NIPASHE
Watu wanne waliohukumiwa jana na Mahakama Kuu kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kuua albino, wameongeza idadi ya waliokwisha kutiwa hatiani ili wanyongwe kwa kosa hilo kufikia 17 nchini.
Idadi hiyo imeongezeka baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza kuwatia hatiani watu wanne jana kwa mauaji ya mwanamke mwenye ulemavu wa ngozi yaliyofanyika mwaka 2008.
Kabla ya jana, watu 13 walihukumiwa kunyongwa hadi kufa kutokana na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi katika maeneo kadhaa ya Tanzania hususan mikoa ya Kanda ya Ziwa kutokana na imani za kishirikina.
Watu wanne jana akiwamo mume wa marehemu, walihukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mlemavu wa ngozi, Zawadi Mangidu (22), mkazi wa Nyamalulu, Kata ya Kaseme, wilayani Geita.
Hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza, huku ndugu wa waliohukumiwa adhabu hiyo ya kunyongwa hadi kufa ambao walikuwa miongoni mwa wakazi wengi wa mji huo waliofurika mahakamani hapo kushuhudia hukumu hiyo, wakiangua vilio.
Waliokumbwa na adhabu hiyo ni Masalu Kahindi (54), Ndahanya Lumola (42), Singu Nsiyantemi (49) na Nassor Said (47), mume wa marehemu Zawadi Mangindu.
Mahakama hiyo iliwahukumu watu hao ambao ni wakazi wa wilaya hiyo, baada ya kupatikana na hatia ya kula njama na kushiriki kumuua kwa kukusudia mlemavu huyo wa ngozi.
Akitoa hukumu hiyo, Jaji De-Mello, alisema amezingatia kwa makini na tahadhari kubwa katika kufikia uamzi huo baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na mashahidi 12 wa upande wa mashtaka na utetezi, kwamba washtakiwa walitenda kosa hilo bila kuwa na shaka yoyote.
Jaji De-Mello alisema katika hukumu zilizotangulia, pia zilibainisha kuwa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yamekuwa yakitekelezwa na mtandao mkubwa na siyo rahisi kuubaini kirahisi.
Awali, upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Hezron Mwasimba, akisaidiana na wakili Janeth Kisibo, ulidai kuwa washtakiwa kwa pamoja kwa makusudi walishirikiana kula njama na kutenda kosa la kumuua mlemavu huyo wa ngozi, saa moja usiku, Machi 11, mwaka 2008 katika kijiji cha Nyamalulu kata ya Kaseme wilayani Geita.
NIPASHE
Wakati idadi ya watu waliopoteza maisha katika maafa yaliyosababishwa na mvua iliyonyesha ikiambatana mawe, upepo mkali na kubomoa nyumba za wananchi Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, ikiongezeka kutoka 42 na kufikia 46, baadhi ya wananchi wa eneo hilo wamelihusisha janga hilo na ushirikina.
Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Mwakata wilayani Kahama, Salum Mohamed, alimweleza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuwa baadhi ya wananchi wamejenga dhana kuwa tukio hilo limetokana na ushirikina.
Hata hivyo, Pinda aliyewasili hapa jana, aliwataka wananchi hao kuachana na dhana hiyo potofu kuwa mvua zilizonyesha na kusababisha maafa hayo, zimetokana na ushirikina.
Mvua hiyo ilinyesha juzi usiku na kuleta maafa katika vijiji vya Mwakata, Nyumbi na Magung’hwa vilivyopo kata ya Isaka wilayani Kahama.
Idadi hiyo imeongezeka kufuatia majeruhi wanne waliokuwa wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama kufariki dunia usiku wa kuamkia jana kuongeza idadi ya waliokufa katika janga hilo kufikia 46.
Waziri Mkuu, alitembelea vijiji vilivyoathirika na kuwapa pole waathirika na kusema serikali itahakikisha waathirika wote wanapewa msaada unaotakiwa na kwamba tayari chakula kimeanza kugawiwa kwa wananchi na mahema ya kutosha yametolewa. Pinda aliagiza waatalam kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuweka kambi katika kijiji cha Mwakata kilichoathirika kwa ajili ya kufanya tathmini.
Waziri Mkuu alisema kutokana na janga hilo, kuna uwezekano wa kutokea magonjwa ya mlipuko.
Aidha, aliiagiza timu ndogo ya uratibu wa maafa iliyoundwa na Mkoa wa Shinyanga, isimamie vizuri misaada inayotolewa na wasamaria wema ili iwafikie waathirika wote.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, jana aliwasili Kahama na kutembelea vijiji vilivyoathirika na kuwapa pole waathirika na kuwataka wananchi waondokane na fikra potofu kuwa tukio limetokana na masuala ya kishirikina.
NIPASHE
Serikali imekiri kuwapo kwa uhaba wa tani 100,000 za sukari nchini ikieleza kuwa kiasi kilichopo sasa cha tani 67,000 kinatosheleza hadi mwisho wa mwezi huu pekee.
Kutokana na uhaba huo, serikali imezuia tani 11,059.75 za sukari iliyokuwa inasafirishwa kwenda nje ya nchi ili itumike nchini kuziba pengo hilo.
Hayo yalibainishwa na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, wakati akiwasilisha taarifa yake kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, kuhusu hali ya uzalishaji na usambazaji wa sukari nchini.
Alisema uhaba huo unatokana na uzalishaji wa sukari kutotosheleza mahitaji ya nchi, baadhi ya viwanda kutokuwa na akiba yoyote hadi sasa na vingine kufungwa kwa ajili ya kusubiri msimu mwingine wa uzalishaji.
Alisema kiasi halisi kinachotosheleza mahitaji ya nchi ni tani 420, 000 kwa mwaka, lakini kiasi kilichozalishwa kwa msimu wa 2013/2014 ni tani 300,000 pekee hivyo kuwa na upungufu wa tani 120, 000.
Kwa mujibu wa Wasira, hali hiyo inatokana na changamoto mbalimbali ikiwamo ya kuyumba kwa soko la sukari ambako kulisababishwa na uingizwaji wa bidhaa hiyo kwa njia za magendo.
Hata hivyo, alisema utaratibu wa kuagiza sukari kwa pamoja ni mpya na unaweza kuchukua muda mrefu hivyo, imeamuliwa kuwa sukari iliyohifadhiwa kwenye maghala kwa muda mrefu kiasi cha tani 11, 059.75 ifanyiwe tathmnini ya ushuru na Mamlaka ya Mapato (TRA) na iingizwe kwenye soko kuziba pengo.
MTANZANIA
Wakazi wa Kijiji cha Mwakata, Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga, jana walilazimika kufukua makaburi mawili walimokuwa wamezika watoto watano wa familia moja waliofariki dunia juzi baada ya mvua kubwa ya mawe kunyesha kijijini hapo.
Ufukuaji wa kaburi hilo ulifanyika mchana na kuitoa miili ya watoto hao, Luku Masemba (14), Paschal Masemba (11), Mulyante Masemba (9), Sesela Masemba (7) na Masele Masemba (5).
Taarifa zilizopatikana zinasema kuwa kaburi hilo lilifukuliwa baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, kuagiza lifukuliwe ili marehemu hao wazikwe kila mmoja katika kaburi lake.
Kabla ya agizo hilo lililotolewa na Mpesya mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ali Rufunga, miili ya watoto watatu wote wa kike ilikuwa imezikwa katika kaburi moja.
Wakati watoto hao wa kike walikuwa wamezikwa katika kaburi moja, maiti mbili za watoto wa kiume zilikuwa zimezikwa katika kaburi moja.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, maiti hizo zilikuwa zimefungwa kwenye mifuko ya sandarusi baada ya wananchi kukosa sanda kutokana na Serikali kuchelewa kutoa utaratibu wa namna ya kuzikwa miili hiyo.
“Nimeambiwa mmewazika hawa watoto watatu kaburi moja na wengine kaburi lao moja. Hapana, hapana, huu siyo utaratibu hata kidogo.nataka hawa marehemu wafukuliwe na kila mmoja azikwe kwenye kaburi lake siyo kama mlivyofanya ninyi.a watu kwa pamoja labda itokee hawatambuliki na ndugu zao hawajajitokeza.
“Hawa watoto ni wa familia moja na mnawafahamu kwa majina na umri wao, iweje muwazike kaburi moja watatu na jingine wawili?
“Naagiza wafukuliwe na wazikwe upya katika mazingira ya binadamu,”:- Mpesya.
MTANZANIA
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino), wamepigana ngumi na mateke wakigombea kuingia kumwona Rais Jakaya Kikwete, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo la aina yake lilitokea jana majira ya saa nne asubuhi ambapo lilianzia kwenye eneo la mapokezi Ikulu mara baada ya walemavu hao kukaguliwa na kuwekwa kwenye chumba maalumu cha kupumzikia wageni.
Baada ya muda, ofisa wa Ikulu alifika kwenye chumba walipokuwa walemavu hao akiwa na karatasi yenye orodha ya watu 15, ambao ndiyo waliopaswa kumwona Rais.
Baada ya ofisa huyo kuanza kusoma majina ya wahusika, albino wote waliokuwa kwenye chumba hicho walinyanyuka kutoka kwenye viti vyao na kusimama karibu na mlango, ambako alikuwa amesimama.
Kila ofisa huyo alipokuwa akisoma jina, mhusika alitoka nje ya chumba hicho tayari kwa kwenda kumwona Rais.
Baada ya ofisa huyo kumaliza kusoma majina hayo, alisema: “Hawa ndio wanaokwenda kuwawakilisha kwa sababu hamuwezi kuingia kundi lote hili.”
Baada ya majina hayo kutajwa, mmoja wa albino hao, Nuru Chagutu, ambaye hakutajwa, alisema hakubalini na kitendo cha viongozi pekee kumwona Rais ili hali wajumbe wengine ambao pia ni wahathirika wa mauaji ya albino wakibaki getini.
Alisema pia yeye na wanaharakati wenzake wa Chama cha Tunataka Haki ya Kuishi (THK), hawamtambui Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu wa Ngozi Tanzania (TAS), Ernest Kimaya, ambaye alikuwa kwenye orodha ya watu 15 waliopangwa kumwona rais.
Alihoji pia sababu za Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Walemavu Tanzania (Shivyawata), Amon Mpanju, ambaye si mlemavu wa ngozi, kuwamo kwenye orodha hiyo huku akiwa si mlemavu wa ngozi.
MWANANCHI
Wakati CCM ikielekea katika kipindi kigumu cha kuamua mgombea wake wa urais kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, Makongoro Nyerere, ambaye ni mtoto wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, amezungumzia taarifa zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii zikimtaja kuwa na mpango wa kuwania nafasi hiyo ya juu nchini.
CCM, ambayo imeshika nchi tangu kurejeshwa kwa siasa za vyama vingi, hujikuta katika wakati mgumu kila wakati inapotakiwa kutoa mgombea wa kurithi nafasi ya Rais aliye madarakani baada ya kuongoza vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja.
Tayari wanachama wanne wa chama hicho tawala wameshatangaza rasmi kuwania urais huku wengine sita wakifungiwa kwa makosa ya kudaiwa kuanza kampeni mapema, huku kukiwa na mlolongo wa watu wanaotajwa kuwa na mpango wa kujitokeza kuwania nafasi hiyo, akiwamo Makongoro, ambaye imeelezwa kuwa ameshauriwa kuchukua uamuzi huo kujaribu kukinusuru chama kutokana na makundi yanayoonekana kujitokeza katika mbio hizo.
“Mimi si mtabiri, siwezi kukwambia nitagombea au la, lakini uamuzi wangu utajulikana mara kipenga kitakapopulizwa na CCM,” alisema Makongoro ambaye ni ofisa wa zamani wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) na mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala).
Vyanzo hivyo vya habari vimeeleza kuwa mkakati wa kuhakikisha Makongoro anakuwa rais, unaratibiwa na baadhi ya makada waliowahi kufanya kazi na Mwalimu Nyerere.
Mkakati huo pia unatajwa kuwa ulianza pale alipochaguliwa kuwa mbunge wa Eala. Tayari Waziri Mkuu Mizengo Pinda, January Makamba, ambaye ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Lazaro Nyalandu ambaye ni Waziri wa Maliasili na Utalii na Hamisi Kigwangala wametangaza nia ya kuomba ridhaa ya CCM kuwapitisha kuwania urais.
Hata hivyo, upinzani mkubwa unaonekana kuwa kwa vigogo ambao hawajatangaza nia hiyo na ambao wanatumikia adhabu ya kufungiwa kwa zaidi ya miezi 12 kutokana na kikiuka taratibu za chama hicho.
Miongoni mwa ambao hawajajitokeza ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ambaye wafuasi wake wamekuwa wakijitokeza katika siku za karibuni kueleza wazi msimamo wao kuwa ndio chaguo sahihi, na Bernard Membe, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Pia yumo Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye, Spika wa zamani wa Bunge, Samuel Sitta, Waziri wa Kilimo na Chakula, Steven Wasira na Naibu Waziri wa Fedha-Sera, Mwigulu Nchemba, ambaye alionywa na chama hicho dhidi ya safari zake mikoani zilizodaiwa kuwa na dalili za kampeni.
Makongoro hakuonyesha kukataa wala kukubali kuhusu uamuzi wa kugombea nafasi hiyo iliyoshikwa na baba yake kwa takribani miaka 25.
“Ninachoweza kutabiri kwa sasa ni iwapo nina njaa basi lazima nitakula au simba akitokea lazima nikimbie. Kama nina usingizi na kuna kitanda karibu lazima nitalala lakini mambo mengine siwezi kuyasemea,” alisema Makongoro ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Arusha Mjini kwa tiketi ya chama cha NCCR-Mageuzi. Alisema anasubiri siku ambayo CCM itatangaza mchakato wa kuchukua fomu ndipo hatma yake itajulikana.
MWANANCHI
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli ameagiza kusimamishwa kazi aliyekuwa kigogo wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) ambaye hafanyi kazi tena kituoni hapo.
Agizo hilo alilitoa juzi, huku akitaka pia mkurugenzi wa zamani wa majengo na miradi wa AICC, Paul Ndossa ambaye awali akifanya kazi Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) akiwa mtaalamu na mshauri, asimamishwe.
Wakati Dk Magufuli akitoa agizo hilo, Ndossa alikuwa ameshaondoka AICC tangu Januari.
Agizo hilo lilitokana na Mtendaji Mkuu wa TBA, Elius Mwakifugile kudai kuwa Ndossa ndiye aliyesimamia ujenzi wa majengo ya ofisi za wakuu wa wilaya za Siha na Moshi.
Majengo hayo mawili yanadaiwa kugharimu mabilioni ya shilingi, lakini yalijengwa chini ya kiwango tangu yalipokamilika miaka mitano iliyopita na hayafai kwa matumizi ya kiofisi.
Hata hivyo, Ndossa alipotafutwa kuzungumzia madai hayo alishangazwa na kutuhumiwa kuwa alikuwa mtaalamu mshauri wa miradi hiyo.
Ndossa alisema waziri atakuwa amepewa taarifa potofu.
“Mimi sikuwa consultant (mtaalamu mshauri) wa ujenzi wa hilo jengo (la Siha). Consultant wa mradi walikuwa TBA, Makao Makuu…waliitumia ofisi ya Kilimanjaro mimi sikuwa Moshi.
“Nilikuwa nakwenda kule kusaidia tu. Wakati wa kufanya Site meeting (vikao eneo la mradi). Mimi nilikuwa Arusha nitakuwaje consultant Kilimanjaro? Watakuwa wamempotosha Waziri,” alisisitiza Ndossa.
Licha ya kukana, wakati Dk Magufuli akikagua jengo la ofisi ya mkuu wa Wilaya Siha, alielezwa kuwa, ujenzi wa jengo hilo uliokuwa chini ya viwango na ulisimamiwa na Ndossa .
HABARILEO
Baraza la Maadili ya viongozi wa umma limesitisha kusikiliza mashauri mawili likiwemo la Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Philip Saliboko hadi pale Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi juu ya uhalali wa mashauri hayo, kusikilizwa na baraza hilo.
Shauri lingine lililositishwa kusikilizwa na baraza hilo ni la aliyekuwa Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma ambaye pingamizi aliloweka lilikubaliwa kutokana na kuwa na kesi ya jinai Kisutu inayofanana na shauri linalomkabili mbele ya baraza hilo.
Baraza hilo lilifikia uamuzi huo, baada ya upande wa mlalamikiwa kuweka pingamizi la kuendelea kusikilizwa kwa mashauri hayo, lakini baraza hilo liliyatupilia mbali mapingamizi hayo yanayomhusu Saliboko, ndipo upande wa mlalamikiwa ulipoamua kukata rufaa Mahakama Kuu juu ya uamuzi huo.
Awali Mwenyekiti wa baraza hilo, Jaji Hamisi Msumi, alipinga na kulitupilia mbali pingamizi lililowekwa na wakili wa Saliboko, lililotaka baraza hilo lisitishe kusikiliza shauri hilo kwa kuwa halina uwezo wa kufanya hivyo kutokana na amri iliyotolewa mwaka jana Mahakama Kuu.
Akiwasilisha pingamizi hilo mbele ya Baraza hilo, Dar es Salaam jana, Wakili wa mlalamikiwa, Jamhuri Johnson, alisema kutokana na zuio lililowekwa na amri iliyotolewa mwaka jana katika shauri namba 51 la Mahakama Kuu, baraza hilo halina uwezo wa kuendelea na shauri hilo linalomkabili Saliboko.
“Katika amri ile inatokana na kesi ya msingi ya IPTL dhidi ya Waziri Mkuu na wenzake saba, ilikataza na kuweka zuio kwa vyombo vyovyote vya umma kujadili suala linalohusiana na IPTL na akaunti ya Escrow, hadi kesi ya msingi itakapoamuliwa,” Johnson.
Alisema anafahamu kuwa tayari baraza hilo lilishatolea uamuzi pingamizi kama hilo lililotolewa na Mbunge wa Bariadi Magharibi Andrew Chenge, lakini bado anaamini zuio hilo linalihusu pia na baraza hilo, hivyo halina uwezo wa kuendelea kusikiliza shauri hilo.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram, na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook