Mahakama kuu ya Indonesia ilikubali rufaa kutoka kwa waendesha mashtaka na kumhukumu kifo Mkuu wa Shule ya Bweni ya Kiislamu kwa kubaka wanafunzi 13 kwa zaidi ya miaka mitano na kuwapachika mimba baadhi yao.
Herry Wirawan alikuwa amehukumiwa na jopo la majaji watatu katika Mahakama ya Wilaya ya Bandung mwezi Februari, kifungo cha maisha jela. Alikuwa ameshtakiwa kwa kubaka wasichana kati ya miaka 11 na 14 kutoka 2016 hadi 2021 katika shule, hoteli au vyumba vya kukodi katika jiji la West Java. Takriban watoto tisa waliripotiwa kuzaliwa kutokana na ubakaji huo.
Kesi yake ilizua kilio cha umma kwani kulikuwa na wahasiriwa kadhaa kwa miaka kadhaa. Polisi walisema waathiriwa walikuwa na woga sana kumwambia mtu yeyote.
Majaji wa Mahakama Kuu ya Bandung katika uamuzi wao wa Jumatatu walikubaliana na rufaa ya waendesha mashitaka ya hukumu ya kifo na mali ya Wirawan kutwaliwa.