HABARILEO
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema watu 152 watafikishwa mahakamani mkoani Njombe kutokana na kujiandikisha mara mbili katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo mpya wa ‘Biometric Voter Registration Kit’ (BVR).
Aidha, imeeleza kuwa kata 130 zimeongezeka kutokana na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kufanya mabadiliko ya kiutawala katika kata, vijiji ,vitongoji na Mitaa hivyo kulazimu NEC kuhairisha kwa wiki moja uandikishaji wa daftari uliokuwa ukianza jana kwa baadhi ya mikoa.
Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Dk Sisti Cariah alisema hayo jana wakati akielezea kuahirishwa kwa wiki moja uandikishaji hadi Juni 16 mwaka huu kwa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Mara.
Alisema katika mkoa wa Njombe ambao Daftari hilo liko tayari na wiki ijayo litawekwa wazi kwa siku tano na kisha kufanyiwa marekebisho kwa siku moja na wamebaini watu 152 waliojiandikisha mara mbili.
Alisema watu hao wametenda kosa la jinai na watashtakiwa, huku akitoa onyo kwa watu kuacha kufanya hivyo kwani mashine za BVR zinagundua wanaojiandikisha zaidi ya mara moja.
Alisema mpaka sasa tayari wamepokea madaftari yaliyokamilika ya uandikishaji kwa mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma huku uandikishaji huo ukiwa umekamilika kwa asilimia 50 na wanatarajia kukamilisha uandikishaji mwezi Julai.
HABARILEO
Licha ya idadi kubwa ya makada wa CCM waliojitokeza na wanaoendelea kujitokeza kuomba ridhaa ya kuteuliwa kuwania urais kupitia chama hicho tawala, Rais Jakaya Kikwete anayemaliza muda wake amesema hana mgombea, hivyo asihusishwe nao.
Amesema baadhi wamekuwa wakiomba ridhaa yake, lakini hakuna aliyemkatisha tamaa huku akimtakia kila la heri anayejiona ana ubavu wa kutaka kumrithi baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Aidha, amesisitiza ana imani na chama anachokiongoza, kitafanya chaguo sahihi na mgombea wa urais atakayepeperusha vyema bendera ya CCM katika mchakato wa kumpata Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania baadaye mwaka huu.
Rais Kikwete alisema hayo juzi usiku katika mkutano wake na Jumuiya ya Watanzania waishio Uholanzi, uliofanyika katika hoteli ya Crownie Plaza mjini hapa.
Alisema hayo alipokuwa anaelezea hali ya kisiasa nchini na pia maandalizi yanayoendelea ya uchaguzi mkuu ujao na pia mchakato wa Kura za Maoni ya Katiba Inayopendekezwa.
Akizungumzia mbio za urais zinazoendelea kushika kasi, alisema hali ya kisiasa ya Tanzania ni shwari, licha ya kuwa kumekuwa na kishindo katika kuwania kumrithi.
“Nyumbani hali ni shwari, lakini kwa kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi kuna mengi yanayoendelea, hasa mchakato wa kuwania Urais… huko CCM mpaka leo (juzi) watu 15 walishachukua fomu, na wengine zaidi ya 15 ama wametangaza nia au wanakusudia kufanya hivyo. “Ndiyo demokrasia ndani ya CCM, lakini niwahakikishie acheni waumane, lakini mimi binafsi sina chaguo langu. Chama ndicho kitakachoamua na ninaamini kitatupatia kiongozi sahihi kwa saizi na hadhi ya CCM na huyu atatuvusha mpaka Ikulu,” .
“Nasisitiza chama chetu ni makini na kitatupatia mgombea makini. Mwenyezi Mungu atuepushie mbali ili tusipate kiongozi atakayeipeleka nchi pabaya,” alisema na kuwataka Watanzania hao kutokuwa na hofu juu ya mchakato huo ndani ya CCM.
HABARILEO
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira amesema iwapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitafanya kosa kumsimamisha mgombea mla rushwa, kitapoteza dola.
Wassira alisema kamwe wana CCM hawatakubali kupoteza dola, badala yake atateuliwa mtu safi.
Mgombea huyo alisema Watanzania hawana nchi, ambayo iko sokoni na akaongeza kuwa kama Tanzania ingekuwa inauzwa, wangetangaza zabuni ya kuinunua, hivyo akawataka wagombea wenzake wanaotumia rushwa, kuacha.
Alisema yeye hatoi rushwa na anatafuta wadhamini mikoani kwa kutumia gari na sio kupanda ndege au helikopita.
Alisema hadi jana alikuwa ameshapata wadhamini kutoka mikoa 15 na akasisitiza kuwa atazunguka nchi nzima, kusaka wadhamini kwa kutumia gari lake.
Hata hivyo, Wassira aliwasihi wagombea urais wa CCM ambao wametangaza nia na wale ambao wamechukua fomu kuomba kugombea urais, wasigombane kwani kufanya hivyo kutawanufaisha wapinzani.
Alisema ugomvi wa miongoni mwa wana CCM, uliwanufaisha wapinzani katika majimbo ya Kawe na Ubungo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, hali ambayo ilisababisha CCM kupoteza majimbo hayo kwa vile tu wagombea waliingia kwenye ugomvi.
“Mimi nagombea na sitaki kugombana na mtu na nawasihi wenzangu wengine pia tusiingie kwenye ugomvi kwani kufanya hivyo wapinzani watapita katikati yetu na kushinda uchaguzi,” Wassira.
Wassira alisema ana hakika atashinda na atakipokea kijiti kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete na akawataka wana CCM, waamua kwa haki na sio kwa rushwa. “Haki itapatikana katika mazingira tulivu na sio mazingira ya rushwa,” alisema Wassira.
NIPASHE
Mgomo wa wanafunzi wa vitivo vya Sayansi ya Afya vya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala(KIU)– tawi la Dar es Salaam, umesababisha chuo hicho kufungwa.
Mgomo huo uliokwenda sambamba na maandamano ya wanafunzi, ulisababisha Polisi kuingilia kati na kupambana na wanafunzi hao na baadaye uongozi wa chuo kikifunga kwa muda usiojulikana.
Wanafunzi hao waligoma kufanya mitihani kutokana na uongozi wa chuo kushindwa kushughulikia usajili wa kozi za famasia, maabara na udaktari.
Mmoja wa wanafunzi wa shahada ya udaktari mwaka wa pili, alisema wameamua kugomea mitihani kutokana na kutojua hatma ya kozi wanayosoma kama imesajiliwa hivyo kuushinikiza uongozi kuhakikisha kozi hizo zinafanyiwa usajili.
“Uongozi umekuwa ukitupa ahadi ya kushughulikia madai yetu kwa muda mrefu, cha kushangaza hadi sasa hakuna majibu ya kuridhisha juu ya usajili wa kozi zetu,”.
Aidha, alisema uongozi wa chuo umeshindwa kuwatatulia matatizo hali inayosababisha migomo isiyokwisha.
Naye, mwanafunzi wa Shahada ya Famasia mwaka wa pili, alisema tangu Baraza la Famasia liwape siku 10 kusajili kozi hadi leo kozi yao haijafanyiwa usajili.
Rais wa KIU, Elias Mbogho, alisema wanafunzi wachache wa kozi ya Famasia ndiyo wanawashawishi wenzao kugomea mitihani akisisitiza usaili wa kozi hiyo umefikia katika hatua nzuri.
“Mgomo unaofanyika hauwahusishi wanafunzi wote wa vitivo vya Sayansi ya Afya, bali wanafunzi wa famasia wanachochea mgomo,” alisema.
Kwa mujibu wa Afisa Masoko na Mahusiano wa chuo hicho, Kenneth Uki, kutokana mgomo huo wanafunzi wanne walijeruhiwa na kutibiwa katika zahanati ya KIU kufuatia vurugu zilizozuka juzi chuoni hapo.
Uki, alisema mgomo huo ulisababisha uharibifu wa milango minne na madirisha 75 ambayo hadi sasa thamani yake haijajulikana.
Alisema wanafunzi wanane walikamatwa na polisi na kupelekwa katika Kituo cha Polisi Stakishari-Ukonga.
MTANZANIA
Siku moja baada ya Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee (Chadema), kumlipua Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, akidai kuwa amekuwa dalali wa viwanja, hatimaye amejibu mapigo na kusema kusakamwa kwake kunatokana na msimamo wake dhidi ya wa wanywaji pombe wilayani Rombo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, alisema kauli ya Mdee imejaa siasa, hasa kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, lakini hatorudi nyuma.
Alisema pamoja na kusakamwa kwake ndani ya Bunge na wapinzani, alishangazwa na hatua ya kuhusishwa na kufunguliwa kwa Soko la Kati mjini Moshi, ambalo awali lilikuwa limefungwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), akisema huenda itakuwa imeongeza hasira, hasa baada ya upinzani kushindwa kuwatetea wanyonge.
“Ninapenda kusema kuwa sitoruhusu upikaji wa gongo uendelee kwenye mkoa wangu, na nitaendelea kupambana na hilo, sasa naona msimamo wangu na jitihada ambazo nimekuwa nikifanya imekuwa nongwa, mimi najiamini ni msafi, sina wasiwasi katika hilo,” alisema Gama.
Alisema anashangazwa na kauli ya Mdee kudai kuwa ameshirikiana na Kampuni ya Jun Yu Investment International ya nchini China, kutaka kumiliki ardhi iliyokwishalipiwa fidia na Halmashauri ya Wilaya ya Rombo ya Sh milion 168 kinyume cha sheria.
Gama alisema alifanya juhudi kiwanda cha saruji kujengwa Kilimanjaro kwa ajili ya kuinua uchumi pamoja na nafasi ya ajira, ambapo aliwaomba wawekezaji hao kujenga katika Wilaya ya Rombo katika eneo la halmashauri na sio la mwekezaji.
“Walipojenga kiwanda siyo mali yangu na wala sikuhusika kudalalia, ni mali ya halmashauri ambayo ilihusika pia kuwalipa fidia wananchi ambao walikuwa na eneo hilo,” alisema Gama.
Alisema hana hisa kwenye kampuni hiyo huku akikiri mtoto wake Muyanga Gama, kuwa ni mmoja wa wanahisa katika kampuni hiyo ambapo ni haki yake kisheria kutokana na makubaliano waliyofikia na wenzake.
“Kama kweli nilikuwa nimehongwa shilingi milioni 500 ungekuta nimebaki kwenye ukuu wa mkoa? Na kama hizo fedha zipo naomba wazilete, na pia suala la hisa ni haki yangu, lakini katika hiki kiwanda cha saruji sina hisa hata moja,” alisema.
Kwa upande wa eneo la Lokolova alisema tayari limeshabadilishwa kutoka eneo la kilimo na ufugaji kwenda viwanda na biashara na kinachosubiriwa ni mkopo kutoka Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB), ambapo kila hatua inasimamiwa na mkoa.
“Kitu kikishasemwa bungeni hata kama siyo kweli unayetajwa huna sehemu ya kuzungumzia, ila ukweli wawekezaji wa Rombo walikuwa wanataka kwenda kuwekeza Bagamoyo, ndiyo nikamwambia mwanangu pamoja na wenzake ambao walikubali kuwekeza hapa,” alisema.
Kuhusu kutajwa kuhusika katika kiwanja cha Mawenzi chenye hati namba C.T 056035 kilichopo chini ya Mawenzi Sport Club, alisema kilichofanyika ni suala la kisheria.
Alisema sheria za ardhi, mmiliki akishajenga na kuwa na hati, hata asipolipia miaka 100 bado eneo litaendelea kuwa ni mali yake na ndiyo kilichotokea eneo la Mawenzi.
“Manispaa hawakutaka kutekeleza sheria ya ardhi, na wamiliki walitaka kwenda mahakamani kushitaki manispaa na mimi sikuwa tayari kwa hilo, na kama madiwani walitaka kutetea haki wangetoa mapendekezo kwa rais afute hiyo.
“Madiwani wamepeleka kesi mahakamani,wakachangishana fedha kudai eneo kuwa ni lao, lakini wameshindwa mahakamani, mbona hawasemi kama walishindwa na mimi sitoi haki kwa upendeleo kwa kuwa manispaa ni Serikali, hapana,” alisema.
Juzi Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mdee, alidai kuwa Gama anahusika na ufisadi wa kutaka kumiliki ardhi katika maeneo mbalimbali, ikiwamo Wilaya ya Rombo mkoani humo.
Kutokana na hali hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imemwomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kuzuia mchakato wowote haramu utakaofanywa na Gama kuhusu ardhi.
MTANZANIA
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ameendelea kutesa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa anakopita kutafuta wadhamini akitafuta kuteuliwa mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Lowassa alianza kusaka wadhamini alipotua mkoani Mwanza wiki iliyopita ambako alipata mapokezi makubwa huku maelfu ya wana CCM wakijitokeza kumdhamini.
Hadi sasa Lowassa ametembelea mikoa ya Mwanza ambapo alidhaminiwa na wanachama 2676 , Geita, Mara, Mjini na Magharibi Zanzibar na Kaskazini na Kusini kisiwani Pemba.
Jana aliingia Mkoa Mara akitokea Mkoa wa Geita na kupata mapokezi makubwa katika uwanja wa ndege wa mjini Musoma saa 5.00 asubuhi.
Kabla hata Lowassa hajawasili Musoma, tayari watu wengi walikuwa wakimsubiri katika uwanja wa ndege, huku waendesha pikipiki (bodaboda) na magari mbalimbali yakiwa yamepangwa kwa ajili ya msafara wake.
Wanachama hao walimzuia Lowassa na msafara wake aliyekuwa akienda kwenye ofisi ya CCM mkoa huku wakitaka kwanza azungumze nao.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Christopher Sanya, aliwazuia akisema kanuni za chama kwa sasa haziruhusu Lowassa kuhutubia kwa vile muda wa kampeni bado.
Baada ya kutoka katika ofisi ya CCM mkoa, Lowassa alikwenda wilayani Butiama katika Kijiji cha Mwitongo nyumbani kwa hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.
Alipokewa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Annarose Nyamubi na watoto wa Mwalimu Nyerere, Madaraka na Andrew na Chifu wa ukoo huo, Japhet Wanzagi.
Akiwa Mwitongo, mtoto wa Mwalimu Nyerere, Andrew, ndiye alizungumza kwa niaba ya familia kwa kumkaribisha Lowassa.
Hata hivyo Mama Maria Nyerere hakuwapo kwa kile kilichoelezwa na Madaraka Nyerere kuwa yuko Dar es Salaam kwa muda mrefu.
Lowassa na msafara wake walipata nafasi ya kuzuru kaburi la Mwalimu Nyerere kabla ya kutembelea msiba wa dada yake Mwalimu Nyerere, Tagaz na mpwa, John, waliofariki dunia juzi.
Baada ya kutoka Butiama, msafara wa Lowassa ulielekea wilayani Bunda. Hata hivyo ilibidi usimame katika Kijiji cha Bitaraguru baada ya wana CCM na mashabiki kuusimamsha wakitaka azungumze nao.
Akizungumza na wana CCM hao, Lowassa aliwataka kumwombea katika safari yake ya matumaini.
“Asanteni kwa maokezi makubwa mliyonipa. Naomba mniombee mambo yangu yawe mazuri. Naenda na natamani kuwahutubia ila muda hautoshi, nitarudi mambo yatakapokuwa mazuri. Nawaomba wenye misalaba, rozari mpige magoti mniombee,” alisema Lowassa.
Akizungumza katika ofisi ya CCM Wilaya ya Bunda, Mbunge wa Mwibara, Alfaxard Kangi Lugola alisema, “wananchi wa wilaya hiyo wameacha kazi zao ili kuja kupakia gari lako la matumaini.
“Hii inanikumbusha maandiko ya Biblia ambako Yesu aliwauliza wanafunzi wake, Je, watu wananinenaje huko nje? Wanafunzi wake wakajibu, wengine wanakuita Eliya, wengine Yohana Mbatizaji. Akauliza tena, na ninyi mnaninenaje? Wakajibu, Wewe ni Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai.
“Tulipokuwa ofisini Lowassa uliniuliza lakini sasa umeona jinsi watu wanavyokunena hapa.”
Lugora alisema wananchi hao wameridhishwa na kazi ya Lowassa alipokuwa Waziri wa Maji ya kutoa maji kutoka ziwa Victoria kuyapeleka kwa wananchi.
Lowassa alipata wananchama 617 waliomdhamini.
Bunda ni jimbo la Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira ambaye pia amechukua fomu ya kugombea urais kupitia CCM.
MWANANCHI
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Njombe kimejipanga kuchukua majimbo yote matano ya mkoani hapa katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha), Emmanuel Masonga alisema kuwa katika kuhakikisha ushindi huo, chama hicho kinajipanga kwa ajili ya kuwapata wagombea wanaokubalika na watu.
“Tumejipanga vizuri kuchukua majimbo yote ya Mkoa wa Njombe, tuna watu makini na wasomi waliotangaza nia kwa ajili ya kugombea na tuna imani kuwa kupitia hapa, tutapata watu wazuri watakaopeperusha bendera ya chama hicho na tutawaunga mkono,” alisema Masonga.
Aliwataka wakazi wa majimbo yote ya Mkoa wa Njombe ambayo kwa sasa yanawakilishwa na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukipa kura chama hicho katika Uchaguzi Mkuu ili kupata uwakilishi madhubuti na wenye tija kimaendeleo.
Alisema wakazi wa Njombe hasa wa Jimbo la Njombe Kusini linaloongozwa na Spika wa Bunge Anne Makinda, kwa muda mrefu wamekosa uwakilishi wa kweli, baada ya mwakilishi wao kushindwa kuwatembelea jimboni na kujua matatizo kutokana na shughuli nyingi zinazomkabali.
“Makinda anafika kwenye misiba na wakati wa kampeni tu hana muda wa kusikiliza matatizo ya wananchi,” alisema Masonga.
Majimbo mengine yanayowaniwa na Chadema ni Wanging’ombe linaloongozwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Gerson Lwenge na Jimbo la Makete la Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Dk Binilith Mahenge, Njombe Kaskazini linaloongozwa na Deo Sanga na Jimbo la Ludewa aliko Deo Filikunjombe.
Hata hivyo, Masonga alisema ikilinganishwa na wabunge wengine, Filikunjombe kuna jambo alilofanya katika jimbo la Ludewa, lakini napo bado kuna kazi ya kufanya ndiyo maana Chadema wanajipanga kulichukua.
“CCM katika Ilani yao waliahidi kupeleka lami Ludewa na Makete, lakini wameshindwa kufanya hivyo. Kwa hiyo kwa sasa sisi wa Chadema tunawaomba wananchi watupe ridhaa tuwawakilishe ili tukaisimamie Serikali kwa ajili ya maendeleo baada ya wabunge wa CCM kushindwa,” alisema Masonga.
Wakati Chadema ikiweka mikakati hiyo, CCM wameendelea na kampeni zake za chini chini kuyatetea majimbo hayo.
MWANANCHI
Makada watatu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) akiwamo wa darasa la saba, jana walijitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kuomba kuteuliwa na chama hicho wagombee urais.
Waliojitokeza ni Dk Mwele Malecela, Dk Hamis Kigwangalla na Elidephonce Bilole mwenye elimu ya darasa la saba ambao walifika Makao Makuu ya CCM kati ya saa nne asubuhi na saa saba kwa staili tofauti kwa ajili ya kuchukua fomu hizo.
Hata hivyo, Bilole (43) aliyetembea kwa miguu huku akiwa amebeba chupa mbili za maji, mfuko wa plastiki na begi dogo jeusi, hakuweza kuchukua fomu kutokana na kufika katika ofisi hizo akiwa hana Sh1 milioni za malipo.
Baadaye alifanikiwa kulipa ada hiyo na sasa amepangiwa kuchukua fomu yake leo saa 10.00 jioni.
“Nilikuwa Benki ya CRDB, nikaitwa ofisi za chama nikaona nije ili nisikilize wito, kabla ya kuchukua fedha kwanza,” alisema Bilole aliyefika peke yake kwenye ofisi hizo.
Bilole alisema anajua Mungu atamwezesha kukabiliana na watu wengine walioomba ridhaa ya chama kuwania nafasi hiyo.
Alipoulizwa sababu ya kufika pekee yake katika ofisi hizo, alisema hajawahi kuwa na makundi ambayo yameonekana kwa makada wengine… “Nadhani naweza ndiyo maana nimejitokeza kuwania nafasi hii. Nitawavusha kuwapeleka kwenye nchi ya ahadi,” alisema na kuongeza kuwa alijiunga na chama hicho mwaka 2003 huku akiahidi kuhakikisha anainua uchumi wa nchi kwa kutumia rasilimali zilizopo.
Baada ya kuchukua fomu hizo, Dk Kigwangalla alieleza vipaumbele vitatu alivyosema atavitekeleza. Aliyataja mambo hayo kuwa ni kupunguza wigo wa walio nacho na wasionacho, kukabiliana kisayansi na mabadiliko ya tabianchi katika uchumi na kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.
“Tanzania ya leo haiwezi kuendelea kwa fikra zilezile, watu walewale… tunalia na amani, umoja na upendo, lakini bado kuna haja ya kuwa na mabadiliko. Lazima tufikiri upya, lazima kuwa na mustakabali mpya wa Taifa la Tanzania,” alisema Dk Kigwangalla.
MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete amesikitika kushindwa kukuza sekta ya kilimo hali iliyosababisha wananchi kuendelea kuwa maskini.
Kutokana na hali hiyo ameziomba nchi wahisani kusaidia kuendeleza kilimo cha Tanzania kwa kuwa ndiyo sekta inayotoa ajira kwa Watanzania wengi hasa waishio vijijini.
Rais Kikwete alisema hayo jana nchini Uholanzi alipozungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Bert Koenders.
“Nasikitika sikuweza kubadilisha sekta ya kilimo inayohitaji kupewa msukumo zaidi,” alisema Rais Kikwete huku akitumia nafasi hiyo kuishukuru Uholanzi kwa misaada ya maendeleo inayoisaidia Tanzania.
“Kilimo kinategemewa na wengi, lakini hakijakua kwa kiwango cha kuridhisha na wala hakijapewa kipaumbele.
Alisema ni vyema wahisani wakaendelea kusaidia hata baada ya kutoka madarakani ili kupunguza umaskini.
Rais Kikwete alisema misaada iliyotolewa haijapotea kwa kuwa juhudi za kukuza uchumi katika nyanja mbalimbali zimefanikiwa kwa kiwango kikubwa, licha ya kuwapo kwa mfumuko wa bei uliotokana na msukosuko wa uchumi wa dunia mwaka 2011.
Wakati huohuo, Rais Kikwete alikutana na Jumuiya ya Watanzania waoishi Uholanzi (Tane), ambao walisema wanapenda Serikali ijayo iendeleze juhudi za kukuza uchumi katika hatua iliyofikiwa na Serikali yake.
“Tunajua kuna mambo mengi hautayakamilisha, basi tunaomba uyakabidhi kwenye utawala unaofuata ili atakayeshika madaraka aendeleze pale utakapokuwa umefikia,” alisema Makamu Mwenyekiti wa Mpito kutoka Tane, Johannes Rwanzo katika risala yao.
Rwanzo aliyataja baadhi ya mambo yanayohitajika kuendelezwa na awamu ijayo kuwa ni juhudi za kupambana na umaskini nchini na ujenzi wa miundombinu.
Watanzania hao walimuomba Rais Kikwete aendelee kutoa msaada kwa wananchi licha ya kwamba anastaafu.
MWANANCHI
Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Pius Msekwa amewataka wananchi kutoshtushwa na msululu wa makada wa chama hicho waliojitokeza kutangaza nia ya kugombea urais, akisema chama kitampata mgombea makini asiye na doa miongoni mwao.
Alisema hata kitendo cha baadhi ya wakongwe wa chama hicho kujitokeza na kuwaunga mkono baadhi ya wagombea, kinaonyesha ukomavu wa demokrasia.
“Haijalishi wamejitokeza wagombea wangapi hadi sasa inaweza kuwa kama foleni ya magari. Hata watu waliopo kwenye kambi zao kujionyesha sioni tatizo lolote binafsi, kwani mwisho wa siku nakiamini chama kitatoa mgombea mwenye sifa atakayekubalika na wananchi wengi,” alisema Msekwa na kuongeza:
“Kama angejitokeza mgombea akiwa ameongozana na mkewe tu au mumewe na kutangaza nia yake ni wazi wengi tusingemuelewa, tungeweza kumwambia basi mwambie mkeo au huyo mumeo akupigie kura. Kujitokeza na wapambe wao kunawafanya wajipime wenyewe jinsi wanavyokubalika hayo yasiwasumbue kabisa,” anasisitiza.
Wanasiasa wakongwe nchini, akiwamo Kingunge Ngombale Mwiru, wamekuwa wakijitokeza kama wapambe wa baadhi ya wagombea urais.
Mbali na Kingunge, mkongwe mwingine aliyejitokeza kwenye mikutano ya kutangaza nia ya baadhi ya wagombea hao ni George Kahama.
Kingunge alijitokeza kwenye mkutano wa kutangaza nia wa Mbunge wa Monduli Edward Lowassa na Kahama aliibuka kwenye mkutano wa Benard Membe.
“Hili nalo lisiwatishe, hii inaonyesha kukua kwa demokrasia,” alisema Msekwa.
Akizungumza katika mkutano huo Kingunge alisema ili CCM isiyumbe, kinahitaji mwanasiasa mwenye kuweza kufanya maamuzi magumu, mkongwe wa siasa na anayeijua vizuri nchi.
“Tunamtaka pia kiongozi anayepinga rushwa kwa vitendo na huyo ni Lowassa,” alisema
MWANANCHI
Huku ikionekana dhahiri kuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limemlazimisha mshambuliaji Ramadhani Singano ‘Messi’ kubaki Simba, mchezaji huyo alibubujikwa machozi hadharani huku akisema analiacha jambo hilo mbele ya Mungu.
Singano aliangua kilio wakati katibu mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa alipotoa uamuzi wenye utata kuhusu kimkataba ambao umegeuka kizungumkuti baina ya mchezaji huyo na klabu yake, Simba.
Singano amekuwa akiilalamikia Simba kuwa imeghushi mkataba wake wa miaka miwili alioingia nayo kwa kumwongeza mwaka mmoja zaidi katika mkataba wake wa awali.
Simba, kupitia uongozi wake, akiwamo makamu rais, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na mwenyekiti wa kamati ya usajili, Zacharia Hanspoppe imekuwa ikijibu mara zote kuwa ilikuwa na mkataba halali wa miaka mitatu na mchezaji huyo, ikieleza kuwa utamalzika mwakani, 2016.
Jana, uamuzi ya kikao kilichokaa kujadili suala hilo umekuwa wa kukanganya baada ya TFF kushindwa kutoa majibu, hasa ya upande upi ulighushi mkataba.
Katika uamuzi wake TFF imezitaka pande mbili kukaa mezani na kuanza makubaliano ya kusaini mkataba mpya, jambo linaloashiria kuwa mchezaji huyo ameibuka mshindi kwenye malalamiko yake.
Akisoma uamuzi uliofikiwa kwenye kikao hicho cha usuluhishi, Mwesigwa alisema kuwa kikao hicho kilibaini kuwa kulikuwa na utata kwenye baadhi ya vipengele vya mikataba yote miwili iliyowasilishwa mbele ya shirikisho hilo, ambayo ni ule wa Simba pamoja na ule wa Singano
“Katika kikao chetu, pande zote zimeeleza kutambua utata uliojitokeza kwenye mikataba yote miwili. Kwa mantiki hiyo, pande zote zimekubaliana kuanza mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya utakaojumuisha yale yaliyokosekana kwenye mkataba wa awali,” alisema Mwesigwa.
Alipoulizwa kuhusu mkataba ulioko mbele yao (TFF) na jinsi unavyosema, Mwesigwa alijivua kuwa kikao hicho hakikuwa cha kumpata mshindi, bali kilikuwa mahususi kwa ajili ya kutolea ufafanuzi vipengele vilivyomo kwenye mikataba iliyowasilishwa kwao na pande mbili zinazokinzana.
Hata hivyo, huku akitoa machozi kuonyesha kutoridhishwa kwake na uamuzi ya kikao hicho, Singano alisema kuwa anamwachia Mungu suala hilo na atalazimika kufanya kile ambacho wamekubaliana.
“Uamuzi wametoa kuwa mimi nifanye mazungumzo na Simba, je, ikitokea kuwa mimi sijaelewana nao itakuwaje?
Hilo ndilo swali nililouliza, hivyo huku wao wakinijibu kuwa ni lazima tutakubaliane, ingawa najua kama hatutokubaliana tena.
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.