Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, (NHC) bwana Hamad Abdallah amewatoa hofu wapangaji wa nyumba za shirika hilo wa eneo la Kariakoo ambao watatakiwa kupisha eneo hilo kwa ajili ya uwekezaji.
Amesema wapangaji hao wangeweza kupewa notisi ya mwezi mmoja lakini wameongezewa muda wa miezi saba ndipo wapishe mradi wa ujenzi kisha watarejea kwenye majengo mapya baada ya uwekezaji huo mkubwa kukamilika.
Mkurugenzi huyo amesema kinachotumika ni jicho la huruma kama ambavyo anataka Rais Samia kwamba Pamoja na sheria lakini litumike jicho la huruma na siyo kuwaacha watu barabarani wakiwa hawana pa kuishi
Mbali na Kariakoo NHC imepanga kuanza ujenzi wa nyumba 200 za makazi katika jiji la Dodoma ikiwa ni sehemu ya mpango wa Shirika hilo kuwezesha makazi bora kwa Watanzania.
Akiendelea kuzungumza na Waandishi wa Habari kwenye viwanja vya Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam bwana Hamad Abdallah amesema Kwa mwaka huu wa fedha wataanza ujenzi wa nyumba 100 katika eneo la Njedengwa ikiwa ni awamu ya kwanza ya Mpango wa Samia Scheme kwa Jiji la Dodoma
Shirika la Nyumba la Taifa ni miongoni mwa Mashirika na makampuni 1, 188 ya ndani yanayoshiriki maonesho ya 47 ya kimataifa ya biashara maarufu kama Sabasaba na zaidi ya Mataifa 30 duniani, yanatarajiwa pia kushiriki katika maonesho hayo ya mwaka 2023.