Waziri wa Kilimo,chakula na Ushirika Steven Wassira amesema kosa alilolifanya la kufunga vifungashio vya koti limempa umaarufu mkubwa kiasi cha kumpa Urais.
Waziri huyo amesema amefurahishwa na kosa hilo kwani sasa imekuwa staili mpya ya uvaaji wa makoti kwa vijana wa ndani na nje ya nchi.
Wasira alikiri kwamba siku hiyo alikosea kuvaa koti kiasi kwamba vishinikizo vyake kupishana lakini hajutii kosa hata kidogo kwani limempa umaarufu.
“Ile picha niliyopigwa kwenye mitandao ya kijamii ikinionyesha nimekosea kuvaa koti ni ya kweli wala si ya kutengeneza kwa ajili ya kunichafua,baada ya muda nikaona vijana nao wanavaa kwa staili ile na kujita Wassira Staili..imenipa umaarufu mkubwa sana” Wassira.
Alisema hata watu ambao walikuwa hawamjui sasa wanamjua kupitia kosa hilo na kosa kama hilo pia lilishawahi kufanywa na Rais wa Rwanda Paul Kagame hivyo si jambo la ajabu.
Aliongeza kuwa kosa lile lilitokana na haraka aliyokuwa nayo kuwahi kwenye kazi za uwaziri hata mkewe hakuwepo kuhakiki kama ametoka vizuri.
MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete amesema baadhi ya wakuu wa wilaya walitemwa kutokana na upungufu, ikiwa ni pamoja na madeni mitaani.
Rais alisema baadhi yao walikuwa wakienda baa wanalewa na ili kuwaondoa ilibidi wake zao waitwe kuwachukua.
Rais Kikwete alisema hayo jana mjini Dodoma alipokuwa akifungua semina elekezi kwa wakuu wa wilaya 27 wapya walioteuliwa hivi karibuni.
Februari 18 mwaka huu, Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya wakuu wa wilaya na kutengua uteuzi wa wakuu wa wilaya 12.
Rais Kikwete alisema waliotemwa walikuwapo wenye upungufu mbalimbali na wengine walikuwa na madeni mitaani huku baadhi yao wakiwa na tatizo la ulevi kiasi kwamba wakienda baa hulewa kupita kiasi.
Aliwaasa wakuu wa wilaya wapya kuwa wengine ni wadogo kiumri lazima wafanane na madaraka waliyopewa.
“Pale ulipo ni role model (mfano wa kuigwa), lazima uwe na tabia njema kwa kauli, matendo, nidhamu na uadilifu usiotiliwa shaka,” Kikwete.
MWANANCHI
Wakati Taifa likijiandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, yamebainika mambo matatu mazito ambayo yanaliweka njiapanda , hali inayosababisha viongozi na hata wananchi kubaki na maswali lukuki wakihoji hatma ya nchi yao.
Mambo hayo ambayo hadi sasa hayajulikani hatma yake ni Katiba Inayopendekezwa, Mahakama ya Kadhi na uboreshaji wa Daftari la Wapigakura kwa vifaa vya kielektroniki vya Biometric Voter Registration (BVR).
Mambo hayo yamekuwa mjadala wa kitaifa kwa muda sasa, hoja kubwa ikiwa ni endapo matukio makubwa ya kitaifa – upigaji wa kura ya maoni kupitisha Katiba Mpya na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba yatafanyika kwa mafanikio au yanaweza kukwama na kusababisha sintofahamu.
Hoja kubwa katika eneo hili imekuwa ni iwapo kura ya maoni ya kupitisha Katiba itafanyika Aprili 30, mwaka huu kama ilivyopangwa, lakini Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva mara kadhaa amesimamia msimamo wa Serikali kuwa uandikishaji unaendelea bila matatizo katika Mkoa wa Njombe kama ilivyopangwa.
Ukiacha upungufu unaosababisha shughuli hiyo kuchukua muda mrefu, Jaji Lubuva amekuwa akikwepa kuzungumzia madai kuwa Serikali haikutoa fedha za kutosha kufanikisha shughuli hiyo, lakini juzi alikiri kuwa Tume yake ilijaribu hata kuazima vifaa hivyo Kenya na Nigeria bila mafanikio.
Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba amekaririwa na gazeti hili jana akisema hata bajeti ya mchakato huo ya Sh297 bilioni iliyopangwa haipo kwa kuwa katika kasma ya tume zilikutwa Sh7.01 bilioni na fedha za maendeleo na fedha za tume hazikuonekana.
Profesa Lipumba alisema pia hata Sh144 bilioni za kura ya maoni zilizoelezwa na Tume hazikuonekana kwenye vitabu vya bajeti na kuwa BVR 250 zilizopo badala ya 8,000 zilizokusudiwa haziwezi kufua dafu.
Kuhusu muda uliosalia wa siku 42 kabla ya kura ya maoni, umeelezwa na wachambuzi kuwa hautoishi, ukilinganishwa na Kenya iliyokuwa na BVR 15,000 na ikaandikisha wapiga kura milioni 14 kwa siku kati ya 45 hadi 60.
Kutokana na hali hiyo, kinachosubiriwa na wananchi ni ama kuelezwa ni muujiza gani utafanyika hadi shughuli hiyo kukamilika na kura ya maoni kupigwa bila matatizo au kuahirisha kura hiyo hadi wakati au baada ya uchaguzi mkuu.
Saula jipya kabisa katika mjadala wa uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi inayotambuliwa na Serikali ni kesi iliyofunguliwa Mahakama Kuu na Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila akitaka mahakama itamke kuwa Mahakama ya Kadhi na masuala ya Jumuiya ya Kiislamu (OIC) ni haramu na itamke kuwa ulinzi na uhai na utu wa binadamu nchini hauwezi kubaguliwa na Uislamu.
MTANZANIA
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ameibua ufujaji wa mabilioni ya fedha kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Katika ripoti ya ukaguzi wa CAG kwa vyama hivyo aliyoikamilisha Septemba mwaka jana kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa namba tano ya mwaka 1992, sehemu ya 14 (1)(b) imeibua madudu hayo.
Taarifa hiyo ya CAG imechambua hesabu za Chadema na CCM na kusema wakati wa ukaguzi walibaini masuala mengi ikiwamo kutotolewa taarifa sahihi za matumizi.
Kutokana na hali hiyo, CAG alilazimika kutoa hati yenye shaka kwa chama tawala – CCM ambacho kilionyesha kumiliki mali za kiasi cha Sh bilioni 19.5.
Hata hivyo, imebainika kuwa CCM haina daftari la mali za kudumu, ambalo lingeweza kubainisha ukamilifu wa taarifa kuhusu umiliki huo wa fedha za chama hicho.
CAG alisema chama hicho hakikufanya tathmini ya mali zake kwa kipindi kirefu, hivyo, fedha hizo haziwakilishi thamani halisi.
Alisema chama hakikutenganisha thamani ya ardhi na majengo badala yake kikieleza kuwa na thamani ya Sh bilioni 11.4 ambapo alishindwa kubainisha kwa kutenganisha thamani za ardhi na zile za majengo kama kinavyoagiza kifungu cha 58 cha viwango vya uhasibu vya kimataifa (IAS) 16.
“Hatukuweza kupata taarifa za ukaguzi zinazounga mkono uwekezaji wa CCM ulioelezwa kuwa na thamani ya Sh bilioni 9.6 ambao umejumuishwa katika hali ya taarifa ya kifedha iliyoishia Juni 30, 2013 zilizoelezwa katika vipengele 6 na 7 vya taarifa za fedha.
MTANZANIA
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu jana alionekana kumpiga kijembe Katibu MKuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana aliposema kuwa sasa atakuwa anazurura angani.
Nyalandu alitoa kauli hiyo Dar es Salaam alipozindua ndege nyepesi (Micro-Light, 5H – Hel), ambayo itatumika kupambana na ujangili katika Hifadhi ya Taifa ya Selous.
“Karibuni wote, leo tunazururia hapa uwanja wa ndege na ninazindua ndege hii nyepesi ambayo imetengenezwa Ufaransa, itatumika kupambana na majangili katika Mbuga ya Selous.
“Kwa maana hiyo sasa tunaanza kuzururia angani kupambana na majangili na nasisitiza kwamba ndege hii ni mpya kabisa na gharama za uendeshaji wake ni ndogo kwa vile inatumia petroli,” alisema.
Hivi karibuni Kinana akiwa ziarani mkoani Arusha alimsifia Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM) kuwa ni mchapakazi lakini Waziri Nyalandu ni mzururaji.
Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa ndege hiyo ya kupambana na ujangili, Nyalandu alisema imetengenezwa kwa gharama ya Dola za Marekani 2,040,000 na ina uwezo wa kubeba askari mmoja na rubani.
Waziri Nyalandu alisema ndege hiyo imeundwa kwa usalama wa hali ya juu kwa kuwekewa puto (parachute) ambalo litatumika kushuka chini iwapo ndege itaishiwa mafuta angani.
“Itakapoanza kutumika itasaidia kuwabaini majangili, inakwenda kwa mwendo mdogo iwapo angani hali ambayo inawezesha kuwaona majangili na kila kinachoendelea ardhini kwa wepesi,” Nyalandu.
MTANZANIA
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Cecilia Mosha aliyejirusha kutoka ghorofa ya tatu hadi chini kutokana na hofu ya moto uliotokea katika Hosteli ya Mabibo, amevunjika mfupa wa bega.
Mwanafunzi huyo alijirusha kupitia dirishani juzi katika harakati za kujiokoa na moto baada ya jengo la wasichana, Block A kushika moto huku wanafunzi wakiwa vyumbani wakiendelea na shughuli zao.
Cecilia ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Shahada ya Uhandisi wa Uchimbaji Madini, alisema alisikia kelele akiwa chumbani na alipotoka nje akakuta moshi umetanda kila kona.
“Baada ya kuona hivyo niliona ni vema nijiokoe kwa kujirusha kutoka ghorofa ya tatu ya bweni hilo hadi chini kupitia dirishani,”Mosha.
Alisema baada ya kuruka hadi chini alikimbizwa katika kituo kidogo cha afya karibu na hosteli hiyo ambako alipoteza fahamu na kushtukia yupo katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI).
Naye Meneja Ustawi na Uhusiano wa Taasisi ya MOI, Almasi Jumaa alisema hali ya Cecilia si mbaya na anaendelea na matibabu.
“Tumempokea huyo mgonjwa jana na baada ya timu ya madaktari kumfanyia vipimo vya kutosha wamebaini amevunjika mfupa wa bega la kulia na kupata mshtuko wa mwili … alipata maumivu ya kiuno na mwili kwa ujumla,” alisema Jumaa.
Ajali hiyo ya moto ilitokea juzi katika Hosteli ya Mabibo iliyopo Mtaa wa Ubungo Kibangu, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala moto huo uliteketeza ghorofa ya tatu ya jengo A linalotumiwa na wanafunzi wa kike.
HABARILEO
KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa(UN), Ban Kimoon amemteua Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman kuongoza Timu Huru ya Wataalamu kuchunguza kifo kilichotokana na ajali ya ndege cha aliyekuwa Katibu Mkuu wa UN, Dag Hammarskjöld na ujumbe wake Septemba 18, 1961 katika Jamhuri ya Kongo.
Taarifa iliyotolewa na UN jijini Dar es Salaam juzi imewataja wajumbe wengine wa timu hiyo kuwa ni pamoja na Kerryn Macaulay, raia wa Australia na Henrik Larsen wa Denmark.
Kuundwa kwa timu hiyo kwa mujibu wa taarifa hiyo kunatokana na azimio namba 69/246 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitolewa Desemba 29, mwaka jana lililomwomba Katibu Mkuu, kuunda timu huru ya kuchunguza na kutathmini kifo cha Hammarskjöld na ujumbe wake walipokuwa katika harakati za kuleta amani nchini Congo.
Baraza hilo kwa mujibu wa taarifa hiyo pia lilizitaka nchi wanachama wa UN kutoa kumbukumbu zozote muhimu walizonazo kuhusu na kifo hicho cha Hammarskjöld.
Taarifa imefafanua kwamba timu hiyo ya wataalamu itaanza kazi yake rasmi Machi 30, mwaka huu na kukabidhi ripoti yake kwa Katibu Mkuu wa UN si zaidi ya Juni 30, mwaka huu.
Dag Hammarskjöld, raia wa Sweden alikuwa Katibu Mkuu wa pili wa UN kati ya Aprili 10, 1953 na Septemba 18, 1961 alipokufa katika ajali ya ndege nchini Congo pamoj
HABARILEO
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekamata bidhaa za magendo zenye thamani ya Sh milioni 228.4, ikiwa ni katika jitihada za kudhibiti uingizaji wa bidhaa kwa njia ya magendo na biashara ya magendo nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, bidhaa hizo zimekamatwa ndani ya miezi mitatu tangu Januari hadi Machi katika mikoa minne pekee.
Bidhaa hizo zimekamatwa katika mikoa ya Arusha, Kagera, Morogoro na Tanga katika operesheni inayoendeshwa kwa ushirikiano kati ya TRA na Jeshi la Polisi nchini.
Taarifa hiyo imefafanua zaidi kuwa, kwa upande wa Mkoa wa Kagera, viroba 675 vilivyosheheni katoni 2,043 za pombe aina ya Signature Vodka kutoka Uganda ambazo ni sawa na lita 24,516 yenye thamani ya zaidi ya sh milioni 61.3 zilikamatwa kwenye jahazi.
Kwa upande wa Mkoa wa Morogoro, taarifa hiyo inabainisha kuwa madumu 1599 ya lita 20 za mafuta ya kupikia yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 65.9 yalikamatwa eneo la Bwawani yakiwa katika malori mawili yaliyokuwa yakitokea Bagamoyo kwenda Morogoro.
Taarifa hiyo inasema pia TRA wamekamata madumu 888 ya lita 20 za mafuta ya kupikia yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 15.8 yalikamatwa eneo la Kwame katika bandari bubu wilayani Mkinga, mkoani Tanga.
Taarifa hiyo inabainisha kuwa kwa kutumia taarifa kutoka kwa wasamaria wema, TRA imekamata jumla ya madumu 75 ya mafuta ya taa yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 2.9 mkoani Arusha yakiwa yamepakiwa katika gari aina ya Toyota hiace yakisafirishwa kutoka Holili kwenda Moshi kwa magendo.
NIPASHE
Wakati Tanzania ikitajwa kuwa kichochoro cha kupitishia dawa za kulevya, wabunge wamehoji dawa hizo zinazokamatwa kama ushahidi zimekuwa zikipelekwa wapi kwa kuwa haionyeshi kama zimekuwa zikichomwa moto au la hali inayotia shaka udhibiti wa biashara hiyo.
Mbunge wa Viti Maalum, Rukia Ahmed, akiuliza swali la nyongeza jana bungeni, alisema kumekuwa na ucheleweshaji wa kesi za dawa za kulevya licha ya mtuhumiwa kukutwa na dawa hizo tumboni na pia zilizokamatwa haionyeshi zinapelekwa wapi.
Alisema kesi nyingi za mauaji na dawa za kulevya zinachukua muda mrefu kumalizika mahakamani na kusababisha watuhumiwa kukaa zaidi ya miaka saba rumande na kuhoji kwa nini muda wanaokaa rumande usijumuishwe kama sehemu ya hukumu wanapotiwa hatiani.
Mbunge wa Karagwe (CCM), Gosbert Blandess, alihoji lini serikali itaanzisha mahakama maalum kwa ajili ya kushughulikia kesi za dawa za kulevya na rushwa kama njia ya kudhibiti tatizo hilo.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Ummy Mwalimu, alisema mahakama inaendeshwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi, hivyo suala la hukumu pamoja na kipindi cha mshtakiwa kutumikia kifungo chake hufanyika kulingana na sheria inavyotamka kuhusu adhabu ya kosa husika.
Kuhusu zinapopelekwa dawa za kulevya zinazokamatwa, alisema kiutaratibu vidhibiti havirudishwi na hukumu ikishatolewa vinateketezwa.
NIPASHE
Wakati Spika wa Bunge, Anne Makinda, akisema hawezi kumtangaza Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kuwa siyo mbunge hadi atakapopata barua ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amesema bado hawajaandika barua kuiarifu Nec, kwa kuwa hilo siyo jambo kubwa ambalo chama kinapaswa kuhangaika nalo kwa sasa.
Spika Makinda aliwaambia waandishi wa habari nje ya viwanja vya Bunge mjini Dodoma jana kuwa ofisi yake haiwezi kufanyia kazi taarifa za kwenye vyombo vya habari, badala yake inasubiri taarifa za kiofisi kutoka Nec.
“Hatuwezi kutangaza sasa kwa sababu hatujapata barua. Tumesikia kwenye vyombo vya habari tu. Kwa hiyo hadi hapo tutakapopata barua ya Nec ndipo tutakapotangaza,” Spika Makinda.
Hata hivyo, alisema kwa mujibu wa sheria, chama kikimvua mbunge uanachama anapoteza ubunge wake.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alisema hana taarifa kama barua ya taarifa ya kumvua Zitto uanachama imekwishaandikwa kwa Nec au la kwa kuwa Ofisi ya Katibu Mkuu wa chama hicho ndiyo inahusika kuiandika.
Dk. Slaa alisema hatua ya kuandika barua hiyo itafuatia baada ya kikao cha Kamati Kuu ya Chama kuitishwa na kufanyika. Hata hivyo, alisema suala la kuitisha kikao hicho linahitaji mchakato na kwamba hivi sasa kuna vitu vikubwa na vyenye athari kubwa kwa umma na siyo suala la uanachama wa Zitto ndani ya Chadema.
Alitaja vitu ambavyo Chama kinahangaika navyo kwa sasa kuwa ni pamoja na Daftari la Kudumu la Wapigakura.
“Sidhani kama waandishi wa habari mnahangaika nalo hilo, kama mnavyohangaika na suala hilo la uanachama wa Zitto,” Dk. Slaa.
Kitu kingine ambacho alikitaja kuwa ni katika vitu wanavyohangaika navyo kwa sasa kuwa ni mamilioni ya shilingi ‘yanayoteketea’ kwa ajili ya kuandaa sherehe za ‘Wiki ya Maji.’
“Hatujaandika hiyo barua, tutaandika ratiba yetu ikituruhusu,” Dk. Slaa.
Zitto alitangazwa kupoteza uanachama katika chama hicho wiki iliyopita baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam kutupilia mbali kesi yake dhidi ya Chadema iliyokuwa ikihoji uhalali wa uanachama wake ndani ya chama hicho.
Hautopitwa na stori yoyote inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook