Mahabusu zaidi ya 15 wa gereza la Segerea, jijini Dar es Salaam wanaokabiliwa na kesi za kusafirisha na kuingiza dawa za kulevya nchini, wanadaiwa kugoma kula wakilalamikia kusota gerezani kwa muda mrefu huku kesi zao zikiendeshwa muda mrefu bila kumalizika.
Mahabusu hao ambao waligoma kwa siku tano hadi jana wanalalamika kwamba, wamecheleweshewa haki zao zaidi ya miaka minne tangu wafunguliwe mashitaka na Jamhuri.
Kwa mujibu wa barua ya mahabusu hao, wanailalamikia Jamhuri kwa kuwasotesha zaida ya miaka minne wakati kesi zao zilikuwa kwenye hatua ya kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri na utetezi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) aliwafutia mashitaka na kuwafungulia upya mashitaka yale yale katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Mbali na mgomo wa kula, barua hiyo imeeleza kwamba, baadhi yao wamejishona midomo kwa sindano na kwamba bwana jela wa gereza hilo anawatembezea mkong’oto ili wasiendelee na mgomo huo.
Pamoja na mambo mengine, watuhumiwa hao wanalalamika kwamba hawaruhusiwi kupelekewa chai, sukari, majani ya chai, vitumbua, maandazi na vitu vingine kwa mahitaji yao.
“Tumeamua kugoma kula chakula, tumechoka kusota mahabusu zaidi ya miaka minne sasa kesi zetu zilifikia hatua ya kufunga
Msemaji wa Jeshi la Magereza nchini, Deodatus Kazinja, kuzungumzia madai hayo, lakini alisema kwa sasa yuko kwenye mafunzo, hivyo hawezi kuzungumza chochote.
“Niko kwenye mafunzo, siwezi kuzungumzia suala hilo wasiliana na Mkuu wa Magereza wa mkoa,” Kazinja.
NIPASHE
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, ameondoka nchini kuelekea Marekani kwa ziara ya kikazi.
Mkuu wa Mambo ya Nje Chadema, Deogratias Munishi, alisema jana kuwa Dk. Slaa ambaye aliambatana na mkewe, Josephine Mushumbusi, waliondoka juzi na watakuwa Marekani kwa ziara ya siku tisa.
Alisema ziara hiyo inafuatia mwaliko wa Gavana wa Jimbo la Indiana, Mike Pence, pamoja na taasisi mbalimbali za nchini humo vikiwamo vyuo vikuu kutokana na kutambua mchango wa kisiasa na kijamii wa Dk. Slaa na chama chake katika maendeleo ya Bara la Afrika.
Munishi alisema ziara hiyo itamwezesha Dk. Slaa kushiriki mijadala mbalimbali inayohusu uwekezaji, elimu na uongozi iliyoandaliwa kwa ajili yake ambayo lengo lake kuu ni kuitangaza Tanzania.
Alisema akiwa Marekani, Dk. Slaa atafanya mihadhara kwenye vyuo vikuu vya Purdue, Indiana na Marion.
Aliongeza kuwa Dk. Slaa pia atakua na vikao vya mashauriano na baadhi ya wahadhiri wa vyuo vikuu mbalimbali kwa lengo la kubadilishana uzoefu juu ya masuala ya kisiasa na maendeleo na kijamii na ushiriki wa Chadema katika siasa za kimataifa.
Alisema ziara hiyo itamkutanisha Dk. Slaa na viongozi na watendaji wakuu wa kiserikali wa Jimbo la Indiana, kampuni na taasisi kubwa za uwekezaji kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika masuala ya uchumi na uwekezeji barani Afrika.
MTANZANIA
Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ameeleza kushangazwa na hatua ya Serikali kuwapatia kazi ya ujenzi wa Bandari ya Mwambani mkoani Tanga watuhumiwa wa sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.
Amesema watuhumiwa hao wamepewa kazi hiyo kupitia Mradi wa Mwambani Economic Corridor (MWAPORC), ambao utagharimu Sh trilioni 54, huku kukiwa hakuna taratibu za utangazaji wa zabuni zilizofuatwa na Serikali.
Kauli hiyo aliitoa jana alipokuwa akihutubia mikutano ya hadhara iliyofanyika katika miji ya Mafinga na Iringa mkoani hapa ambapo alisema Serikali imeipa kazi ya ujenzi Kampuni ya VIP Engineering and Management inayomilikiwa na James Rugemalira ambaye anahusika katika sakata la Escrow.
Zitto alisema ACT-Wazalendo wanamtaka Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta afanye uchunguzi kuhusu mradi huo wa Mwambani na achukue hatua kwa kile alichodai kuwa utapeli wa watu wa Escrow.
“Taratibu hazijafuatwa, hakuna zabuni iliyotangazwa kuhusu Bandari ya Mwambani, miradi mikubwa kama hii Serikali hutakiwa kutoa ‘guarantee’ kwa mikopo ambayo inachukuliwa.
“Hivyo kuhusika kwa Rugemalira wa Escrow na mwanasheria Cathbert Tenga wa Richmond kwenye mradi huu ni mwendelezo wa miradi ya kitapeli,” Zitto.
Zitto ambaye pia alikuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema uzito wa mradi huo wa bandari unakwenda sambamba na reli ambayo itafika hadi Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).
Akitoa taarifa kuhusu mradi huo hivi karibuni, msimamizi wa mradi huo ambaye pia ni Mwanasheria mashuhuri nchini, Cathbert Tenga, alisema utamilikiwa na Watanzania wenyewe na si watu kutoka nje ya nchi kama ilivyo katika miradi mingine.
MTANZANIA
Shule mbalimbali za sekondari za bweni zinazomilikiwa na Serikali zimefungwa kutokana na kukosa chakula.
Uchunguzi umebaini takribani kwenye mikoa yote kuna shule zimefungwa na nyingine ziko hatarini kufungwa kwa kukosa chakula.
Mkoani Dodoma Shule ya Sekondari Mpwapwa iliyopo katika Wilaya ya Mpwapwa ilitakiwa kufunguliwa tangu Aprili 8, lakini imeshindikana kutokana na ukosefu wa chakula.
Mkuu wa shule hiyo, Nelson Mbilinyi, alisema walifunga shule kwa ajili ya likizo fupi, lakini hadi sasa hawajajua ni lini watafungua kutokana na tatizo hilo.
Mkoani Tabora, shule nne zimefungwa kutokana na wazabuni kusitisha huduma kutokana na kuidai Serikali zaidi ya Sh bilioni 1.5 za chakula walichokisambaza kwa shule mbalimbali.
Sekondari zilizofungwa ni Kazima ambayo wanafunzi wote wamerudishwa makwao isipokuwa wale wa kidato cha sita ambao wamepewa maelekezo ya kuwa wavumilivu kwani watabaki wakijiandaa kwa ajili ya kufanya mitihani.
Shule nyingine iliyofungwa ni Sekondari ya Tabora Boys ambapo kwa mujibu wa mwalimu ambaye hakutaka kutaja jina lake, wanafunzi wote wamerudishwa majumbani kwao na kubakishwa wa kidato cha sita tu wanaojiandaa kwa mitihani yao ya mwisho.
Sekondari nyingine ambazo pia zimefungwa kutokana na kadhia hiyo mkoani humo ni pamoja na Milambo na Tabora Girls ambazo idadi ya wanafunzi waliorudishwa makwao haijafahamika.
Katika Mkoa wa Mtwara, taarifa zinasema shule za sekondari zilizopo wilayani Masasi tayari zimefungwa kutokana na hali hiyo.
Shule hizo zimetajwa kuwa ni Ndanda Boys, Masasi Girls, Chidya na Ndwika.
Katika Mkoa wa Mwanza, wazabuni wa vyakula mashuleni wametishia kugoma kutokana na Serikali kushindwa kulipa deni la Sh milioni 800.
Shule ya Sekondari Mwanza, iliyopo katika Wilaya ya Nyamagana inadaiwa na mzabuni kiasi cha Sh milioni 116, ambazo ameshindwa kulipwa kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo.
Shule nyingine ambazo zinadaiwa na wazabuni ni Sekondari ya Nsumba pamoja na Ngaza, ambapo taarifa za uhakika zinaeleza kuwa kwa ujumla wake zinadaiwa zaidi ya Sh milioni 300.
Mkoani Arusha nako hali si shwari baada ya shule za Ilboru, Longido, Engutoto, Makuyuni na Kisimiri kudaiwa kuwa katika hali mbaya kutokana wazabuni kudai mamilioni ya fedha.
Mkoani Mbeya, Shule ya Sekondari ya Iyunga, inatarajiwa kufungwa leo, kutokana na ukosefu wa chakula.
Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Edward Mwakimwa, alikiri kukabiliwa na uhaba wa chakula na kusema tayari uongozi wa shule kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa unaendelea na mchakato wa kuhakikisha chakula kinapatikana kwa wakati.
MTANZANIA
Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema Watanzania waishio ughaibuni hawataweza kupiga kura wakiwa nje ya nchi wakati wa Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Alisema pamoja na kwamba Watanzania hao wanatakiwa kupiga kura wakati wa uchaguzi huo, jambo hilo halitawezekana kwa sababu kuna mambo kadhaa ambayo Serikali inabidi iyatekeleze kabla ya uchaguzi huo.
Waziri Mkuu Pinda alitoa kauli hiyo jana kwenye makazi ya Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Peter Kallaghe, wakati akizungumza na baadhi ya Watanzania waishio nchini humo.
Akizungumza na Watanzania hao ambao baadhi yao walitoka miji ya Leicester na Manchester, alisema mambo makuu ambayo yanahitaji kuzingatiwa kabla hawajaweza kupiga kura ni pamoja na marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi namba moja ya mwaka 1985 pamoja na uandikishwaji wa Watanzania wana-Diaspora kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura.
“Najua suala kubwa ambalo mnatamani kulisikia ni hili la Watanzania kuweza kupiga kura kutokea huku mliko.
Hili inawezekana lisifanikiwe wakati huu kwa sababu kuna mambo muhimu ya kuzingatia, kubwa likiwa ni marekebisho ya sheria na hili zoezi la uandikishaji wa wapigakura kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi wanaamini kwamba jambo hilo linaweza kufanikiwa kwenye uchaguzi wa mwaka 2020.
MWANANCHI
Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amemwomba Rais Jakaya Kikwete kuvikemea vyombo vya dola vinavyomfuatafuata vikihoji mambo binafsi na kwamba akishindwa kufanya hivyo itakuwa wazi kwamba yeye ndiye anawatuma.
Akihubiri mamia ya waumini wa kanisa hilo jana, Gwajima alisema amekuwa akifuatwafuatwa na vyombo vya Serikali utadhani yeye si raia wakati ni Mtanzania halisi.
“Rais Kikwete tafadhali namuomba awakemee watu hawa… asipowakemea, basi kanisa langu litajua kwamba yeye ndiye anayewatuma,” alisema Gwajima huku akishangiliwa na waumini waliokuwa wakimsikiliza.
Huku wakinyeshewa na mvua, waumini hao walikuwa wakimsikiliza Askofu Gwajima, siku tatu baada ya kiongozi huyo kuhojiwa kwa mara ya pili na polisi na kutakiwa awasilishe mambo 10 yanayohusiana na usajili wa kanisa, uongozi na mali zake.
“Mimi ni Mtanzania halisi acheni nifanye kazi ya Mungu, kama mnadhani mimi si Mtanzania, basi mmepotoka kwani kwa hilo mtashindwa,”.
“Madaktari, wanasiasa, wafanyabiashara wamekuwa wakitoa misimamo yao lakini hawabughudhiwi iweje Gwajima tu? Nitaendelea kuwapa vidonge vyenu kila mtakapopotoka, nafanya kazi ya bwana,” .
Gwajima alisema amekuwa akishangazwa na vyombo vya Serikali vinavyohoji utajiri alionao bila kujua anaongoza idadi gani ya waumini.
Alisema anaongoza kanisa lenye waumini zaidi ya 70,000 ambao ni kama watoto wake na kwamba yeye ni baba yao wa kiroho.
“Waumini hawa mimi ni baba yao wa kiroho, nikiwaomba kila mmoja anipe Sh1,000 tu nitakuwa na Sh70 milioni, halafu mnahoji utajiri ninaupata wapi?” alisema na kisha kuwauliza waumini hao… “Hivi baba yenu nikiwaomba kila mmoja anipe Sh1,000 mtanipa au mtaninyima?”
MWANANCHI
Watu 18 wameteketea kwa moto baada ya basi la Kampuni ya Nganga Express na lori aina ya Fuso kugongana uso kwa uso na kuwaka moto katika eneo la Iyovi, Milima ya Uduzungwa, Morogoro
Katika ajali hiyo iliyotokea jana saa mbili asubuhi, abiria 15 waliokuwa kwenye basi na wengine watatu wa lori waliteketea kwa moto huku wengine 10 wakijeruhiwa vibaya.
Taarifa na picha za ajali hiyo zilianza kusambaa jana asubuhi kupitia mitandao ya kijamii zikionyesha masalia ya miili ya walioteketea.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul alisema ajali hiyo ilitokea baada basi hilo lililokuwa linatoka Kilombero kwenda Mbeya likiwa kwenye mistari ya barabarani ya katazo na kwenye mwendo kasi kugongana na lori lililokuwa limebeba matikiti na kuwaka moto.
Alisema majeruhi wanne wamelazwa katika Hospitali ya St. Kizito, Mikumi na sita wako katika Hospitali ya Mtandika, Iringa.
Alisema kwenye basi hilo kulikuwa na pikipiki ambayo pia iliungua na kusema inawezekana ndiyo iliyosababisha moto huo.
Ajali hiyo ni mfululizo wa ajali zinazotokea katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni siku moja baada ya watu watano kufariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mikoa ya Dodoma na Iringa saa 36, baada ya kumalizika mgomo wa madereva nchini.
HABARILEO
Watanzania wengi wametajwa kuingia na kuishi nchini China kinyemela na kusababisha wanapopata matatizo yanayohitaji msaada wa serikali kushindikana kupewa, kwa kuwa hawamo katika utaratibu wa Diaspora.
Balozi wa Tanzania nchini China, Abdulrahman Shimbo alisema lipo tatizo kubwa kutokana na Watanzania wengi kuingia kinyemela kuishi, wakifanya biashara zisizo na vibali na wengi wao ni mama lishe na wafanyabiashara ndogo.
Aidha, amehadharisha juu ya Watanzania kujikuta wakisoma kwenye vyuo visivyo na ubora nchini hapa kwa kutaka wanaosoma vyuo vikuu mbalimbali wasaidie kutoa taarifa muhimu.
Shimbo alisema hayo jana alipozungumza na viongozi wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Tanzania Beijing (TZSUB) katika kikao cha makabidhiano ya uongozi mpya na utoaji vyeti kwa Tume ya Uchaguzi ya Jumuiya hiyo.
Kikao hicho kilifanyika ubalozini na uchaguzi ulifanyika Aprili 5, mwaka huu ubalozini pia. Akizungumzia Watanzania wanaoingia kinyemela China, Shimbo alisema, “Wanaishi hapa, hawakamatwi ingawa hawana nyaraka muhimu, kwa kuwa wengi wao wanasaidiwa na Wachina wenyewe wasio waadilifu.
“Wengi ni mama lishe, wakipata shida sasa wanaanza kuitafuta serikali, unaanzia wapi kumsaidia mtu wa aina hii, ni shida na suala la vibali kwa wenzetu hapa wapo makini kweli kweli.”
Alitaja miji yenye tatizo hilo kwa kiwango kikubwa ni Guangzhou na Hong Kong.
Aliwataka Watanzania kujiandikisha ubalozini wanapofika nchini hapa na pia kuhakikisha wana vibali muhimu vya kuwawezesha kuishi ugenini.
Kuhusu masuala ya elimu, Balozi aliwataka wanafunzi Watanzania wanaosoma katika vyuo vikuu mbalimbali nchini hapa, kusaidia taasisi za elimu na wizara kutoa taarifa muhimu kuhusu vyuo nchini hapa kusaidia kupunguza wimbi la watu wanaotumia vibaya nafasi hiyo kuwapotosha watu na kujikuta wanasoma katika vyuo visivyo na ubora.
“Wasaidieni nyumbani kujua vyuo bora, kuna watu wanakuja hapa wanasoma miaka minne lugha, hawana hati wala maendeleo yao hayajulikani.
HABARILEO
Jumla ya walimu wa shule ya msingi 18,000 kutoka mikoa 14 nchini, leo wanaanza mafunzo yenye kulenga kuwajengea uwezo wa kufundisha Mtaala mpya wa Elimu ya Msingi Darasa la I na la II.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na kufadhiliwa na Ushirika wa Kimataifa wa Maendeleo ya Elimu (Global Partnership for EducationGPE).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Jumanne Sagini mafunzo hayo yatatolewa kwa awamu nne kuanzia leo. Mtaala huo umetengenezwa na Serikali kwa lengo la kukuza stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).
Taarifa hiyo kwa vyombo vya habari, imesema mafunzo hayo yatatolewa pia kwa walimu ambao watawezesha ufundishaji na ujifunzaji wa KKK kwa watoto walio katika vituo vya elimu nje ya mfumo rasmi.
Kwa mujibu wa taarifa awamu ya kwanza itaanza Aprili 13 hadi 21; Awamu ya pili Aprili 27 hadi Mei 6; awamu ya tatu kuanzia Mei 11 hadi Mei 20 na awamu ya nne itakuwa Mei 25 hadi Juni 3, mwaka huu.
Walimu 4,430 kutoka mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Tanga, Singida, Rukwa, Ruvuma, Morogoro na Pwani watashiriki mafunzo katika awamu ya kwanza.
Walimu 4,492 watashiriki mafunzo katika awamu ya pili kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Manyara, Simiyu, Katavi, Geita, na Mwanza na walimu 9,078 watashiriki katika awamu ya tatu na ya nne ya mafunzo hayo.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza>>>twitter Insta Facebook