Bunge la Jimbo la Nairobi limepokea mswada wa sheria unaosema mtu yeyote atakayekutwa akitema mate ama kupenga kamasi bila kutumia kitambaa Jijini Nairobi, atahukumiwa kifungo cha miezi sita gerezani au kutozwa faini ya Sh10,000.
Sambamba na wenye makosa hayo, adhabu kama hiyo itatolewa kwa yeyote atakayebainika kushiriki katika vitendo vya ukahaba.
Makosa mengine yaliyoorodheshwa na mswada huo ni kuacha mbwa ovyo kwenye barabara, kuosha ama kurekebisha magari kwenye barabara za jiji, kuvuta sigara kwenye maeneo ya umma na utingo kuwaita abiria kwenye magari yao.
Mswada huo, ambao uko katika awamu ya kwanza, unalenga kuchukua mahali pa sheria za jiji la Nairobi, ambazo zimepitwa na wakati baada ya mfumo wa ugatuzi kuanza kutekelezwa.