Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) limetangaza Matokeo ya Darasa la Saba 2019 na kusema kuwa ufaulu umeongezeka kwa asilimia 3.78 ambapo waliofaulu ni asilimia 81.50 ya Watahiniwa 933,369
Pia, limesema Watahiniwa 909 wamefutiwa matokeo kwa sababu mbalimbali ikiwemo kufanya udanganyifu ambapo Baraza limesema limebaini Walimu Wakuu, Wasimamizi na walinzi walihusika kwenye udanganyifu
Katibu Mtendaji wa NECTA, Dkt. Charles Msonde ameeleza kuwa katika kikao kilichokaa leo tayari wameshazitaarifu Mamlaka za Ajira na Sheria ili ziwachukulie hatua waliohusika na udanganyifu huo
Dkt. Msonde amesema Mwanafunzi aliyeongoza Kitaifa ni Grace Manga kutoka Shule ya Msingi Graiyaki wa Mkoani Mara, akifuatiwa na Francis Gwagi kutoka Shule ya Msingi Paradise ya Geita na aliyeshika nafasi ya tatu ni Loi Kitundu kutoka Shule ya Msingi Mbezi ya DSM.
Aidha, ameeleza “Katika ufaulu wa masomo, somo la Kiswahili, Kiingereza na Sayansi katika mtihani huo ufaulu wake umepanda na somo la Hisabati umeshuka,”