MWANANCHI
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imeshusha bei ya petroli kutoka Sh1,955 hadi Sh1,768 kwa lita ikiwa ni punguzo la Sh187, sawa na asilimia 9.56 kwa bei ya rejareja kuanzia leo.
Hii ni mara ya pili katika kipindi cha siku 28 kwa Ewura kushusha bei, mara ya mwisho ilikuwa Januari 7, iliposhusha kutoka Sh2,097 hadi Sh1,955 kutokana na kushuka kwa bei ya nishati hiyo katika soko la dunia.
Akitangaza bei mpya, Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi alisema bei ya petroli imeshuka sambamba na dizeli iliyoshuka kwa Sh139 na mafuta ya taa kwa Sh177. Bei ya Dizeli kwa mkoa wa Dar es Salaam ni Sh1,708 na mafuta ya taa Sh1,657.
Januari 7, bei ya petroli ilishuka kwa Sh74 kwa lita, dizeli Sh62 na mafuta ya taa Sh54.
“Bei hii inayoanza kutumika kesho (leo) inatokana na kushuka kwa mafuta hayo katika soko la dunia… Desemba mwaka jana, bei ilichelewa kubadilika katika soko la ndani kwa sababu ya mchakato wa usafirishaji:-Ngamlagosi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe na wadau wengine wamekuwa wakisema kupungua kwa bei ya mafuta katika soko la dunia hakulingani na bei za ndani.
MWANANCHI
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imesema imemhoji na inaendelea kumchunguza mmiliki mwenza wa zamani wa Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL), James Rugemalira.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah alisema vigogo wote waliohusika na sakata la uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow, ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wanachunguzwa akiwamo Rugemalira.
“Tunawachunguza wote, hatuwezi kufanya kazi harakaharaka kama zimamoto, tunakwenda hatua kwa hatua, uchunguzi ukikamilika wote watakaopatikana na hatia watapelekwa mahakamani“–Dk Hoseah.
Rugemalira akiwa mbia wa IPTL chini ya Kampuni ya VIP Engineering and Management (VIPEM), ndiye kiini cha vigogo wengi wa Serikali kupewa mgawo wa fedha kupitia Benki ya Mkombozi.
Akizungumzia suala hilo, Msemaji wa Takukuru, Doreen Kapwani alisema Rugemalira anachunguzwa na kueleza kuwa taratibu zote za uchunguzi ikiwamo mahojiano zimeshaanza kufanyika; “Tumeshamuhoji na tunaendelea kumchunguza, hilo linaeleweka.”
MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete ametangaza Aprili 30 kuwa ni siku ya kupiga Kura ya Maoni, lakini Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kinataka kuitumia kwa malengo tofauti; imepanga kuanza mgomo nchi nzima wa kudai stahiki zao.
Chama hicho, ambacho kinaongoza walimu shule za msingiu na sekondari wapatao 206,000 kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2010, kimeeleza kuwa iwapo Serikali itakuwa haijatekeleza maazimio yao matano ifikapo tarehe hiyo, walimu watachukua uamuzi mgumu kama ule wa mwaka 2012.
Uamuzi huo uliofikiwa kwenye mkutano wa Baraza la CWT uliomalizika Morogoro wiki mbili zilizopita, umekuja katika kipindi ambacho wadau wengi wana shaka na utayari wa Serikali kufanikisha mchakato wa Kura ya Maoni kutokana na viashiria vingi vya vikwazo, hasa muda wa kutosha kutekeleza masuala yote yanayohitajika kama Sheria ya Kura ya Maoni inavyotaka.
Rais wa CWT, Gratian Mukoba alitaja maazimio hayo kuwa ni kuitaka Serikali kulipa Sh 16 bilioni ambazo ni madeni ya walimu, kupandisha walimu wanaostahili, kulipwa mishahara waliokuwa wanadai tangu mwaka 2012, mwalimu kuwa na mwajiri mmoja kati ya Wizara ya Elimu na Tamisemi na kubadilishwa kwa kanuni za viinua mgongo kwa wastaafu.
“Yote haya yanatakiwa kutekelezwa ifikapo Aprili 30 mwaka huu la sivyo Baraza litawataka walimu kuchukua uamuzi mgumu. Fedha za kumlipa mwalimu zipo, lakini wanaozifaidi ni wachache,” alisema Mukoba, ambaye pia ni rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta).
NIPASHE
Siku moja baada ya Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma kusema imewaita watuhumiwa tisa wa sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow, mbunge wa Bariadi Mashariki (CCM), Andrew Chenge, amekiri kupokea barua ya wito wa kuhojiwa.
Chenge ambaye hadi anakumbwa na kashfa hiyo alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, alipoulizwa jana kama amepokea barua ya wito huo, alijibu kwa kifupi na bila kufafanua: “Nimepokea barua yangu tu.”
Katika kashfa hiyo, Chenge alipata mgawo wa Sh. bilioni 1.6.
Kwa upande wake, mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja, alipoulizwa swali hilo alisema: “Sina la kusema kwa hilo.”
Ngeleja aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, alipata mgawo wa Sh. milioni 40.4.
Naye, aliyekuwa Waziri wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, alisema hajapokea barua ya wito huo.
Profesa Tibaijuka ambaye ni Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM), alisema hajapata wito wowote na kwamba hata bungeni hayupo.
“Mimi nimekuambia kwamba sijapata wito wowote, kwanza mimi naumwa na hata bungeni sipo, kama wameniita waulize wenyewe waliokuambia:-Prof. Tibaijuka.
NIPASHE
Rais Jakaya Kikwete amewakingia kifua polisi waliotembeza kichapo kwa wafuasi wa Chama Cha Wananchi (CUF), na kudai kuwa maandamano na mikutano yote ni lazima iwe na kibali cha polisi.
Rais Kikwete aliyasema hayo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, baada ya kuwaeleza waandishi wa habari walichozungumza faragha na mgeni wake, Rais wa Ujerumani, Joachim Gauck, na baadaye kuja mbele ya waandishi wa habari na kujibu maswali mbalimbali.
Akijibu swali la waandishi wa habari wa Ujerumani, aliyetaka kujua hali ya usalama na haki za binadamu nchini ikoje hasa ikizingatiwa Januari 27, mwaka huu, kulikuwa purukushani kati ya polisi na wafuasi wa Cuf, na kutumia nguvu kubwa katika kuwadhibiti.
Akijibu swali hilo, Rais Kikwete alisema zipo sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza watu wanapotaka kuandamana au kufanya mikutano ya hadhara na kwamba ni lazima zifuatwe kwa kupata kibali cha Polisi.
“Huwezi kuamka asubuhi na kuanza kuandamana au kufanya mkutano wa hadhara ni lazima sheria na taratibu zilizopo zifuatwe…vyama vya upinzani vimekuwa vikifanya mikutano na maandamano bila kubugudhiwa iwapo wamefuata sheria zilizopo:Kikwete
MTANZANIA
Watanzania wametakiwa kujenga utamaduni wa kula vyakula vya asili katika kujikinga na ugonjwa wa saratani, ambao hivi sasa umekuwa tishio duniani.
Mbali na hilo, pia wametakiwa kuepuka uvutaji wa sigara, ulevi wa kupindukia na kubadili aina ya maisha kama njia ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk. Harrison Chuwa, alisema katika kipindi cha mwaka mmoja hali ya ugonjwa huo imezidi kuwa mbaya.
“Katika kuadhimisha Siku ya Saratani Duniani leo, hali imekuwa ikibadilika na katika kipindi cha miaka mitatu, taasisi hiyo imekuwa ikipokea wagonjwa wa saratani 1,500 hadi 4,000 kwa mwaka,” alisema.
Alisema kati ya wagonjwa hao, wengi wao ni wale ambao ugonjwa huwa umefikia hatua za juu kiasi cha kusababisha matibabu yao kuwa ya gharama kubwa.
“Kwa kweli hata hali yetu ya maisha imekuwa ikichangia kwa kiwango kikubwa kuongezeka kwa ugonjwa huu hapa nchini. Kuacha kula vyakula vya asili na mboga za majani ni tatizo… badala yake vyakula vya kemikali nyingi vimechukua nafasi jambo ambalo si zuri kwa afya za Watanzania:- Dk. Chuwa.
HABARILEO
Kituo cha Afya cha Msanda Muungano kilichopo wilayani Sumbawanga Mkoa wa Rukwa, kinalazimika kutumia chumba kidogo, mwanga wa kibatari na mshumaa nyakati za usiku kwa ajili ya wajawazito kujifungua.
Kutokana na hali hiyo, Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Charles Apolinary ameishauri Serikali kukishusha hadhi kwa kutokidhi mahitaji.
Dk Apolinary alisema hayo juzi alipozungumza na viongozi wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Tanzania CCM (UWT) Wilaya ya Sumbawanga waliotembelea kituoni hapo katika kusherehekea miaka 38 ya chama hicho.
Alisema kituo hicho kina ukosefu wa nishati ya umeme hali inayoleta usumbufu wakati wa kutoa huduma za afya.
“Ni aibu kituo hakina hata dawa za kutuliza maumivu na bado unaita ni kituo cha afya? Kwa nini wasikishushe hadhi kiwe zahanati, kwa kuwa kuna zahanati nyingine dawa zipo:-Apolinary.
HABARILEO
Mahakama ya Tanzania inatarajia kujenga Mahakama za Rufani katika mikoa yote nchini ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za utendaji wa haki kwa wananchi.
Jaji Mkuu Mohamed Chande Othman alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akifunga Maonesho ya Wiki ya Sheria, yalikuwa yakifanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja kuanzia Januari 30 hadi jana.
Alisema lengo la kujenga mahakama hizo ni kuhakikisha kesi zote, zinazofunguliwa na kukatiwa rufaa zinasikilizwa na kuishia mkoani, pia wananchi wapate huduma kwa urahisi, haraka na kwa unafuu.
“Tunataka kila mkoa uwe na Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu, kwa sasa mikoa 10 haina Mahakama Kuu lakini tutahakikisha tunazijenga, pia tutaongeza idadi ya majaji ili kurahisisha utendaji wa kazi:-Othman.
Alisema kwa sasa Mahakama ya Rufani ina majaji 16, Mahakama Kuu majaji 80 lakini lengo lao ni kuwa na majaji 120.
Pia, alisema wana upungufu wa watendaji wengine wa mahakama wakiwemo makarani, jambo linalosababisha ucheleweshwaji wa nakala za hukumu.
Akizungumzia maonesho hayo, Jaji Othman alisema lengo ni kuelimisha wananchi kuhusu masuala ya kisheria na taratibu za kimahakama na ameshuhudia wananchi wakijitokeza na kuuliza maswali mbalimbali.