Baada ya wiki nzima ya makada wa CCM kutangaza nia na hatimaye kuchukua fomu za kugombea urais, wapinzani ndio wanaonekana kunufaika zaidi kutokana na wengi kutumia hotuba zao kuelezea udhaifu wa kila mmoja.
CCM imepanga mwezi mzima, kuanzia Juni 3 hadi Julai 2 kuwa ni muda wa makada wake kuchukua na kurudisha fomu kabla ya vikao vya juu vya chama hicho kukutana kuanzia Julai 12 kuchuja wagombea na baadaye kumpata mmoja atakayesimama kwenye Uchaguzi Mkuu kupambana na wa vyama vingine.
Tayari makada 15 wameshachukua fomu na wengine wanaendelea kuchukua, huku waliochukua wakiwa wameshaanza kuzunguka mikoani kutafuta wadhamini 30 kila mkoa ili kupata idadi ya wadhamini 450. Wanatakiwa kupata wadhamini kwenye mikoa 15, kumi ya Bara na mitano ya Zanzibar.
Karibu wagombea wote walizungumzia nia yao ya kupambana na rushwa, lakini walilitaja tatizo neno hilo kwa nia ya kuwashambulia baadhi yao huku maneno ya kuponda umaskini, kujisifu kwa utajiri, kukaa madarakani muda mrefu, ufisadi na masuala mengine yakitumika kupondana.
Makongoro Nyerere, mtoto wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, ndiye aliyetumia muda mwingi wa hotuba yake kijijini Butiama kuponda makada wote, akiwataja kwa majina kuanzia Edward Lowassa aliyeanza kutangaza nia baada ya kuruhusiwa na chama, Mwigulu Nchemba, hadi Steven Wasira, mwanasiasa mkongwe ambaye alianza kuwa waziri tangu miaka ya sabini.
Makongoro aliwaponda makada watatu waliojitokeza kwenye maeneo matatu ambayo ni matumizi ya fedha yaliyopindukia wakati hawana vyanzo vinavyoeleweka, ahadi zao kabla ya kutoka Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuwa serikalini kwa muda mrefu bila ya kufanya chochote.
Makongoro alisema viongozi wengi wanamyumbisha mwenyekiti wao, Jakaya Kikwete na kusema kama wanachama wa CCM wanataka chama hicho kisipotee, wampe nafasi ya kukirudisha kwenye njia.
Mgombea wa CCM anatarajiwa kukumbana na upinzani mkubwa zaidi ya mwaka 2010 baada ya vyama vinne-CUF, Chadema, NLD na NCCR Mageuzi- kukubaliana kusimamisha mgombea mmoja, huku vyama vingine nikionekana kujikita zaidi kwenye ubunge.
“Kwanza, kwa chama tawala kuwa na watu wengi wanaojitokeza kutaka urais, inaonyesha kuwa CCM haina mgombea,” alisema katibu mkuu wa zamani wa NCCR-Mageuzi, Sam Ruhuza alipoulizwa maoni yake kuhusu hali hiyo ya kupondana.
Miongoni mwa makada wa CCM waliotangaza nia au wanaotajwa kuwa wataingia kwenye mbio za urais wameshatajwa kwenye kashfa kadhaa zilizoikumba Serikali ya Awamu ya Nne, ambazo ni pamoja na Operesheni Tokomeza Ujangili, ubadhirifu ulioibuliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG), mkataba wa umeme wa dharura na kampuni ya Richmond, uchotwaji wa zaidi ya Sh306 bilioni kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow na EPA.
Hata hivyo, karibu wagombea wote wameahidi kupambana na rushwa, wakisema ndilo tatizo kubwa linalosumbua utekelezaji wa mikakati ya Serikali katika kuwahudumia wananchi.
MWANANCHI
Spika Anne Makinda amesema endapo Watanzania wataendekeza itikadi za udini na ukabila, Taifa litagawanyika na hakuna atakayenusurika na machafuko.
Makinda alisema kinachosikitisha kwa sasa ni uongo unaopandikizwa na wanasiasa juu ya tofauti mbalimbali zinazojitokeza, kama ilivyokuwa kwenye mchakato wa Katiba.
Kauli hiyo aliitoa jana wakati wa ibada ya maziko ya mbunge wa Ukonga (CCM), Eugen Mwaiposa aliyefariki dunia siku tano zilizopita kwa shinikizo la damu.
“Kuna kundi la watu wasioitakia mema nchi yetu, lakini hawana hoja. Wanasambaza na kuwapandikizia uongo wananchi, kwa mfano walieneza uongo kwenye Katiba Watanzania wakajigawa. Tusipokuwa makini tutagawanyika, Makinda.
“Ni ajabu sana mtu mwenye elimu na vyeo vyake akaonekana kuwa sehemu ya kuleta mpasuko kwenye jamii, lakini huyo ni shetani tu kwani tunaamini Mungu yupo…ni vyema kila mtu afikirie mchango wake katika jamii.”
Alikuwa akisisitiza maneno yaliyotolewa na Msaidizi wa Askofu wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Chediel Lwiza ambaye alimzungumzia Mwaiposa kuwa ni mtu asiye na ubaguzi, muadilifu na aliyejihusisha na jamii kwa karibu bila kujali makundi yao.
Mwaiposa jana alizikwa nyumbani kwake na wabunge walioongozwa na Spika Makinda, mameya na wakuu wa wilaya za Mkoa wa Dar es salaam.
Awali Askofu Lwiza alitoa tahadhari kwa Watanzania kuchagua kiongozi makini atakayelivusha Taifa kwenye mpasuko wa udini na ukabila.
Alionyesha masikitiko yake akisema kwa sasa hatari ukabila na udini, imeshaanza kuonekana kwenye jamii hususani katika kipindi cha uchaguzi.
JAMBOLEO
Mgombea wa nafasi ya Urais ambaye pia ni Naibu waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba amechukua fomu yay a kugombea Urais na kuweka bayana utajiri wake kwa kusema kwa sasa ana milioni tano kwenye akaunti yake.
Pia alisema Rais Jakaya Kikwete atakuwa Rais wa mwisho kuongoza Tanzania maskini kwani zipo rasilimali nyingi zilizogunduliwa nchini na endapo zitatumika vizuri zinatosha kuwaondoa wananchi kwenye umaskini.
Nchemba alitoa ufafanuzi wa utajiri wake baada ya kuulizwa swali na waandishi wa habari kuhusu mali anazomiliki.
“Wakati nimeshinda Ubunge wazazi wangu walikuwa wakiishi kwenye nyumba ya Tembe, nikawajengea nyumba na hivi sasa ndiyo namalizia nyumba yangu kule kijijini ambapo fedha za ujenzi wa nyumba hiyo nimekopa kwenye mafao yangu ya Ubunge” Mwigulu.
“Kwa upande wa Dar es salaam nina nyumba moja ambayo niliijenga wakati nafanya kazi BoT , lakini kwenye akaunti yangu hivi juzi juzi nilikuwa na milioni 5 na nilipunguza kutokana na hizi heka heka za uchaguzi”.
Alisema kwa sasa zimegundulika rasilimali nyingi ikiwemo gesi pamoja na madini yanayoendelea kugundulika kila mahali, zinatosha kuifanya nchi kuondokana na umaskini.
NIPASHE
Mnikulu Shabani Gurumo, aliyepokea asante ya Shilingi milioni 80.8 katika mgawo wa fedha za kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow, ametimuliwa kazi Ikulu.
Taarifa za kuondolewa Gurumo, zilitolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue , katika mahojiano na gazeti hili ambaye alisema kuwa hatua hiyo ilichukuliwa wiki moja iliyopita.
Gurumo aliyekuwa na wadhifa wa Ofisa Mkuu wa Ikulu, alikiri kupokea fedha hizo kutoka kwa mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing James Rugemalira, alipohojiwa na Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma.
Rugemalira alikuwa mzawa wa kampuni binafsi ya kuzalisha umeme ya IPTL ambayo pamoja na Tanesco zilifungua akaunti hiyo ya Escrow.
Fedha alizopokea Gurumo zinadaiwa kuwa ni sehemu ya zaidi ya Shilingi bilioni 300 zilizochotwa kifisadi katika akaunti hiyo, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Balozi Ombeni alisema hawana cha kumfanya kwa upande wao na kwamba Ofisi ya Utumishi wa Umma ndiyo yenye jukumu la kuamua kinachofuata dhidi ya mtumishi huyo. “Sisi hatuna cha kufanya zaidi ya kuondolewa Ikulu, Ofisi ya Utumishi itaamua nini kinachofuata.”
Awali Mnikulu huyo alipinga madai ya yeye kupewa zawadi hiyo ya Escrow na lakini alikiri kuwa alipokea Shilingi milioni 80.8 kutoka kwa Rugemalira kwa sababu za urafiki walionao kwa muda wa miaka 10 na hazihusiani na mgawo.
Aliwaambia wajumbe wa Tume ya Maadili kuwa aliyemuunganisha na Rugemalira, ni Dk. Fred Limbanga wa hospitali binafsi ya Sanitas, iliyoko Mikocheni, Dar es Salaam.
Alijieleza zaidi kuwa hata siku moja hajawahi kuwa na maslahi ya kiuchumi na Rugemalira, mbali na ya kifedha na pia hana uhusiano wowote na kampuni ya VIP Engineering and Marketing.
Akasema anahisi pengine Rugemalira alifanya hivyo kwa kuwa kipindi hicho alikuwa ana mgonjwa anayesumbuliwa na maradhi ya saratani.
Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ilitoa taarifa kuwa Shilingi bilioni 301 zilichotwa kwenye akaunti hiyo na kusababisha vigogo kadhaa akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema kujiuzulu.
NIPASHE
Askofu wa Jimbo Katoliki Rulenge mkoani Kagera, Severine Niwemugizi, amesema anamuunga mkono, kada wa CCM, Edward Lowassa katika safari ya matumaini.
Aidha amewahimiza Watanzania wanaofikiri wanazo sifa za kuwaongoza wananchi wajitokeze ili wapimwe uwezo wa kuitumikia nchi.
Mbali na hilo ameungana na Lowassa katika kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana ambayo mara nyingi amekuwa anaizungumzia.
Askofu Niwemugizi alitoa msimamo huo jana kwenye maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya seminari ndogo ya Mtakatifu Karoli Lwanga.
Alisema Watanzania wanajua Lowassa ametangaza nia ya kugombea urais kwa tiketi ya CCM na wanamuombea na kumtakia mafanikio katika safari yake hiyo.
“Tunatamani kuiombea nchi yetu iwapate viongozi makini, waadilifu, wakweli, watakaoongoza kwa misingi ya haki na usawa. Watakaoijenga jamii yenye kuaminiana na kuheshimiana, inayojali mema ya wote, watakaolinda amani na kudumisha umoja wa taifa,”
“Nimefurahi Lowassa kukubali mwaliko wangu, tumekualika wewe maana najua yatasemwa mengi yasiyo sahihi kwa kuja kwako huku, sote tunajua kuwa sasa ni joto kubwa la uchaguzi.”
“Wanaweza kufikiri nimekuita kukupigia kampeni katika safari yako ya matumaini uliyoitangaza kule Arusha, hayo siyo malengo yangu, ila wanaotaka kuliona hivyo basi juu yao, na kwanini sikuita mwingine ila wewe, nafikiri tuna uhuru wa kupanga na kuchagua,”alisisitiza.
Alisema amemualika Lowassa kumshukuru kwa kumpokea bila miadi, kumsikiliza wakati akiwa Waziri Mkuu mwaka 2007 na kutatua msigano wa ardhi ya Two Biharamulo iliyokabidhiwa na jeshi kwa askofu mtangulizi wake mwaka 1996.
Alisema alimuagiza Waziri wa Ardhi kipindi hicho Dk. John Magufuli, kulitatua na jimbo likapewa ardhi yake na sasa jimbo lina hati ya kumiliki ardhi hiyo hata kama ilipunguzwa kiasi.
Akizungumzia vijana, elimu na ajira alimwambia Lowassa:“Ujue kuwa tuko pamoja na wewe ndiwe mwasisi wa shule za kata, sasa zina wanafunzi wengi sana, lakini wanapomaliza kidato cha nne wengi wao wanarudi vijijini na wanajikuta hawana ajira, hali hii inawatesa sana na wana hasira.”
Akizungumza, Lowassa aliwaomba kuendelea kumuombea kwa sala na maombi ili Mungu akijalia katika safari yake ya matumaini kazi ya kwanza iwe ni kuunda chombo maalum cha elimu kwa kushirikisha wadau na wataalam.
NIPASHE
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Sharif Hamad, anakusudia kuanzisha Wizara ya Mafuta na Gesi, ikiwa ni vipaumbele vyake akichaguliwa kuiongoza Zanzibar.
Hamad ambaye ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, ambaye CUF imemteua kuwa mgombea wa urais wa Zanzibar kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba, ameeleza hayo jana.
Sambamba na hilo aliahidi kuwa endapo atachaguliwa kuiongoza Zanzibar, atahakikisha kuwa Zanzibar inakuwa na shirika la ndege ndani ya kipindi cha mwaka mmoja ili kurahisisha safari na shughuli za kibiashara ikiwamo utalii.
Aliahidi kuitangaza Zanzibar kuwa bandari huru, sambamba na kujenga bandari mpya itakayotoa huduma bora kwa mwambao wa Afrika Mashariki.
Alisema Zanzibar inazo fursa nyingi za kuweza kunyanyua kipato cha wananchi na kwamba ataweka kipaumbele katika kuziibua na kuziendeleza.
Alisema katika kujenga mazingira bora ya uwekezaji, ataisimamia ipasavyo mamlaka ya vitega uchumi ili kuondosha vizingiti vinavyokwamisha uwekezaji.
Alifahamisha kuwa wapo wafanyabiashara wengi wa ndani na nje ya nchi wenye nia ya kuwekeza miradi mikubwa ya kiuchumi, lakini wamekwamishwa jambo ambalo ameahidi kulishughulikia mara akiingia madarakani.
Mapema akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa CUF Taifa Profesa Ibrahim Lipumba, alisema Baraza Kuu la Uongozi la CUF limeshawishika kumuidhinisha Hamad kuwa mgombea urais wa Zanzibar, kutokana na uwezo na nia ya dhati ya kuwatumikia Wazanzibari.
HABARILEO
Rais Jakaya Kikwete ameendelea kuaga Watanzania kila anapopata fursa ya kukutana nao, huku mafanikio ya miaka kumi ya uongozi wake yakijidhihirisha katika maeneo mbalimbali, ikiwemo katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambako Bajeti ya Serikali kupitia wizara mbalimbali imekuwa ikijadiliwa na kupitishwa.
Mwishoni mwa wiki hii akiwa jijini Stockholm nchini Sweden alikokwenda kwa ziara ya siku tatu, ambayo pia ni ya kwanza ya kuaga nchi wahisani, Rais Kikwete alikutana na Watanzania waishio nchini humo, ambako kabla ya kuwaaga, alielezea changamoto anazoziacha.
Rais Kikwete katika mazungumzo hayo, amesema Rais ajaye anakabiliwa na changamoto ya kuhakikisha Tanzania inayoundwa na Muungano wa nchi mbili, inaendelea kuwa moja kwa kudumisha umoja wa Watanzania na amani.
“Hapa tulipofikia lazima tuhakikishe Taifa linakuwa moja, kuna vyama na makabila mbalimbali, lakini lazima tuhakikishe nchi inabaki moja,” Rais Kikwete.
Rais Kikwete pia alielezea matumaini yake kuwa Tanzania itapata kiongozi mzuri na kuelezea mafanikio ambayo Serikali yake imeyapata na kutumaini kuwa yatadumishwa na kuendelezwa na Rais ajaye.
Uchumi Awali akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika uchumi alipokutana na Waziri Mkuu wa Sweden, Stefan Lofven, Rais Kikwete alisema uchumi wa Tanzania umekua kwa wastani wa asilimia 7, katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Mbali na kukua kwa uchumi wastani, pato la Taifa limekua kwa zaidi ya mara tatu, kutoka Dola za Kimarekani bilioni 14.4 hadi kufikia Dola bilioni 49.2 za Marekani.
Aidha, pato la mtu mmoja mmoja kwa mwaka 2005, wakati Rais Kikwete alipokuwa akiingia madarakani lilikuwa Dola za Marekani 375, lakini mwaka jana lilifikia Dola za Marekani 1,038.
Mafanikio hayo kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, zilisababisha Waziri Mkuu wa Sweden, Lofven, kuona umuhimu wa kuanzisha awamu nyingine ya uhusiano katika maendeleo, utakaoleta maana zaidi.
Hata hivyo, Rais Kikwete alipokuwa akizungumzia kasi ya kuondoa umasikini, alisema bado juhudi za kuondosha umaskini zinahitajika na zitafanikiwa kwa kuelekeza nguvu kwenye kilimo, ambacho ndicho kinachoajiri na kutegemewa na Watanzania wengi zaidi hasa wanaoishi vijijini.
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.