeka kwa pande zote wakati kesi ikiwa inaendelea.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mtalania ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 26, 2019 kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.
Katika kesi hiyo mshitakiwa anakabiliwa na mashitaka saba, ikiwemo kumpa ujauzito mwanafunzi, huku mashitaka mengine yakiwa ya Ubakaji.
Mwalimu huyo ameshitakiwa chini ya kifungu cha sheria 130 (1)(2)(e) na 131 (1) cha makosa ya jinai kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Pia kosa la kumpa mimba mwanafunzi huyo anashitakiwa chini ya kifungu cha 60 (a) kifungu kidogo cha (3) cha Sheria ya elimu namba 353 ya mwaka 2002 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2016.