Madaktari katika maeneo yaliyonufaika na bajaji za kubebea wagonjwa, wamelazimika kuwa madereva wa kuziendesha baada ya Serikali kushindwa kuajiri madereva.
Mganga Mkuu wa hospitali ya Dodoma Dk. Ezekiel Mpuya alisema Mkoa wa Dodoma ulifanikiwa kupata bajaji 10 na kila Wilaya ilipatiwa mbili lakini zote hazina madereva.
Dk Mpuya alisema madaktari hao licha ya kuziendesha bajaji hizo hukumbana na changamoto ya ubovu wa barabara unaowapa wakati mgumu pindi wanaposafirisha wagonjwa wanaopatiwa rufaa kwenda hospitali ya Mkoa wa Dodoma.
“Wakati mwingine huwa zinafia njiani kutokana na ubovu wa barabara, kwa upande mwingine naweza kusema sio msaada sahihi ” Dk Mpuya.
Ameiomba Seikali kuzipatia uwezekano wa magari ya wagonjwa hospitali hizo ili kuepuka adha wanayokumbana nayo sasa.
MWANANCHI
Uwezekano wa Kura ya Maoni kufanyika mwaka huu na hasa sambamba na Uchaguzi Mkuu, umeanza kujionyesha baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza zabuni za ununuzi wa vifaa vitakavyotumika kwenye shughuli hiyo, zikiwamo karatasi za kupigia kura.
Kati ya matangazo hayo mawili, moja litakamilisha mchakato wa upokeaji maombi ya zabuni Mei 11, mwaka huu na nyingine kufungwa siku tisa baadaye.
“Serikali ya Tanzania imetenga fedha kwa ajili ya uendeshaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika mwaka wa fedha 2014/15. Imepanga kuwa sehemu ya fedha hizo zitatumika kugharamia ununuzi wa vifaa mbalimbali na huduma zisizo za kishauri kwa ajili ya Kura ya Maoni 2015,” inasomeka sehemu ya tangazo hilo.
Katika matangazo hayo, NEC imetoa zabuni sita tofauti zitakazojumuisha ununuzi wa fulana na kofia, ununuzi wa bahasha zisizoweza kuchakachuliwa, uchapaji na uchapishaji wa karatasi za kupigia Kura ya Maoni.
Wazabuni hao pia watatakiwa kutoa huduma mchanganyiko zinazojumuisha vifaa vya ofisini, vifaa vya kuhifadhia nyaraka na vitu mbalimbali pamoja na taa za chemli.
Pia, wataiuzia NEC chemba za kupigia kura, wino maalumu, lakiri za masanduku ya kura na betri.
Vilevile, Tume inataka wazabuni kufanikisha ununuzi wa kompyuta, skana, printa, modemu, projekta na mashine za kunakili.
Huduma nyingine zinahusisha ununuzi wa vifaa mbalimbali vinavyotumika katika printa na mashine za kunakili.
Katika tenda nyingine, NEC inatafuta kampuni itakayotoa huduma za kukodisha malori na magari madogo yenye uwezo wa ‘four wheel’ kwa ajili ya kubebea vifaa vya Kura ya Maoni katika kata mbalimbali.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva alisema pamoja na maandalizi hayo, hadi sasa hakuna tarehe maalumu iliyokubaliwa kufanyika kwa Kura ya Maoni na kwamba nguvu zote zimeelekezwa kwenye uboreshaji wa Daftari la Wapigakura kwa kutumia teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR).
MWANANCHI
Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema amedai kuwa serikali iliyopo madarakani imeshindwa kazi kutokana na mawaziri na watendaji wengine kumwachia majukumu yote Rais Jakaya Kikwete.
Akizungumza wakati wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa chama hicho uliofanyika Dar es Salaam jana, Mrema alisema kuna mambo mengi ya ajabu yanayojitokeza katika ofisi za Serikali yanayokatisha tamaa wananchi.
Mrema alisema karibu kila sekta ikiwamo ya ulinzi na usalama, zinayumba na mbaya zaidi wasaidizi wa Rais bado hawajaweza kufanya kitu chochote kuikabili hali hiyo.
“Nchi inaelekea kubaya, kuna matatizo mengi ya kiusalama ambayo hayana majibu, kuna masuala ya ugaidi, udini, mauaji ya albino, uvamizi, uporaji wa silaha na mauaji katika vituo vya polisi,” .
Mrema aliyataja matukio mengine kuwa ni migomo ya madereva na wafanyabiashara na alisema yote hayo yanatokea, hakuna kiongozi hata mmoja ambaye amejitokeza kuyashughulikia kikamilifu, kila mmoja anasubiri Rais Kikwete aseme neno au achukue hatua.
MTANZANIA
Mwili wa mwanafunzi wa kidato cha pili katika Sekondari ya Matuo, Manyara anayedaiwa kufariki baada ya kuchapwa viboko na walimu wake Emmanuel Mbigima umefikishwa katika hospitali ya rufaa ya Dodoma kwa uchunguzi.
Wakati mwili huo unafikishwa hospitalini hapo jana ulikuwa umewekwa kwenye gari la Halmashauri ya Kiteto ukisindikizwa na baadhi ya ndugu wa karibu wa familia ya marehemu.
Baba wa marehemu Emmanuel Ngowi alisema mwili huo umeletwa hospitalini hapo ili kufanyiwa vipimo ambavyo vimekosekana katika hospitali ya Kiteto.
“Hata hivyo majibu ya awali yaliyotolewa hospitali hapo yalionyesha jicho la kulia limevilia damu, pia alikutwa na michubuko miguuni” Ngowi.
Naye Mjomba wa marehemu Michael Ngowi alisema matukio ya wanafunzi kupigwa hadi kufariki yamekuwa yakitokea shuleni hapo kila mara kutokana na wahusika kutochukuliwa hatua yoyote.
MTANZANIA
Mwanasiasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mapinduzi ya Zanzibar, Nassor Hassan Moyo amesema hafikirii kujiunga na chama chochote cha siasa, baada ya kuvuliwa uanachama wa CCM.
Wiki iliyopita, Katibu wa CCM Mkoa wa Magharibi Unguja, Aziza Iddi Mapuri alitangaza kumfukuza mwanasiasa huyo mkongwe kwa madai ya kukisaliti kwa kukiuka maadili na kutoa matamshi yasiyokubaliana na sera za chama chake.
Moyo alisema umri wake haumruhusu kujiunga na chama chochote cha siasa, lakini ataendelea kuitetea Zanzibar.
“Sina mpango wa kujiunga na chama chochote cha siasa kwa sababu umri wangu hauruhusu, nitaendelea kuungana na wale wote wanaopenda maendeleo ya Zanzibar na wale wanaounga mkono muundo wa serikali tatu, nitashirikiana nao vyovyote iwavyo,”a Moyo.
Mzee Moyo aliyepata kushika nyadhifa mbalimbali, alisema tatizo kubwa linaloisumbua CCM ni kwamba hakitaki kukosolewa jambo ambalo wanadhani linawapa nguvu wapinzani.
“CCM wanadhani nchi hii ni yao, kumbe ni ya Tanganyika na Zanzibar. Fikiria kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Warioba, tulipeleka maoni yetu ya kamati ya maridhiano na baadaye tukaiunga mkono, lakini Rais Dk.Ali Mohamed Shein aliwahi kusema haitambui kamati yetu.
“Hatuna shida na Rais Shein, bali tuna shida na wananchi tu na si lingine. Sasa wamenifukuza lakini nitaendelea kutetea maoni ya wananchi,”alisema.
Akizungumzia alivyoshiriki mkutano wa Chama cha Wananchi (CUF), alisema hakuibuka tu, bali alialikwa kama mwenyekiti wa kamati ya maridhiano.
HABARILEO
Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge juzi aliokolewa kwa risasi katika vurugu za kundi la wananchi, waliomvamia karibu na ofisi za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Simiyu na kusababisha taharuki katika ofisi za chama hicho.
Mmoja wa watu waliokuwa kwenye gari la mbunge huyo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliyekuwa na msafara wake kutekeleza shughuli za ubunge jimboni mwake, ndiye aliyefyatua risasi hewani ili kutawanya umati huo.
Hata hivyo, hali hiyo ilitafsiriwa na Chadema kuwa ni mkakati wa mbunge huyo wa kuwafanyia fujo katika ofisi zao, hivyo kulifikisha suala hilo Polisi ambako wamefungua jalada.
Madai ya tukio hilo yaliyotolewa na John Heche, Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA), yamethibitishwa Jeshi la Polisi ambalo limesema aliyefyatua risasi si Chenge, bali mmoja wa watu waliokuwa kwenye gari lake.
Heche alisema tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 1:30 jioni katika ofisi za chama hicho mkoa wa Simiyu zilizoko eneo la Salunda.
“Mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa chama hicho uliohutubiwa na Naibu Katibu Mkuu Chadema Tanzania Bara, John Mnyika baadhi ya wanachama walipanda magari na wengine kutembea kwa miguu ili kwenda kwenye ofisi zao za mkoa ambako watu walishtuka kumuona mbunge huyo akishuka katika gari lake,” Heche.
“Kutokana na kitendo hicho, mmoja wa walinzi wa Chadema aliwaomba waondoke eneo hilo na pia waache kupiga muziki huo kwani kuna kikao cha ndani cha viongozi wa chama hicho kinachoendelea lakini waligoma.
Kutokana na hali hiyo, viongozi wa Chadema mkoa wa Simiyu waliripoti tukio hilo Makao Makuu ya Polisi wilaya ya Bariadi na kutoa malalamiko yao juu ya tukio hilo .
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Gemini Mushi alikiri kutokea kwa tukio hilo, lakini alisema kuwa aliyefyatua risasi si Chenge, bali ni kijana Ahmed Ismail aliyekuwa katika gari la Mbunge huyo, ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa zamani na Waziri aliyeziongoza wizara kadhaa, zikiwemo Katiba na Sheria na Miundombinu.
HABARILEO
Uchaguzi wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) mkoa wa Simiyu uliofanyika jana, nusura uvunjike baada ya baadhi ya wagombea, kuanza kutuhumiana ndani ya ukumbi wakati wakijieleza kwa wajumbe.
Mmoja wa wagombea hao ambaye alikuwa akigombea nafasi ya Uwakilishi wa Kamati Tendaji Taifa, Chananja Buluba alipopewa nafasi ya kujieleza, alidai kuwa uchaguzi huo umegubikwa na vitendo vya rushwa.
Alidai kuna baadhi ya wajumbe walipewa Sh 50,000 hadi Sh 100,000 kutoka kwa wagombea wa nafasi za Uwakilishi wa Kamati Tendaji Taifa, Mwenyekiti na Mweka Hazina.
Akiwa anazomewa na baadhi ya wajumbe hao, mgombea huyo alieleza kuwa mbali na kupewa fedha, baadhi ya wajumbe walilipiwa sehemu za kulala kwa siku tatu pamoja na chakula.
Hali hiyo ilionekana kuwakera wajumbe wa uchaguzi huo na kumtaka athibitishe mbele yao na kuwataja watu ambao walipewa pesa, kulipiwa sehemu za kulala pamoja na chakula.
Akiwa tayari kutaka kuwataja wahusika wa vitendo hivyo, mgombea huyo alizuiliwa na Mratibu wa Uchaguzi huo ambaye ni Katibu wa CWT mkoani hapa, Fatuma Bakari kwa madai kuwa alikuwa amekiuka taratibu za uchaguzi.
Kitendo cha kuzuiliwa na katibu huyo, kilionekana kumkera mgombea huyo na kuacha kujieleza mbele za wajumbe hao, ambapo aliamua kuwaita waandishi wa habari nje ya ukumbi wa mkutano ili kuwaeleza hali hiyo.
“ Nimechukia sana kitendo cha Mratibu ambaye ni Katibu CWT Mkoa kunizuia…hali ya uchaguzi huu imechafuliwa sana na rushwa, wagombea wamegawa pesa kama karanga na sijui wametoa wapi wakati wao ni walimu kama mimi,” Buluba.
Alibainisha kuwa pesa walizokuwa wakizitoa wagombea hao, zilikuwa na ufadhili kutoka katika vyama vikubwa vya siasa, alivyovitaja.
NIPASHE
Chama cha Tanzania Labour (TLP), kimefanya mkutano mkuu wa uchaguzi huku mwenyekiti wake wa Taifa, Augustino Mrema, akitumia muda mrefu kumshutumu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahaman Kinana na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, kwamba wanakihujumu chama hicho ili kianguke.
Alisema hayo jana wakati wa mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumchagua mwenyekiti wa Taifa na kumuidhinisha mgombea urais atakayepeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Mrema alisema Kinana alipofanya ziara katika Jimbo la Vunjo alisema uongo kwa kuwaeleza wananchi kwamba fedha za mfuko wa jimbo zilizopelekwa na serikali katika jimbo hilo kwa miaka minne ni Sh. milioni 400 wakati ni Sh. milioni 150 tu.
“CCM wameamua kuishi kwa uongo, nani atawaheshimu, nani atamuheshimu Kinana, mbona anamdhalilisha Rais Kikwete, Kinana hafai mbona tembo wanauawa na meno ya tembo yanaibwa lakini hasemi haya anakaa kimya,” alisema.
Alisema Kinana anashangaza Watanzania kwani katika ziara zake hazungumzii viongozi waliokula fedha za akaunti ya Tegeta Escrow badala yake anaiandama TLP na Mrema na kwamba hata akifanya hujuma hizo kamwe hataweza kuangushwa katika jimbo la Vunjo.
“Kinana anatukana mawaziri Rais amekaa kimya hamkemei, Kinana anatumia fedha nyingi kunichafua na sijui kama ni fedha halali, Rais usinyamaze watu wa Vunjo hawatakubali kuona hujuma zinazofanywa na Kinana dhidi ya TLP,” alisema.
Mrema alisema kutokana na hali hiyo amemwandikia barua Rais Jakaya Kikwete kumlalamikia Kinana kwa kauli zake kwamba amejilimbikizia madaraka na kumuomba Rais achukue hatua.
Kuhusu Mbatia, alidai kuwa amekuwa akiendesha kampeni chafu ya kuichafua TLP ambazo zimepewa jina la ‘delete TLP’ katika jimbo la Vunjo kiasi cha kusababisha baadhi ya viongozi wa TLP kuhamia NCCR-Mageuzi.
“Kuna madiwani wa TLP ambao waliasi hadharani na wakawa wanampigia debe Mbatia na waliingia katika kampeni hiyo na walikuwa wakidai uamuzi wa kumuunga mkono Mbatia ni uamuzi wa Mungu,” alisema.
Alisema watu ambao wamekuwa wakimuombea mabaya afe ili wagombee jimbo la Vunjo wahesabu kuwa wameumia kwani hivi sasa yupo ‘fiti’ na kuwahakikisha wajumbe wa mkutano huo kwamba atagombea jimbo hilo na kuchaguliwa kwa mara nyingine tena.
Mbatia alipopigiwa simu yake ilikuwa inaita bila kupokelewa na alipotumiwa sms alijibu kuwa yupo kwenye mkutano.
“Hali ya kisiasa katika nchi si nzuri, nchi inaelekea kubaya, kuna matatizo mengi kama vile ugaidi, udini, mauaji ya albino, uvamizi wa vituo vya polisi, mauaji ya polisi na kuporwa bunduki. Sioni kiongozi anayejitokeza kukabiliana na matatizo hayo,” .
NIPASHE
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinari Pengo, amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kugombea urais, ili wananchi wapate wigo mpana wa kuchagua anayefaa kuiongoza nchi.
Kardinali Pengo alitoa wito huo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kumalizika kwa mahafali ya saba ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph Tawi la Dar es Salaam (SJUIT).
Alisema iwapo watajitokeza wagombea wengi wa urais, itawasaidia wananchi kuwafahamu wagombea wao vizuri, kuwapima kwa kulinganisha sifa zao kabla ya kuchagua mmoja kuwa kiongozi wa nchi.
Alisema kujitokeza kwa watu wengi wenye nia ya kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu ni jambo jema, kwani watakapojitokeza wachache au mmoja, wananchi wanaweza kuchagua kiongozi asiye na sifa.
“Mimi nadhani ni jambo zuri kwa watu wengi kujitokeza kugombea nafasi ya urais, akijitokeza mtu mmoja kugombea urais wananchi watashindwa kufahamu kama anafaa kwani hakutakuwa na wa kumlinganisha naye,”.
Baadhi ya makada ndani ya vyama vya siasa wametangaza nia ya kuwania nafasi hiyo na wengine wanatajwa.
Kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), makada kadhaa wamejitokeza kutangaza nia ya kumrithi Rais Jakaya Kikwete atakapong’atuka Oktoba mwaka huu.
Waliotangaza nia hadi sasa ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu; Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangalah na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye alitangaza akiwa ziarani nchini Uingereza na kueleza kuwa alifanya hivyo kimya kimya.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Prof. Mark Mwandosya na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, aliyetangazia nia hiyo nchini Uingereza.
Viongozi wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa; Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira.
Wengine ni Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli; Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta; Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro; Mbunge wa Sengerema, Willium Ngeleja na Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Kwa upande wa Tanzania Labour Party (TLP) aliyejitokeza na alitarajiwa kupitishwa na Mkutano Mkuu ulioanza jana jijini Dar es Salaam ni Macmillan Lyimo.
Vyama vya Chadema, CUF, NCCR- Mageuzi na NLD vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vimepanga kusimamisha mgombea mmoja wa urais.
Wanaotajwa katika vyama hivyo ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa na Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba.
Kadhalika, Kardinali Pengo aliwatahadharisha wananchi dhidi ya wagombea wa nafasi ya urais wanaotoa rushwa ili waingie Ikulu, kwani uongozi wa taifa hauwezi kununuliwa.
Hakuna Stori itakayokupita mtu wangu,niko tayari kukutumia wakati wowote kupitiatwitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>> twitter Insta Facebook