Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza, imewafukuza kazi watumishi wawili baada ya kutiwa hatiani na Mahakama kwa wizi wa dawa katika hospitali ya Wilaya hiyo zenye thamani ya Milioni 88 pamoja na kupokea rushwa zaidi ya Shilingi 100,000.
Akiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya tatu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Joshua Manumbu, amesema kuwa watumishi waliofukuzwa kazi ni pamoja na aliyekuwa Mtumishi wa Maabara katika hospitali hiyo Baraka Bima, ambae alikiri Mahakamani kuhusika na wizi wa dawa hizo na Mtendaji wa Kijiji cha Bukonyo Sabato Mashauri, aliyepatikana na kosa la kuomba rushwa kiasi cha shilingi laki moja na elfu hamsini.