MWANANCHI
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki amewataka waliovamia na kujigawia maeneo ya watu wengine likiwamo la Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Ritha Mlaki waondoke mara moja kwa kuwa wamevunja sheria.
Alisema zaidi ya watu 2,000 wakiwamo waliobomolewa nyumba katika baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam wamevamia na kujigawia mashamba hayo yaliyopo Tegeta na Goba kinyume cha sheria.
“Kisa wamevunjiwa nyumba zao walizojenga kinyume cha sheria ndiyo wameamua kuvamia maeneo yasiyo yao, hili ni kosa kama makosa mengine, nawataka waondoke haraka vinginevyo tutawachukulia hatua kali za kisheria,” alisema mkuu huyo wa mkoa.
Alisisitiza kuwa agizo la Rais John Magufuli lilikuwa ni maeneo yaliyoachwa wazi kuainishwa kwa ajili ya kupangiwa matumizi mengine na siyo kuruhusu watu kuvamia bila taratibu.
Hakuna viwanja Sadiki alisema hakuna viwanja vilivyotengwa kwa ajili ya kuwagawia wananchi waliokumbwa na bomoabomoa katika maeneo ya mabondeni.
Zaidi ya nyumba 8,000 zilizojengwa kwenye Bonde la Mto Msimbazi, fukwe za bahari na kando ya mito zimeanza kubomolewa kabla ya kusitishwa na Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi.
Sadiki alisema wananchi waliobomolewa nyumba zao na ambao watakumbwa na operesheni hiyo wasitarajie kupatiwa viwanja vya kujenga nyumba zao.
Bomoabomoa hiyo inaendeshwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ikiwalenga waliojenga kinyume cha sheria.
“Serikali haina viwanja vinavyotosha kuzigawia familia zaidi ya 8,000 zitakazobomolewa, niwashauri tu wasiendelee kupoteza muda wao kwa kuwasikiliza wanasiasa, watafute makazi mengine waende. Kama walivyovamia na kujenga ndivyo wanatakiwa kutafuta maeneo mengine wahamie,” alisema Sadick.
Alisema viwanja 1,007 vya Mabwepande vilitolewa kwa wananchi waliokumbwa na mafuriko mwaka 2011 ambao waliwekwa kwenye kambi baada ya kukosa makazi. Alisema kaya zote zilizokosa makazi kutokana na mafuriko hayo zilipatiwa maeneo. Waathirika 580 walitokea Ilala, Kinondoni 349 na Temeke 81.
“Kuna upotoshaji unaendelea kwamba yapo maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kuwapatia wanaobomolewa sasa, jambo hili halina ukweli, ikumbukwe tuligawa viwanja vya Mabwepande baada ya Rais (Jakaya Kikwete) kuagiza tufanye hivyo ili kuwasaidia wale tu, waliokumbwa na mafuriko,” alisema.
Sadiki alisema kinachoendelea kwenye eneo la Mabwepande ni uandaaji wa hati za viwanja na tayari kaya 102 zimeshapatiwa. Alisema Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) iliikopesha Manispaa ya Kinondoni zaidi ya Sh17.5 bilioni kwa ajili ya kupima viwanja katika eneo hilo.
MWANANCHI
Wakati NEMC ikianza tena ubomoaji wa nyumba zilizoko kwenye maeneo ya mabondeni, Mahakama Kuu imeifunga mikono Serikali kwa muda kuendelea na operesheni hiyo kwa wakazi 674 waliofungua kesi kupinga bomoabomoa.
Uamuzi huo wa Mahakama Kuu utahusu nyumba za wakazi hao tu, lakini Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linaloendesha ubomoaji huo, litalazimika kufanya kazi ya ziada kutambua nyumba za wanaohusika na amri hiyo kutokana na majina yao kutojulikana hadi wakati amri hiyo ikitolewa.
Wilayani Temeke, wananchi walimpeleka mbunge wao hadi eneo la Keko na kumuonyesha jengo linaloziba barabara tatu, wakisema operesheni hiyo itakapowafikia, ianze na jengo hilo walilosema ni kero kwa wakazi wa Keko, Chang’ombe na sehemu nyingine waliokuwa wanatumia barabara hizo.
NEMC ilisitisha operesheni ya ubomoaji nyumba zilizojengwa kwenye maeneo ya wazi, fukwe, kingo za mito na mabondeni na kutoa siku 14 kwa wakazi kuhamisha vifaa vyao na kubomoa nyumba.
Muda huo ulimalizika jana na kazi hiyo ilianza tena bila ya kuwapo vikwazo kutoka kwa wananchi kama ilivyokuwa mwanzoni.
Lakini wakazi saba waliofungua kesi kwa niaba ya wenzao zaidi ya 670, walikuwa wameelekeza nguvu kwenye vyombo vya sheria, kupinga kubomolewa nyumba bila ya kuonyeshwa makazi mbadala huku wakiomba mahakama kutoa amri ya kuzuia ubomoaji hadi hapo shauri lao litakapoamuliwa.
Maombi hayo ya Ali Kondo Mshindo na wenzake sita katika kesi hiyo inayosikilizwa Kitengo cha Ardhi cha Mahakama Kuu yalitolewa uamuzi jana.
“Nimeridhika kuwa katika shauri hili kwa misingi ya haki, utawala bora na sheria kuna watu wanastahili haki ya kusikilizwa kutoa hoja zao kwa nini wanataka kufungua kesi kwa niaba ya wenzao,” alisema Jaji Penterine Kente anayesikiliza kesi hiyo baada ya mawakili wa pande zote mbili kutoa hoja zao.
“Lakini kwa kuwa uvunjaji wa nyumba zao unaweza kuendelea, nimeona kuna sababu ya msingi ya kutoa amri ya zuio kwa wajibu maombi wasimamishe ubomoaji kusubiri kusikilizwa kwa maombi namba 822,” aliongeza.
Jaji Kente alisema amri hiyo ya zuio itawahusu wakazi ambao wanahusika na kesi hiyo tu na kwamba ubomoaji na uwekaji alama za X unaweza kuendelea kwa wasiohusika. “Katika kuondoa mashaka, amri hii ya mahakama inawahusu wale tu walioko katika kesi.
Hivyo Serikali haizuiwi kuendelea na zoezi la utambuzi, uwekaji alama na ikiwezekana hata ubomoaji wa nyumba katika maeneo mengine ambako hawahusiki katika kesi hii,” alisema Jaji Kente na kuongeza: “Wakili (anayewatetea watoa maombi, Abubakar) Salim awasilishe mahakamani leo hii orodha ya majina na anuani za makazi ya wale wote watakaohusika katika kesi itakayofunguliwa, ili zuio la kutovunjwa kwa nyumba zao litekelezwe kwa urahisi.
” Baada ya kusoma uamuzi huo Jaji Kente aliahirisha shauri hilo hadi Jumatatu wakati maombi hayo ya kibali yatatajwa kwa ajili ya kupanga tarehe ya kuyasikiliza. Wajibu maombi katika shauri hilo ambao ni Manispaa ya Kinondoni, NEMC na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wametakiwa kuwasilisha mahakamani hapo hati ya kiapo kinzani keshokutwa.
Operesheni ya bomoabomoa ilianza Desemba mwaka jana kwa watu waliojenga bonde la Mto Msimbazi eneo la Mkwajuni na Magomeni kabla ya kuendelea na maeneo mengine, lakini ilisitishwa kwa muda Desemba 22 hadi Januari 5, mwaka huu. Lakini kabla ya muda huo wa siku 14, Desemba 28 wananchi hao walifungua kesi
MWANANCHI
Zaidi ya wakazi 1,500 wa kaya 250 katika Kitongoji cha Mbwamaji wilayani hapa Mkoa wa Morogoro, wamekumbwa na mafuriko baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha hasara ya vitu mbalimbali, ikiwamo nyumba kubomoka na uharibifu wa mali.
Mafuriko hayo licha ya kuharibu mali za kata hizo, pia yameharibu miundombinu ya barabara ya Mikumi hadi Kilosa na mazao ya aina mbalimbali katika mashamba yanayokadiliwa kufikia ekari 400.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mbwamaji, Abdallah Songoro (51) alimueleza Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Devotha Minja kuwa mafuriko hayo yamesababisha uhaba wa vyakula.
Songoro alisema mafuriko hayo yalianza kuingia katika makazi ya watu saa sita usiku juzi hadi jana saa tano asubuhi, baada ya kupasua kingo za Mto Mkondoa katika eneo la shamba la Magereza.
“Waathirika wote katika mafuriko haya wengi wao wanaishi katika majengo ya Mahakama ya Mwanzo, Shule ya Msingi Magomeni na jengo la boma la ofisi ya ofisa mtendaji wa kata na mpaka sasa hivi bado hatujapata taarifa ya kifo,”alisema Songoro.
Kwa upande wake, Minja aliyewatembelea wahanga hao baada ya kukagua eneo lililokumbwa na mafuriko, alisema Serikali inapaswa kutoa huduma za dharura haraka ili kaya hizo ziendelee na maisha yao.
“Nawapeni pole kwa tukio lililotokea, lakini kutokana na hali halisi nawaombeni msirudi tena kwa wale wenye nyumba ambazo hazijabomoka, kwani mvua inaweza kunyesha tena na kusababisha maafa,” alisema.
Mmoja wa waathirika hao, Jema Mduwile (25) alisema mafuriko hayo yalivamia katika makazi yao wakati wamelala na kazi ya kuwaokoa watoto ilikuwa ngumu kutokana na kasi ya maji.
“Nilifanikiwa kuwaokoa watoto wangu wote wanne kwa kuwabeba kutoka ndani ya nyumba hadi sehemu salama, namshukuru Mungu kwani maji yaliingia ndani wa kasi na kufikia usawa wa madirisha,” alisema.
MWANANCHI
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mohammed Kilongo na maofisa wa misitu wa mikoa nchi nzima kupisha uchunguzi wa upotevu wa mapato ya Serikali.
Profesa Maghembe alisema agizo hilo limetokana na ubadhirifu unaofanywa na maofisa wa ukusanyaji maduhuli ya Serikali yanayotokana na rasilimali za misitu katika mikoa na wilaya kutoyawasilishwa katika mfuko mkuu wa Serikali.
Ameagiza pia maofisa hao wanaokusanya maduhuli hayo katika wilaya, watumie siku 10 kuanzia jana, kuhakikisha maduhuli yote yaliyokusanywa yanapelekwa benki ikiwa ni pamoja na kukabidhi vitabu vya kukusanyia mapato kinyume cha hapo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Waziri Maghembe alisema Kilongo ambaye idara yake ndiyo inayotoa vitabu kwa ajili ya kukusanya maduhuli ya Serikali katika mikoa na wilaya zote, amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi.
Katika hatua nyingine, waziri huyo ameuapa uongozi wa TFS siku saba kurudi katika jengo la wizara ‘Mpingo House’ ambalo walihama mwishoni mwa Septemba mwaka jana na kwenda kupanga katika jengo la NSSF, Mafao House lililopo Ilala.
“Tumejenga jengo hili kama la misitu ndiyo maana linaitwa Mpingo House kwa maana ni jengo la misitu, ninyi wenyewe mmejenga jengo kubwa hili mmemaliza mmehama, naagiza hadi Januari 11 muwe mmesharudi katika jengo hili, ghorofa ya tatu nikija kukagua niwakute, haiwezekani mueleze matatizo yote mliyonayo mhame nyumba ya Serikali mkapange jengo hapo jirani,” alisema.
Katika hatua nyingine ya kuboresha uhifadhi wa misitu nchini, Waziri Maghembe ameiagiza Idara ya Misitu na Nyuki kuhakikisha inajiimarisha katika lengo lake kuu la uhifadhi kwa kushirikiana na wadau wanaohusika kuhakikisha mamlaka iliyolengwa ya uhifadhi misitu inakamilika.
“Tunataka tutoke kwenye wakala wa huduma za misitu twende kwenye mamlaka ya uhifadhi wa misitu ili tuweze kufanya vizuri zaidi kwenye eneo la uhifadhi na uendelezaji wa misitu nchini, katibu mkuu tunaomba pia usaidie kufanikisha hili,” alisema Profesa Maghembe.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi alisema maagizo yote yaliyotolewa na waziri yatafanyiwa kazi kwa kuwa lengo lake ni kuona dhamira ya msingi ya Serikali ya awamu ya Tano ya kubana matumizi, kuongeza mapato ya Serikali na kuhifadhi maliasili za Taifa ikiwamo misitu inafikiwa.
Mwigulu awasimamisha viongozi wa tumbaku Waziri wa Kilimo, Uvuvi na Mifugo, Mwigulu Nchemba amewasimamisha viongozi wa vyama vya msingi vya tumbaku mkoani Iringa wanaotuhumiwa kushiriki katika ufisadi wa mkopo wa matrekta tisa kupitia mgongo wa vyama vya msingi vya wakulima wa tumbaku na kujimilikisha wenyewe.
Nchemba alifikia hatua hiyo baada ya wakulima wa tumbaku kulalamikia viongozi wa vyama hivyo na kuwataka wakabidhi ofisi. Awali, mwanachama wa Chama cha Msingi cha Mfyome, Francis Kilatu alisema Benki ya CRDB inawakata fedha zao huku wamiliki wa matrekta hayo wakiwa ni wengine hivyo alimuomba waziri kulishughulikia mara moja.
HABARILEO
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kingwangalla amefanya ziara katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kuridhishwa na utendaji kazi hospitalini hapo.
Baadhi ya idara ambazo, Dk Kingwangalla alitembelea ni pamoja na Kitengo cha dharura, Chumba cha wagonjwa Mahututi (ICU), wadi ya Mwaisela, duka la dawa la MSD na kukagua ufanyaji wa kazi wa mashine ya CT-Scan na MRI.
Akizungumza mara baada ya kutembelea hospitalini hapo, Dk Kigwangalla alisema amefurahishwa na utoaji wa huduma katika upimaji kwa kutumia mashine ya CT-Scan na MRI ambazo awali wakati wanaingia madarakani hazikuwa katika hali nzuri ya ufanyaji wa kazi.
Amewataka watumishi wa hospitali hiyo kufanya kazi kwa bidii na kuifanya hospitali hiyo kuonekana yenye hadhi ya kuwa hospitali ya taifa. Alisema limekuwa jambo ambalo linasikitisha kuona huduma zinazopatikana katika hospitali ya taifa zinashindwa na huduma zinazotolewa katika hospitali za watu binafsi.
Amelinganisha huduma za kulipia vitanda zinazotolewa Muhimbili kuwa hazina viwango vya juu ambavyo vinaweza kuwashawishi wananchi wenye uwezo kuacha kwenda hospitali binafsi na kwenda hospitalini hapo.
“Ni jambo la kushangaza hospitali za watu binafsi zinakuwa na watu wengi kuliko hapa na wakati sisi tuna madaktari bingwa zaidi ya 500 hapa Muhimbili, lakini hizo hospitali zao hazina hata daktari mmoja bingwa lakini na huduma zinazopatikana katika madaraja ya juu zinatakiwa kuboreshwa.
Aidha Dk Kingwangalla aliwatupia lawama Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa jinsi wanavyopanga madaraja ya hospitali na kuilinganisha Muhimbili na hospitali nyingine za watu binafsi kuwa jambo hilo siyo sahihi kwa kuiweka hospitali ya taifa sawa na hospitali za watu binafsi.
Aidha Naibu Waziri aliupongeza uongozi wa hospitali hiyo kwa kuongeza vitanda katika wadi ya wagonjwa mahututi (ICU) ambayo awali ilikuwa na vitanda sita, hali ambayo ilikuwa ikiwashangaza wananchi wengi kutokana na kuwepo kwa vitanda zaidi ya 1,350.
Awali akitoa taarifa mbele ya Dk Kigwangalla, Mkuu wa Idara ya Mionzi katika hospitali hiyo, Dk Flora Rwakatare alisema tangu kuanza kwa kutumika kwa mashine ya MRI mwishoni mwa Novemba mwaka jana, jumla ya wagonjwa 560 wamefanyiwa vipimo katika mashine hiyo na ndani ya siku tatu ambazo wamefunga mashine mpya ya CT-Scan wameshawapima wagonjwa 26.
“Mashine ya CT-Scan ambayo imefungwa ina ubora mkubwa na ni ya pili kwa ukubwa Afrika Mashariki na kwa sasa tunategemea kufanya kazi kwa ubora zaidi kutokana na ukubwa iliyonayo na inaweza kufanya kazi kwa kasi tofauti na ile iliyokuwa ikitumika awali,” alisema.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Lawrence Mseru alisema awali hawakuwa wakifanya visingizio ili wasifanye kazi lakini ni hali halisi iliyokuwepo kuwa mashine iliyokuwepo awali ilikuwa na matatizo.
Alisema kufungwa kwa mashine mpya ambayo imeigharimu serikali Dola za Kimarekani milioni 1.7, kutawapa wao motisha ya kufanya kazi kwa kutumia kifaa cha kisasa na chenye kufanya kazi kwa haraka.
HABARILEO
Bohari Kuu ya Taifa ya Dawa (MSD) imesema kuwa deni ambalo wanaidai Serikali limezidi kuongezeka hadi kufikia Sh bilioni 117 Septemba 2015, hali ambayo imefanya kuzorotesha utendaji wa bohari hiyo.
Deni hilo linatokana na ugomboaji, uhifadhi na usambazaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kwa miradi Msonge ambayo ni kiasi cha Sh bilioni 104.1.
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema deni hilo linatokana na dawa na vifaa tiba zilizokopeshwa kwa hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya ambazo ni Sh bilioni 12.9.
Kutokana na kuongezeka kwa deni hilo, Waziri wa Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameiahidi MSD kuwa atafuatilia serikalini kuhakikisha deni hilo ambalo linadaiwa taasisi za Serikali linalipwa ili bohari hiyo iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Waziri huyo aliyasema hayo baada ya kuelezwa na Bwanakunu kuwa ukosefu wa fedha na deni la serikali ni changamoto kubwa inayoathiri utekelezaji mzuri wa majukumu ya MSD.
Ummy alifanya ziara ya kutembelea bohari hiyo kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi hiyo.
Mbali na hilo, Waziri huyo wa Afya alisema mbali na deni hilo, hata kiasi cha fedha kinachotengwa na serikali kwa ajili ya hospitali, vituo vya Afya na zahanati kununua dawa hakitoshelezi mahitaji, hivyo lazima suala hilo lifanyiwe kazi mapema, huku akisisitiza hata kiasi hicho kidogo kinachopatikana kitumike vizuri.
Katika hatua nyingine aliishauri Bohari ya Dawa kuanza utaratibu wa kununua dawa na vifaa tiba moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji, kuhakikisha dawa muhimu zinapatikana wakati wote na kuiagiza MSD itangaze kwenye vyombo vya habari dawa zote ambazo zinapelekwa vituoni, zahanati na kwenye hospitali.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa MSD, Laurean Bwanakunu alieleza kuwa tayari MSD imeshaanza kubandika kwenye mbao za matangazo za hospitali orodha ya dawa inazofikisha.
Waziri huyo ambaye alifuatana na Katibu Mkuu wa Wizara yake na watendaji wengine, alitembelea maghala ya kuhifadhia dawa ya Makao Makuu, jengo la ofisi linalojengwa pamoja na kuwa na mkutano na menejimenti ya MSD.
Pia aliipongeza MSD kwa hatua iliyofikia ya kuweka nembo ya GOT kwenye vidonge vyake ili kudhibiti upotevu wa dawa za serikali pamoja na kuanzisha maduka ya dawa Muhimbili, na mengine yanayotarajia kufunguliwa hivi karibuni mkoani Mbeya, Arusha na Mwanza.
Waziri Ummy Mwalimu alisema ajenda yake kuu ni upatikanaji wa dawa kwa wakati, kama Rais John Magufuli alivyoainisha, hivyo MSD itekeleze majukumu yake ipasavyo kwani mafanikio ya MSD ni mafanikio kwake pia.
HABARILEO
Zaidi ya wafanyabiashara 23 wa madini aina ya Tanzanite wamekamatwa na kutozwa faini kwa kufanya biashara bila ya kuwa na leseni katika Mji wa Mererani wilayani Simanjiro na kwenye mitaa ya Jiji la Arusha .
Katika msako huo uliofanywa na maofisa wa Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na Polisi madini yenye uzito wa gramu 2,188.53 yalikamatwa.
Akizungumza na gazeti hili jana Kaimu Ofisa madini Kanda ya Kaskazini,Erick Mpesa alisema kuwa madini hayo yaliyokamatwa yana thamani ya zaidi ya sh 46,926,690.
Mpesa alisema kuwa katika mitaa ya Jiji la Arusha hususani mitaa ya Goliondo,Ottu,St Thomas na maeneo mengine walikamatwa wafanyabiashara 15 wasiokuwa na leseni ya kufanya biashara hiyo .
Alisema katika Mji wa Mererani kwenye machimbo hayo ya madini ya Tanzanite walikamatwa wafanyabiashara wadogo wanane wakiyauza bila ya kuwa na leseni.
Ofisa madini huyo alisema katika msako huo ambao utakuwa wa kudumu jumla ya leseni 166 zilikatwa kwa malipo ya sh 250,000 kwa kila mfan yabiashara.
Mpesa alisema baada ya msako huo katika Jiji la Arusha pekee wafanyabiashara wadogo waliokata leseni ni 63 na katika Mji wa Mererani zilikatwa leseni 103.
Alisema msako huo utakuwa wa kudumu na kuwataka wafanyabiashara kufanya biashara na kulipa kodi kwani kufanya biashara ya madani bila ya kuwa na leseni na kukwepa kulipa kodi ni kosa kisheria kwani hatua za kisheria ni lazima zichukuliwe bila ya kusita.
Wakati huo huo mwandishi wetu kutoka Geita anaandika kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani ametoa siku 14 kwa mgodi wa dhahabu wa Buckreef kuanza uzal ishaji vinginevyo, wataandikiwa hati ya makosa na Ofisa Madini Mkazi katika mkoa wa Geita.
Naibu Waziri alitoa agizo hilo baada ya kufika katika mgodi huo uliopo katika kata ya Lwamgasa mkoani Geita na kukuta hakuna shughuli zozote za uzalishaji zinazoendelea.
“Najua kuwa hamjazalisha dhahabu mpaka sasa, lakini lazima mzalishe ili kulipa kodi na mrabaha, bila kufanya hivyo ndani ya siku 14 zijazo mtaandikiwa hati ya makosa kama sheria ya madini ya mwaka 2010 inavyoelekeza, mgodi huu mnaumiliki toka mwaka 2011, lazima muanze uzalishaji,” alisema Kalemani.
MTANZANIA
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza kushuka kwa bei ya mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa, ikilinganishwa na bei ya mwaka jana.
Taarifa iliyotolewa na EWURA jana na kusainiwa na Mkurugenzi Mkuu wake, Felix Ngamlagosi, ilieleza kuwa bei hiyo elekezi itaanza kutumika kuanzia leo Januari 6.
Ngamlagosi alitaja sababu mojawapo ya kupungua kwa bei za mafuta ni kushuka kwa bei za mafuta katika soko la dunia, pamoja na kushuka kwa gharama za usafarishaji na uletaji wa bidhaa hizo.
“Bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya aina hizo, zimeshuka ikilinganishwa na toleo lililopita la Desemba 2 mwaka jana ambapo kwa mwezi huu bei za rejareja kwa mafuta hayo zitapungua kama ifuatavyo Petroli Lita 79 itapungua kwa asilimia 4.01, Dizeli lita 76 punguzo ni asilimia 4.20 na Mafuta ya taa lita 66 itakuwa asilimia 3.73,” ilisema taarifa hiyo.
Katika taarifa hiyo, mamlaka hiyo imewataka wananchi kuzingatia mambo muhimu ambayo ni pamoja na kulinganisha bei hizo za mafuta na zile za toleo la Desemba mwaka jana ambazo zilikuwa Petroli Sh 79.19 kwa lita sawa na asilimia 4.23, Dizeli Sh 76.49 kwa lita sawa na asilimia 4.45 na Mafuta ya Taa Sh 65.86 kwa lita sawa na asilimia 3.97, Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya Mwaka 2008, bei za bidhaa hizo zitaendelea kupangwa na soko.
“EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta. Taarifa hizi zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa za mafuta.
NIPASHE
Wanasheria na watendaji wengine wa kada ya sheria wametakiwa kutenda haki katika kusimamia na kuendesha kesi kwa misingi ya kisheria.
Kinyume cha hapo, hatua kali zitachukuliwa dhidi yao ikiwamo kufukuzwa kazi, kwa yeyote atakayebainika kukiuka maadili ya utumishi wa umma ikiwamo kushiriki vitendo vya rushwa.
Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe alisema jana kuwa hali ya utoaji haki kwa jamii ni mbaya tangu enzi za uhai wa Mwalimu Julias Nyerere, na imeleta picha mbaya kwa watendaji wa umma kuendekeza rushwa na kuacha kutoa huduma stahiki kwa jamii.
Alisema serikali haitakubali kuendelea kufanya kazi na sampuli hiyo ya watendaji akimaanisha ‘wabovu’, badala yake wizara yake kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga, itawawajibisha mara moja.
“Sehemu mliyofika kiutendaji mnahitaji kutumbuliwa majipu yenu bila ganzi.
Hapa tunakwenda na kasi ya Rais, hivyo sheria itafuata msumeno na akitokea mmoja wenu anajihusisha na vitendo vya rushwa atawajibika. Hatuna muda wa kulea mambo ya kale hapa ni kazi tu,” alisema Dk. Mwakyembe.
Alisema rushwa itaendelea kuitesa serikali kutokana na kuwa kiungo kimojawapo kinachorudisha nyuma maendeleo ya wananchi. Alisema wakati serikali inafanya maboresho kwa wanasheria hao itafanya mchakato wa kuwaondoa wahusika wa rushwa kwanza, kwa sababu Watanzania wamechoka na wanahitaji kasi ya mabadiliko ionekane.
Pia alisema pamoja na kupokea changamoto zinazowakabili wanasheria ikiwamo ya kutishiwa kuuwawa, kupigwa, kukosa vitendea kazi, mazingira, rasilimali fedha, amewaahidi kuimarisha usalama wao.
Naye DPP Maganga alisema sekta hiyo imeanzisha kitengo kinachopambana na rushwa, ambapo kitadhibiti makosa dhidi ya binadamu, kesi za mtandao, ubinafsishaji wa mali za udanganyifu na makosa yanayofanyika mpakani mwa nchi.
Kwa mujibu wa Maganga, Septemba, mwaka jana, kesi nane zilizohusika na dawa za kulevya zilitolewa hukumu ambapo wahusika wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 hadi 30 jela na faini ya Sh. bilioni 20.
Sambamba na hilo, Oktoba, mwaka huo, waliteketeza kilo 260 za dawa za kulevya aina ya heroine na cocaine.
Unataka kutumiwa MSG za habari zote kubwa kutoka kwa Millard Ayo? ukiwa na line ya tiGO andika ‘AYO’ tuma kwenda 15510, msg utayotumiwa jibu OK ili uanze kupokea matukio yote kwa sms, pia ungana na Millard Ayo kwenye Twitter, FB, Instagram na YouTUBE wa kubonyeza hapa>>>INSTAGRAM TWITTER FB YOUTUBE