MKURUGENZI Mstaafu wa Makosa ya Jinai nchini (DCI) Balozi Adadi Rajabu ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini kuhakikisha wana buni mbinu zinazoweza kudhibiti vitendo vya rushwa ya ngono nchini.
Balozi Adadi aliyasema hayo wakati wa mahafali ya kidato cha nne ya shule ya Sekondari Muheza Muslim ambapo alisema kwamba vitendo vya Rushwa ya ngono vimekuwepo na Takukuru wamepewa jukumu la kudhibiti vitendo hivyo ni wakati sahihi kuhakikisha wanakuja na mwarobaini wake.
Alisema kwamba wao wanapaswa kuona namna nzuri ya kubuni mbinu ambazo zinaweza kupelekea kudhibiti badala ya kusubiri matukio yanatokea ndio waweze kuanza kupambana nayo.
“Haya mambo yapo kwa sababu kwenye vyuo hivyo ni jinsi ya vyombo vilivyo kabidhiwa kufanya kazi hiyo wanafanya nini ili kuweza kuondokana na tatizo hilo”- Alisema Balozi Adadi.
Aidha alisema kwamba wanataka wanaofanya vitendo hivyo wakamatwe ili iweze kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia za namna hiyo kuweza kubadilika hivyo suala hili lina umuhimu wake hasa chombo ambacho kimepewa mamlaka ya kusimamia.