Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametangaza siku 3 za Maombolezo ya Kitaifa kuanzia Jumamosi kufuatia vifo vya watu zaidi ya 60 vilivyosababishwa na ajali ya kuungua kwa moto wakati wakichota mafuta yaliyokuwa yakimwagika baada ya lori la mafuta kupinduka Mjini Morogoro.
Ajali hiyo imetokea leo majira ya saa 2 asubuhi ambapo lori lenye shehena ya mafuta ya petroli limepinduka jirani na Kituo Kikuu cha Mabasi cha Msamvu Mjini Morogoro wakati dereva alipokuwa akijaribu kumkwepa mwendesha pikipiki.
Pamoja na zaidi ya watu 60 kufariki dunia watu wengine takribani 70 wamejeruhiwa na wanapatiwa matibabu katika hospitali ya Mkoa wa Morogoro na Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.
Rais Magufuli amemtuma Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa kumwakilisha katika mazishi ya Marehemu wa ajali hiyo yanayotarajiwa kuanza kesho Jumapili tarehe 11 Agosti, 2019.
Katika kipindi cha maombolezo bendera zote zitapeperushwa nusu mlingoti.
RAIS MAGUFULI ATOA SIKU TATU ZA MAOMBOLEZO