Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Dk.Festo Dugange, amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuboresha kiwango cha mikopo inayotolewa na Halmashauri kwa kuzisimamia Halmashauri kutekeleza Sheria ya Mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu.
Dk.Dugange ameyasema hayo bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti maalum(CCM), Dk.Pindi Chana ambaye alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kuboresha kwa kutoa viwango vikubwa zaidi vya mikopo kwa vikundi mbalimbali.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Dugange amesema maboresho hayo pia ni kuzijengea uwezo Kamati za Huduma za Mikopo za Kata na Halmashauri ili ziwe na ujuzi wa kutosha wa kuanzisha na kuendeleza Vikundi vya wajasiriamali pamoja na ujuzi wa kusimamia utoaji na urejeshwaji wa mikopo.
Pia amesema kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wanufaika wa mikopo kabla ya utoaji wa Mikopo kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na kuzielekeza Halmashauri kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato.