Katika hali isiyo ya kawaida, raia wa Burundi, Habonimana Nyandwi ambaye ni mshtakiwa katika kesi ya mauaji ya Mwanaharakati wa Tembo, Wayne Lotter amezimia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ikidaiwa ni kwa sababu ya njaa.
Hayo yameibuka mahakamani hapo wakati kesi hiyo ilipotajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mfawidhi, Godfrey Isaya.
Wakili wa Serikali, Easter Martin amemueleza Hakimu Isaya kuwa kesi hiyo imeitishwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi haujakamilika, pia jalada la kesi hiyo lipo kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
Awali kabla washtakiwa hao kupandishwa kizimbani, mshtakiwa Habonimana Nyandwi alishindwa kusimama na kudondoka chini huku akionekana kugeuza macho, ndipo Askari Polisi waliokuwa karibu walimsogelea na kumvua viatu pamoja na mkanda.
Kufuatia hali hiyo, washtakiwa wenzake walipanda kizimbani ambapo mshtakiwa Ndimana Zebadayo alinyoosha mkono huku akiangua kilio kwa nguvu na kudai, raia wa kigeni waliopo kwenye kesi hiyo hawajui ushiriki wao lakini hawana ndugu wala mtu yeyote wa kuwaona wala kuwapa chakula.
“Tumedhoofika hatuna ndugu wa kutuletea chakula hapa nchini na gerezani tunanyimwa chakula leo siku ya tano, tumekatiwa huduma ya chakula kama raia wa kigeni,”amesema.
Akijibu hoja hizo, Wakili Easter amedai, mahabusu wanapatiwa huduma zote za chakula pamoja na malazi Magereza, hivyo kuhusu hilo suala ni vema, wakaulizwa Magareza.
Hata hivyo, askari magereza alipoulizwa juu watuhumiwa hao kutopewa chakula alidai kuwa hana taarifa zozote kwa anachojua yeye mahabusu wote wanapata chakula.
Naye, mshtakiwa Ayubu Selemani amedai, katika mahabusu ya Keko kuna raia wa Kigeni wengi na wote wanapata chakula kwa wakati isipokuwa wawili hao waliopo kwenye kesi hiyo ambapo wamekatiwa huduma siku tano.
Kutokana na hatua hiyo, Hakimu Isaya ameahirisha kesi hiyo kwa siku saba ambapo itatajwa tena Januari 24,2020 ili kupata taarifa zaidi juu ya malalamiko ya washtakiwa hao.
Washtakiwa katika kesi hiyo ya mauaji namba 9 ya mwaka 2017 ni raia wa Burundi Habonimana Nyandwi, Nduimana Jonas maarufu Mchungaji na Robert Mwaipyana.
Wengine ni Godfrey Salamba (42) mkazi wa Kinondoni Msisiri A. Inocent Kimaro (23) mkazi wa Temeke Mikoroshini, Chambie Ally (32) mkazi wa Kia/Boma na Ofisa wa NBC, Robert Mwaipyana (31) mkazi wa Temeke Mikoroshini.
Wengine ni Meneja wa Benki ya Backlays, Khalid Mwinyi (33) mkazi wa Mikocheni B, Rahma Almas (37) mkazi wa Mbagala B na Mohammed Maganga (61) mchimba makaburi, Allan Mafue, Ismail Mohammed, Leornad Makoye, Amino Sham, Ayoub Selemani, Joseph Lukoa, Gaudence Matemu na Abuu Mkingie.
Katika kesi ya msingi washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kuwa kati ya Julai Mosi na Agosti 16, 2017 walikula njama ya kufanya mauaji ya Lotter.
Katika shtaka la pili, washtakiwa hao wanadaiwa Agosti 16, 2017 katika makutano ya barabara za Chole na Haile Selasie iliyopo wilaya ya Kinondoni Dar es Salaam, wanadaiwa kumuua Lotter.