Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imetambulisha rasmi kampeni yake ya ‘Shinda Mechi Zako Kinamna Yako na NBC Shambani’ wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma ikilenga kuchochea kasi ya uzalishaji wa zao la kahawa wilayani humo kupitia huduma zake mahususi na zenye upendeleo kwa wakulima wa zao hilo.
Ikitambulishwa kwa mara ya kwanza, kampeni hiyo inakwenda sambamba na mafunzo ya huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo ikiwemo huduma bima ya mazao na bima za afya, uwakala, huduma za kidigitali, mikopo ya zana za kilimo na pembejeo.
Huduma nyingine ni pamoja ujenzi wa maghala pamoja na kuwasaidia wakulima shughuli mbalimbali zinazohusiana na maandalizi ya msimu wa kilimo na masoko ya mazao yao.
Hafla ya utambulisho wa huduma hiyo imefanyika leo wilayani Mbinga, ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Kisare Makori ikihudhuriwa na viongozi wengine waandamizi wa mkoa huo pamoja na wadau mbalimbali wa zao hilo wakiwemo viongozi wa vyama vya ushirika na wakulima.
Mkuu wa Kitengo cha Mikakati wa Benki NBC, Msafiri Shayo alimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Theobald Sabi kwenye tukio hilo.
Akizungumzia hatua ya benki hiyo Makori pamoja na kuipongeza kwa kutoa kipaumbele kwa wakulima nchini kupitia huduma zake, alisema ujio wa kampeni hiyo wilayani mwake ni ukombozi muhimu kwa wakulima wa kahawa wanaohitaji upendeleo maalum wa huduma za kifedha na kwamba serikali imejipanga kuhakikisha dhamira ya benki hiyo inafanikiwa.
“Zaidi nimefurahi kusikia kwamba kupitia kampeni hii wakulima wanaweza kupata mikopo ya vitendea kazi muhimu kama vile matrekta na zana nyingine za kisasa za kilimo, pembejeo za kilimo na mikopo ya malipo ya awali kwa wakulima.
“Pia huduma za bima za afya na kilimo zinazohamasishwa na NBC kupitia kampeni hii ni muhimu sana kwa wakulima, hasa katika kukabiliana na changamoto za kiafya kwa wao binafsi na familia zao na kujilinda dhidi ya hasara zitokanazo na majanga ya asili ambayo yamekuwa yakiathiri mazao yao,” alisema.
Aidha, Makori alionyesha kuvutiwa pia na uwepo wa zawadi zenye thamani ya zaidi ya milioni 30 ambazo zitatolewa kwa wakulima watakaoshinda droo mbalimbali baada ya kufungua akaunti ya NBC Shambani na kuweka pesa zao za mauzo ya kahawa.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Msafiri alisema kampeni hiyo ni sehemu ya muitikio wa benki ya NBC kufuatia wito wa Serikali wa kuchangia katika kufanikisha agenda 10/30 inayolenga kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo kutoka asilimia 5 hadi 10 ifikapo mwaka 2030.
“Sambamba na uzinduzi wa kampeni hii kwa wakulima wa zao la kahawa wilayani Mbinga, pia tunatoa huduma mbali mbali kwa wakulima ikiwemo, ufunguaji wa akaunti za wakulima, ambazo hazina makato ya mwezi, huduma za mikopo kwa mkulima mmoja mmoja kwa ajili ya zana za kilimo kama matrekta na mikopo kwa vyama vya ushirika (AMCOS/Union) kwa ajili ya pembejeo na malipo ya awali kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani,” Alitaja.
Kupitia kampeni hiyo benki ya NBC inatoa huduma za bima ya afya na huduma za bima ya kilimo kwa wakulima hatua inayotoa fursa kwao kulipwa fidia pindi mazao yao yatakapoathiriwa na majanga mbalimbali yakiwemo yale ya asili.
Akifafanua zaidi kuhusu kampeni hiyo, Mkuu wa kitengo cha Wateja wadogo wadogo, Lariba na Wakulima, Benki ya NBC, Raymond Urassa alisema inawalenga wakulima wote wakiwemo mmoja mmoja, vyama vya ushirika na vyama vya msingi vya mazao ambao watapitisha fedha za mauzo kwenye akaunti zao za NBC Shambani.
“Kupitia kampeni hii wakulima wataweza kujishindia zawadi za vitendea kazi mbali mbali kama vile ‘spray pumps’ (pampu ya kupulizia kahawa) na piki piki. Upande wa AMCOS na UNION watapata fursa ya kujishindia kompyuta mpakato (laptop) na pikipiki.” Alitaarifu.
Akizungumza kwa niaba wakulima hao, Loveness Kapinga, Katibu wa AMCOS ya Nahongo wilayani pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa kampeni hiyo muhimu,alionyesha kuvutiwa na huduma za bima za afya na bima za kilimo kutokana na hitaji kubwa walilonalo wakulima hao upatikanaji wa huduma za afya.
Aidha, Kapinga aliiitaja huduma ya bima ya kilimo kama suluhisho sahihi dhidi ya athari zitokanazo na majanga mbalimbali yanayoathiri mazao yao.
Hii ni mara ya kwanza kwa kampeni ya NBC Shambani kuingia mkoa wa Ruvuma, huku ikiwa tayari ina misimu zaidi ya mitatu katika mikoa mingine kama vile Mtwara na Lindi ambapo benki hiyo iliadhimia kuweka msisitizo wa kuwainua kiuchumi wakulima mmoja mmoja na vyama vya ushirika vya mazao ya korosho, mbaazi na ufuta.
Mwisho.