Tume ya Uchaguzi nchini Uganda inaendelea kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Januari 14. Kwa mujibu wa matokeo yaliyotolewa usiku wa kuamkia leo, rais aliyeko madarakani, Yoweri Museveni anaongoza kwa asilimia 61.98.
Mpinzani Mkuu wa Museveni, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine mgombea wa urais kwa tiketi ya chama cha NUP amepata asilimia 30.91.
Wagombea wengine wa urais hawajafikisha hata asilimia tano ya kura ambazo tayari zimehesabiwa. Hata hivyo, matokeo ya ngome kuu za Bobi Wine maeneo ya mji mkuu, Kampala pamoja na wilaya jirani bado hayajatangazwa.
Matokeo rasmi ya uchaguzi wa urais yanatarajiwa kutolewa leo saa kumi kamili jioni. Matokeo hayo yanatangazwa wakati ambapo bado makaazi ya Wine yamezingirwa na askari wa usalama, huku huduma ya mtandao wa intaneti ikiwa haijarejea hadi sasa. Wine anaendelea kushikilia msimamo wake kuyapinga matokeo hayo.