Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe amesema Watanzania wamepoteza imani na Jeshi la Polisi na ameliagiza kujitathmini na kutoa majibu kuhusu kukamatwa kwa vijana 1,200 wa kikundi cha uhalifu maarufu Panya Road.
Waziri Chikawe aliyekuwa akifungua mkutano mkuu wa mwaka kwa maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi nchini, amelitaka jeshi hilo kujiuliza na kutoa majibu kutokana na madai kwamba baadhi ya vijana hao wamekamatwa kwa matakwa tu ya polisi.
Alisema kuwa anazo taarifa kuwa polisi wamejikita zaidi katika makusanyo, badala ya kuangalia usalama wa watu na ndiyo maana wamekuwa si watu wa kuzuia tena uhalifu kama inavyotakiwa lakini wanasubiri matukio yafanyike.
Alitaka polisi pia watoe sababu za kwa nini wananchi wanasema kuwa kumeibuka kitengo cha dhuluma, ambacho wamekibatiza kuwa ‘kuingia bure na kutoka kwa hela’, jambo linalotia doa chombo hicho.
Hivi karibuni, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alitangaza kuwakamata zaidi ya vijana 1,500 kuwa madai ni Panya Road.
MWANANCHI
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kesho itawasha moto upya bungeni wakati itakaposoma ripoti maalumu ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ikitarajiwa kuibua kashfa tatu nzito ikiwamo ya misamaha ya kodi.
Kashfa nyingine zinazotarajiwa kuibuliwa kesho ni, ufisadi katika gharama za ujenzi wa jengo la watu mashuhuri (VIP) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na uuzaji wa nyumba ya Bodi ya Korosho.
Habari zilizothibitishwa na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe zilisema kuwa, tayari kamati hiyo imepokea ripoti ya ukaguzi huo ambayo inaonyesha ufisadi wa kutisha katika maeneo hayo matatu na mengineyo.
Masuala hayo matatu pia yaliibuka wakati wa vikao vya kamati za Bunge vilivyomalizika Dar es Salaam wiki iliyopita, huku bodi ya korosho ikibanwa kuhusu nyumba yake aliyouziwa Mbunge wa Kibaha Mjini (CCM), Silvestry Koka.
MWANANCHI
Mwenyekiti mmoja wa CCM wilayani Uyui, (jina linahifadhiwa) anatuhumiwa kumlawiti kijana mmoja nyumbani kwake maeneo ya Bachu baada ya kumlewesha pombe.
Kijana huyo anayefanya biashara ya kuuza chipsi eneo la Bachu, Manispaa ya Tabora anadaiwa kulawitiwa na mwenyekiti huyo wiki iliyopita kisha kuingiziwa vitu kwenye makalio yake.
Mmoja wa ndugu za kijana huyo, alikiri kwa ndugu yake kufanyiwa vitendo visivyofaa baada ya kuleweshwa pombe.
Kutokana na tukio hilo, ndugu huyo alimpigia simu mwenyekiti huyo kumuulizia kuhusu tukio hilo lakini alikana na waliamua kutoa taarifa polisi.
Alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo, mtuhumiwa alikanusha kuhusika na kitendo hicho na kwamba ni mahasimu wake wa kisiasa ndiyo wametengeneza tukio hilo kwa lengo la kumchafua kisiasa.
MWANANCHI
Mtoto mchanga mwenye umri wa mwezi mmoja, Yadiko Chigoda amelazwa katika hospitali ya Wilaya ya Benjamini Mkoani Dodoma baada ya kupigwa na mchi kichwani na baba yake mzazi na kumsababishia maumivu makali.
Mama mzazi wa mtoto huyo, Carolina Mnyawami alisema alisema tukio hilo limetokea jana saa 4 asubuhi wakati mume wake Fabian Chigoda alipokua akigombana na kaka yake kwa kuchapana fimbo huku yeye akiwaamulia.
“Nilipowanyang’anya fimbo ili wasiendelee kupigana mume wangu aliokota mchi na kunirushia kichwani… niliukwepa ili usinipige ndipo ulipompiga kichwani mwanangu niliyekua nimembeba mgongoni:-Mama.
Mganga mkuu wa Hospitali ya Mpwapwa amethibitisha kumpokea mtoto huyo na kusema kwa sasa wanaendelea na uchunguzi zaidi wa afya yake kwani fuvu linaonekana kama vile limepasuka.
MTANZANIA
JESHI la Polisi linawashikilia watu wawili wakazi wa Manispaa ya Tabora kwa tuhuma za kuwanyonga watoto wawili hadi kufa, kisha kuwafukia ndani ya nyumba waliyokuwa wanaishi.
Tukio hilo la kusikitisha linadaiwa kufanyika juzi saa moja jioni katika eneo la Chechem Manispaa ya Tabora walikokuwa wakiishi watuhumiwa wa mauaji hayo.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Juma Bwire, amethibitisha jana kutokea kwa mauaji hayo ya kikatili na kuwataja watuhumiwa kuwa ni mama mzazi wa watoto hao, Zuhura Masoud (25) na baba yake Shaban Ramadhan (75) wakazi wa Kata ya Chemchem mjini Tabora.
“Baada ya mama huyo kutekeleza unyama huo, aliwafunga kwa kuwavingirisha mifuko ya sandarusi kisha kuwafukia chini, mmoja sebuleni na mwingine chumbani kwake:-Bwire.
“Tunazo taarifa kwamba hawa watu walikuwa wakigombea nyumba kati yao, na inawezekana ugomvi huo labda ndiyo chanzo halisi cha mama huyo kuamua kuchukua uamuzi mgumu kama huo wa mauaji ya kinyama kwa wanawe wawili:-Bwire.
MTANZANIA
Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, wamekacha makabidhiano ya ofisi hatua iliyofanya mawaziri wapya kukabidhiwa ofisi na watendaji.
Mialiko iliyokuwa imetolewa, ilisema mawaziri hao wangekabidhi ofisi kwa wateule wapya, William Lukuvi, aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na George Simbachawene wa Nishati na Madini.
Kutokana na kutotokea kwa Profesa Muhongo, ilimlazimu Simbachawene akabidhiwe ofisi na wakabidhiwe ofisi na watendaji wa wizara husika.
Baada ya Lukuvi kukabidhiwa ofisi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Alphayo Kidata, alieleleza mikakati yake huku akisema namna wizara hiyo ilivyokuwa ya moto.
Alisema anaifahamu vizuri wizara hiyo kutokana na kuwapo kwa mtandao wa watendaji wanaoshirikiana na matajiri kutapeli wananchi.
MTANZANIA
JUKWAA la Wakristo Tanzania (TCF) limepinga muswada unaopendekeza kuanzishwa Mahakama ya Kadhi, likiitaka Serikali iuondoe bungeni kwa madai kuwa ni wa kibaguzi na upo kinyume na matakwa ya Katiba.
Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ya 2014, unapendekeza pamoja na mambo mengine, marekebisho ya Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu ya mwaka 1964.
Maaskofu na wajumbe wa jukwaa hilo walikutana Januari 20, mwaka huu jijini Dar es Salaam na kushauri Serikali iondoe muswada huo bungeni ili kuepusha kuvunja misingi ya taifa ambayo kwa sasa Tanzania inatambulika kama taifa lisilo la kibaguzi na lisilofungamana na dini.
Taarifa ya jukwaa hilo kwa vyombo vya habari ilitolewa jana na kusainiwa na wenyeviti wake, Askofu Dk. Alex Malasusa, Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Pentekoste Tanzania (CPCT), Daniel Awet.
‘‘Tunatambua kwamba suala la Mahakama ya Kadhi lilikataliwa na Bunge Maalumu wakati wa kupitishwa kwa Katiba inayopendekezwa. Tunaelewa kwamba Katiba inayopendekezwa imetamka wazi kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi isiyofungamana na dini yoyote”:-Taarifa.
‘‘ Katiba hiyo imetamka wazi kuwa shughuli ya uendeshaji wa jumuiya za dini itakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya Serikali.
NIPASHE
Serikali imewaagiza wakandarasi kukamilisha ujenzi wa barabara ndogo zote za jijini Dar es Salaam kwa kiwango cha lami kabla ya Aprili mwaka huu katika harakati zake ya kupunguza msongamano wa magari.
Waziri wa Ujenzi, Dk.John Magufuli, alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kuweka jiwe la msingi katika shule sita za msingi zilizopo jijini na kusema kazi hiyo imetengewa bajeti ya Sh. bilioni 56.323 katika bajeti ya mwaka 2015.
Akiweka jiwe la msingi katika barabara katika Shule ya Msingi Ubungo Msewe, Makuburi na eneo la Kigogo Polisi, Kinyerezi na Goba Tangibovu jana, Waziri alisema barabara hizo zimekamilika kwa asilimia 12 katika hatua za awali.
“Barabara hizo ni zile ambazo ziko chini ya Wakala wa Barabara (Tanroads) na katika bajeti ya 2015, serikali imetenga Sh. bilioni 16 kwa ajili ya barabara ndogo zilizopo katika manispaa zake zote, Kinondoni milioni 10.4 Temeke bilioni 1.8 na Ilala bilioni 4.4:-Dk. Magufuli.