NIPASHE
Nyumba 17 zilizojengwa katika maeneo ya wazi zimebomolewa wilayani Kinondoni na halmashauri ya manispaa ya wilaya hiyo.
Operesheni ya kubomoa nyumba hizo iliyoanza jana itafanyika kwa siku tatu mfululizo na leo mahekalu yalijengwa katika maeneo ya wazi ya Mbezi Beach nayo yatabomolewa.
Mhandisi Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Baraka Mkuya, jana alisema kazi hiyo ilianza jana saa 9:00 alfajiri na kwamba maeneo yote yaliyobomolewa ni ya wazi na wahusika walishapewa notisi ya kuondoka siku nyingi lakini walikaidi kufanya hivyo.
Alisema kazi hiyo ni endelevu na leo itaendelea kwa kubomoa nyumba za waliojenga katika maeneo ya wazi ya Mbezi Beach, Tegeta Mivumoni na Kawe.
Ubomoaji huo unafanyika baada ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutoa agizo kwamba zibomolewe kwa sababu zimejengwa kinyume cha sheria.
Nyumba hizo zilibomolewa chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi na maofisa kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
Kwa mujibu wa msemaji wa wizara hiyo, Hassan Mabuye, kwa waandishi wa habari juzi, maeneo ya wazi, njia za miundombinu na huduma nyingine za umma, zipo kwa ajili ya matumizi ya umma, lakini yamekuwa yakivamiwa na kutumiwa vibaya na waendelezaji binafsi, hivyo kuukosesha umma manufaa yaliyokusudiwa.
Alisema maeneo hayo yapo kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995, tamko namba 6.6.1 na serikali itahakikisha kwamba maeneo yote ya mijini yaliyotengwa kwa shughuli za umma yanatumika kwa shughuli zilizokusudiwa na yanalindwa ili yasivamiwe.
Katika maeneo ya Mwenge, bomoabomoa hiyo ilianza majira ya saa 10:00 alfajiri kwa kubomolewa nyumba 15 pamoja na fremu za biashara.
Nyingine ilibomolewa maeneo ya Sinza Lion kwa kubomoa gereji bubu, pamoja na mtaa wa Bwawani, kata ya Mwananyamala nyumba moja.
Baadhi ya wananchi waliobomolewa nyumba zao walilalamikia hatua hiyo, kwa madai hawakupewa taarifa mapema na kwamba kitendo hicho kimewafanya wapoteze mali nyingi.
“Tulikuwa tunategemea kwamba manispaa ingetoa taarifa mapema ili tutoe mali zetu, lakini tumeshtukizwa, tumekuja kubomolewa usiku saa 10 alfajiri na awali waliwahi kuja kutaka kubomoa lakini tukaenda mahakamani na kesi ilitakiwa isomwe Desemba 2, mwaka huu,” alisema Kevin Francis, mpangaji katika fremu za biashara za Mwenge.
Mmiliki wa nyumba mojawapo na fremu mbili za biashara maeneo ya Mwenge, Elizabeth Mwakasendile, alisema hawajafanikiwa kutoa chochote na nyumba yake ilikuwa na wapangaji watatu na kila mpangaji alikuwa analipa pango Sh. 250,000 kwa mwezi kwa kila fremu na kwamba tayari alikuwa amepokea kodi ya miezi sita kwa kila mpangaji.
NIPASHE
Vigogo wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), wameanza kuhojiwa na Jeshi la Polisi Zanzibar baada ya kuvurugika kwa Uchaguzi Mkuu na kusababisha Mwenyekiti wa tume hiyo, Jecha Salim Jecha, kufuta matokeo ya uchaguzi huo Oktoba 28, mwaka huu.
Uchunguzi wa Nipashe visiwani humu umebaini kuwa viongozi waliohojiwa na Polisi ni ni Makamishna na Watendaji wa tume hiyo akiwamo Makamu Mwenyekiti, Jaji Abdulhakim Issa Ameir.
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar (DDCI), Salum Msangi, alithibitisha mjini hapa Mjini jana kuwa Makamishina wa Zec na Watendaji, wameanza kuhojiwa na maofisa wa upelelezi kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Zanzibar Ziwani Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Alisema hadi sasa uchunguzi umefikia hatua kubwa na baada ya kukamilika, majalada ya uchunguzi yatapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar (DPP), Ibrahim Mzee Ibrahim, kabla ya wahusika kufikishwa mahakamani.
“Tunawahoji Makamishna na Watendaji wa Tume, Makamu Mwenyekiti yeye tayari tumemhoji, bado Mwenyekiti na maofisa wengine,” alifafanua DDCI Msangi.
Alisema Polisi waliingia kazini baada ya kuripotiwa kuwa uchaguzi umevurugwa na kazi inayofanyika ni kukusanya ushahidi na vielelezo kabla ya wahusika kufunguliwa mashitaka kwa kuhujumu Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.
Alisema uchunguzi huo umegawanyika sehemu tatu na kuwahusisha Tume, waathirika na wananchi kutoka sehemu mbalimbali katika Visiwa vya Unguja na Pemba.
Aidha, alisema kuna mambo mazito yameanza kuonekana tangu kuanza kufanyika kwa uchunguzi, lakini alisema ni mapema kueleza uchunguzi huo utachukukua muda gani kukamilika.
“Wahusika watafikishwa mahakamni baada ya majalada ya uchunguzi kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar kabla ya kufikishwa mahakamani,” Msangi.
Hata hivyo, Naibu Mkurugenzi huyo alisema hali ya Zanzibar ni shwari na wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida tangu Zec ilipofuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 28, mwaka huu.
Akitangaza kufuta uchaguzi huo, Mwenyekiti wa Zec, Jecha alisema kuna sababu tisa zimemfanya kuchukua hatua hiyo.
Alizitaja kuwa ni pamoja na vituo vya wapigakura na idadi ya kura katika visanduku zilikuwa nyingi kuliko idadi ya watu waliosajiliwa katika daftari la wapigakura katika vituo vya uchaguzi.
NIPASHE
Serikali ya Zanzibar imeondoa gharama za uchunguzi kwa wagonjwa wanaohitaji vipimo vya CT-Scan, X-ray na Utra-Sound katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, Zanzibar.
Kabla ya uamuzi huo, wagonjwa waliopatiwa huduma za vipimo hivyo walikuwa wakilipia kati ya Sh. 100,000 na 150,000 kwa mashine ya CT-Scan na Sh. 100,000 kwa Utra-Sound wakati huduma za X-ray ni Sh. 30,000.
Katibu wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Hassan Makame, alisema huduma bure za afya kwa vipimo, ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein.
Alisema uongozi wa hospitali hiyo ulipokea agizo la kufutwa kwa gharama za vipimo kwa wagonjwa Oktoba mosi, mwaka huu.
Alisema chini ya maagizo hayo, wagonjwa wote wametakiwa kufanyiwa uchunguzi wa vipimo bure ili kuwaondolea usumbufu wananchi wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharamza za vipimo.
Alisema tangu agizo hilo lianze kutekelezwa idadi ya wagonjwa wanaotaka kutumia vipimo hivyo, imekuwa kubwa ikilinganishwa na awali.
“Uwezo wa mashine ni kuhudumia wagonjwa 20 kwa siku, lakini sasa wagonjwa wamekuwa wengi na wengine kulazimika kupangiwa siku nyingine,” Makame.
Kwa upande wao, baadhi ya wagonjwa katika hospitali hiyo walisema wamefurahishwa na uamuzi huo wa kuondoa gharama za vipimo vya uchunguzi kwa wagonjwa.
Walisema kuwa wananchi wengi ni maskini na walikuwa wakishindwa kumudu gharama za kupata tiba kwa wakati mwafaka na baadhi yao kupoteza maisha yao.
Asha Said, alisema alikwama kupata vipimo kwa muda mrefu kutokana na kushindwa kumudu gharama zake.
Said alisema hali hiyo ilimfanya kukaa muda bila kufanyiwa uchunguzi, lakini sasa amefanyiwa uchunguzi na kuendelea na tiba.
“Naishukuru sana serikali kwa uamuzi wake huu wa kutoa huduma za uchunguzi bure,” alisema mgonjwa mwingine, Asha Saaten.
Hata hivyo, Halima Muhsin, alisema kuna umuhimu kwa serikali kuimarisha huduma za matibabu ambazo hazipatikani katika hospitali zake.
HABARILEO
Watoto wawili, akiwemo mwanafunzi wa shule ya msingi Mkwese wilayani Manyoni mkoani Singida, wamekufa baada ya kuangukiwa na nyumba ya tembe kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kijijini hapo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa Singida, Thobias Sedoyeka aliwataja waliokufa kwenye ajali hiyo kuwa ni Jumapili Mayunga (12) na Masegese Mayunga wakazi wa kitongoji cha Mningaa katika kijiji cha Mkwese wilayani Manyoni.
Sedoyeka alisema mjini hapa jana kuwa ajali hiyo ilitokea juzi baada ya mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali kunyesha kijijini hapo, hivyo kusababisha nyumba walimokuwa wamelala watoto hao kuanguka na kuwafukia.
Kwa mujibu wa Kamanda Sedoyeka, wazazi wa watoto hao walikuwa wamelala nyumba nyingine jirani na kwamba waligundua tukio hilo mara baada ya kusikia kishindo kwenye nyumba walimokuwa wamelala watoto hao na hivyo kwenda kuangalia kulikoni.
“Mara baada ya kuona watoto wao wamefunikwa na udongo wa nyumba hiyo, walipiga kelele za kuomba msaada kwa majirani na walipokuja juhudi za kuwafukua zilianza lakini kwa bahati mbaya waliwakuta tayari wameshapoteza maisha,” Kamanda Sedoyeka.
Kutokana na tukio hilo, Sedoyeka ametoa mwito kwa wakazi wa mkoa wa Singida kuchukua hadhari mbalimbali kwenye maeneo yao wakati huu wa kipindi cha masika ambapo mvua kubwa zinaendelea kunyesha na aghalabu, huleta madhara.
HABARILEO
Hukumu ya kesi inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Shekhe Ponda Issa Ponda, imeshindwa kutolewa jana kutokana na Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Mkoa wa Morogoro, Mary Moyo kuwa mkoani Dodoma kwa shughuli za kikazi.
Hakimu Erick Rwehumbiza aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 30, mwaka huu.
Alisema Hakimu Moyo ambaye ndiye anaisikiliza hadi hatua ya kuandika hukumu, kuanzia Novemba 16, mwaka huu yuko mkoani Dodoma kwa ajili ya kuhudhuria mafunzo maalumu ya kushughulikia kesi za uchaguzi na anatarajiwa kurudi kutoa hukumu hiyo Novemba 30.
Aliamuru Shehe Ponda aliyeletwa mahakamani hapo kwa ajili ya hukumu arudishwe rumande.
Upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Juma Nassoro na upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa serikali mwandamizi Bernard Kongola, ulieleza kuwa wameshakamilisha hatua zote kesi na kwamba wanachosubiri ni hukumu hiyo.
Nassoro akiwa nje ya mahakama aliwaambia ndugu, jamaa na wafuasi wa Ponda waendelee kuwa watulivu na wavumilivu kwa vile suala lililobakia ni la Hakimu kutoa hukumu Novemba 30 mwaka huu.
Alisema, wao wakiwa mawakili wa utetezi kesi hiyo wamemaliza sehemu yao na iliyobakia ni kwa hakimu kuamua siku ya kutoa hukumu na kwamba wote wanasubiri hukumu hiyo.
Baada ya kuahirishwa kwa hukumu hiyo, wafuasi hao waliamua kutawanyika kutoka katika eneo la mahakama hiyo na kuelekea msikiti wa Ijumaa. Shehe Ponda alifunguliwa kesi namba 128/2013 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani hapa.
Awali alikuwa akikabiliwa na mashtaka matatu anayodaiwa kuyatenda Agosti 10, mwaka 2013 katika eneo la Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro.
Alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Agosti 19 mwaka 2013 kwa mashitaka hayo matatu na baadaye alifutiwa shitaka moja na kubakia mawili ambayo ni kutoa maneno yenye kuumiza imani za dini na kushawishi watu kutenda kosa.
MWANANCHI
Hakuna msiba usiokuwa na mwenziwe. Msiba wa kwanza uliowapata wachimbaji watano wa madini katika machimbo ya Nyangalata wilayani Kahama, Shinyanga ulikuwa wa kufukiwa na kifusi na kuishi shimoni kwa shida kwa siku 41, lakini msiba wa pili baada ya kuokolewa ni kukuta mali walizokuwa wanamiliki zimerithiwa. Waliokumbwa na ‘msiba’ wa pili ni Onyiwa Morris na Chacha Wambura.
Mali za Joseph Bulule zimenusurika lakini hakuna taarifa kuhusu mali za Amos Mhangwa na Msafiri Gerald. Taarifa iliyotolewa jana na mganga mfawidhi wa hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kahama, Joseph Ngowi zimesema waathirika hao wote wako katika hali nzuri.
“Waathirika wote watano; Joseph Bulule, Chacha Wambura, Amos Mhangwa, Onyiwa Moris na Msafiri Gerald hawana magonjwa yoyote, wanahitaji lishe ili kurudisha nguvu zilizokuwa zimepotea baada ya siku saba tutawapa ruhusa ya kurudi majumbani kwao,” alisema Ngowi.
“Kati ya hao, Onyiwa bado hajaanza kusimama lakini wengine wote wanasimama na wanaweza kutembea wenyewe bila kuwa na msaada wowote.” Mali za waathirika Akizungumza na Mwananchi jana mjini Kahama, Thobias Oluoti ambaye ni mdogo wake Onyiwa alisema baada ya tukio la kufukiwa kwa kifusi kaka yake na wenzake watano walikwenda nyumbani kwao Tarime na kuweka msiba.
Oluoti alisema kilichosababisha watangaze msiba ni kauli ya aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga kwamba haukuwapo uwezekano wa kuwaokoa wakiwa hai kwa vile hakukuwa na vifaa.
“Baada ya kauli ile tulichukua nguo zake zote tukaenda kijijini ambapo tuliweka matanga kwa siku saba, na baada ya hapo, kwa mujibu wa mila na desturi zatu, tulianua matanga na kugawana mali za “marehemu” zikiwamo ng’ombe, mashamba na nguo,” alisema Oluoti.
Hata hivyo, tukio la kufukuliwa kwa kaka yake akiwa hai liliwashtua. “Nilipigiwa simu na mdogo wangu, mimi nikadhani huenda aliugua malaria au aliingiwa na mtandao wa kishetani wa freemanson.
Tuliingiwa na hofu, nikamzuia mdogo wangu asiende mahali popote hadi nimpe maelekezo mengine,” alisema. Mbali ya kuingiwa na hofu na kumzuia mdogo wake asiende sehemu yoyote, alimtaka afuatilie kwa makini simu iliyopigwa na mtu mmoja aliyemtaja kwa jina moja la Tingwa na baada ya kupata uhakika ndipo alipopigiwa tena simu na mdogo wake.
“Aliponipigia simu aliniambia kwamba kaka Onyiwa ameokolewa akiwa hai na alinitaka niamini hivyo, ndipo nilipofunga safari kuja kwanza mimi mwenyewe kuthibitisha katika hospitali kujionea,” alisimulia.
Oluoti alisema juhudi za kumwona Onyiwa hospitalini zilitatizika kwani alizuiwa na shemeji yake kwa madai hatakiwi kumwona mpaka atengenezewe masuala ya imani ya matambiko ya kwao.
Kutokana na shauku aliyokuwa nayo kumwona kaka yake na ukweli masuala ya mila na matambiko yamepitwa na wakati, Oluoti aligoma kwa madai wao ni Wakristo waumini wa dhehebu la Sabato hivyo aliingia wodini akamwona kaka yake akiwa amedhoofika ambapo alianguka kilio.
Bhoke Mwita ambaye ni mke wa Wambura alisema baada ya Serikali kutangaza kwamba haukuwapo uwezekano wa kuwatoa watu hao wakiwa hai waliamua kuhamisha makazi kutoka Nyangalata hadi Kahama ambako waliweka matanga.
Baada ya hapo msiba ulihamia Tarime huku ndugu zake wakichukua nguo za mume wake na kwenda nazo huko ambako baada ya siku saba walianua matanga na kugawana mali zake. Marco Bulule ambaye ni kaka wa Joseph Bulule alisema mali zake zilinusurika kurithiwa baada ya televisheni moja kutangaza kuwa watu waliofukiwa na vifusi bado walikuwa hai ndani ya mashimo na walikuwa wanawasiliana na wenzao wa nje kwa njia ya simu. Hiyo ilikuwa siku ya saba tangu wafunikwe na kifusi.
Bulule alisema ndugu wote waliokuwa kwenye msiba Bunda walisikia taarifa hiyo na ndipo kwaya ya kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) iliombwa kubadili nyimbo badala ya kuimba za kuomboleza ikaanza kuimba za kuwaomba Mungu awanusuru. Taarifa hiyo iliwafanya waahirishe kufanya matanga na yeye alikaa hapo kwa siku 30 mpaka Novemba 5 alipoondoka kwenda nyumbani kwake Katoro, Geita.
Bulule anasema siku ya tukio la kuokolewa kwa watu hao alipigiwa simu ambayo hakuiamini kwa kuwa zilipita siku nyingi watu hao wakiwa ndani ya mashimo.
Katika hatua nyingine Bulule alisema ingawa mdogo wake amenusurika kifo, kaka zake wawili walishakufa huko Tarime kutokana na tukio kama hilo la kufukiwa na kifusi.
“Maisha yetu sisi ni uchimbaji madini,” alifafanua. Wachimbaji hao watano ni kati ya sita waliofukiwa na kifusi Oktoba 5 na wameishi chini ya ardhi kwa siku 41 hadi walipookolewa Novemba 15 na kulazwa Hospitali ya Mji Kahama. Mchimbaji madini wa sita alifariki siku 15 kabla ya kuokolewa.
MWANANCHI
Vyama vinavyounda Ukawa wamesema wamwandikia Spika wa Bunge, Job Ndugai barua kutaka kujua uhalali wa Rais John Magufuli kuhutubia Bunge bila matokeo Rais wa Zanzibar kujulikana.
Katika mkutano wao na waandishi leo, wamesema kuwa hawatakubali Katiba ivunjwe kwa kumruhusu Dk Shein kuingia bungeni wakati muda wake wa kushika madaraka ulishapita.
Katika hatua nyingine, Umoja huo umesema wabunge wa kambi ya upinzani bungeni wamekubaliana kuchanga kila mmoja Sh 300,000 kwa ajili ya kuchangia familia ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Geita, Alphonce Mawazo.
Uamuzi huo umetangazwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe kwenye mkutano wa waandishi wa habari bungeni baada ya kikao cha wabunge wote wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Pia wamekubaliana Jumamosi ya Novemba 21, wataenda wabunge wote kuungana na viongozi wengine wa kitaifa kumzika marehemu Mawazo.
MWANANCHI
Spika wa Bunge, Job Ndugai anatajwa kuwa na nafasi kubwa ya kumudu changamoto zinazolikabili Bunge la Kumi na Moja kutokana na uzoefu alioupata alipokuwa Naibu Spika miaka mitano iliyopita.
Wakizungumza jana, wachambuzi wa masuala ya siasa nchini wamemwelezea Ndugai kuwa mgombea aliyestahili ushindi wa nafasi hiyo.
“Ni wazi kuwa Bunge lijalo ni gumu, lakini Ndugai si mgeni. Litakuwa Bunge la kibabe lakini Ndugai naye ni mbabe… anazo sifa za ziada na uzoefu wa kuendesha Bunge la wabunge matata, naamini atamudu vyema changamoto atakazokutana nazo,” anasema Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam UDSM), Kitila Mkumbo.
Hata hivyo, Mhadhiri Mwandamizi wa UDSM, Dk Alexander Makulilo alisema ili amudu changamoto zinazolikabili Bunge la Kumi na Moja, Ndugai anatakiwa kusimama imara na kuhakikisha anaendesha Bunge bila upendeleo wala kujali itikadi za vyama vya siasa.
Dk Makulilo alisema Bunge lijalo linakabiliwa na changamoto nyingi kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wabunge wapya na vijana na kuwa ili kuendana na kasi ya Bunge hilo, Ndugai anapaswa kuliendesha kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na kuweka kando masilahi ya chama chake.
“Ndugai si mgeni wa haya mambo, amekuwa naibu spika kwa muda mrefu, anao uzoefu mkubwa tu, hatazamiwi kuwa ni mpya katika nafasi hiyo… kazi yake itakuwa nyepesi endapo atatimiza wajibu wake, aendeshe Bunge bila upendeleo, asichukue upande. Bunge lisiwe na itikadi za vyama,” alisema Dk Makulilo.
Alisema mbali na spika, wabunge wanapaswa kutambua kuwa wao ni wawakilishi wa wananchi hivyo wajibu wao ni kuwatetea na kuwasemea na kuachana na itikadi za kisiasa.
Alisema endapo spika au wabunge watatoka kwenye mstari wa kusimamia masilahi ya Taifa na kukumbatia ya vyama vyao, wataifanya kazi yao ya uwakilishi wa wananchi kuwa ngumu na watashindwa kuiwajibisha Serikali pale inapobidi.
“Wabunge wakipatiwa mafunzo na wote kwa ujumla wao wakizijua na kuziheshimu kazi zao, kamwe spika hawezi kupata na shida kubwa katika kuliongoza Bunge,” alisema,
Alisema wabunge na spika wanayo nafasi ya kurejesha heshima iliyopotea ndani ya chombo hicho muhimu kwa kila mmoja kuzingatia nafasi aliyopewa ni ya uwakilishi wa wananchi wake hivyo anapaswa kuitenda haki.
Mkurugenzi wa Fordia, Buberwa Kaiza alisema Watanzania wasitegemee kitu kipya katika uongozi wa Ndugai bungeni kwa maelezo kuwa atafanya kazi kwa masilahi ya chama tawala ambacho ndicho kilichompa nafasi hiyo.
Alisema Ndugai hajaanza uongozi wa bungeni mwaka huu akisema alikuwa mwenyekiti wa kamati kwenye Bunge la Tisa, naibu spika Bunge 10 na sasa spika hivyo ni mzoefu na anayejua wajibu uliopo mbele yake.
Unataka kutumiwa MSG za habari zote kubwa kutoka kwa Millard Ayo? ukiwa na line ya tiGO andika ‘AYO’ tuma kwenda 15510, msg utayotumiwa jibu OK ili uanze kupokeamatukio yote kwa sms, pia ungana na Millard Ayokwenye Twitter, FB, Instagram naYouTUBE wa kubonyeza hapa>>>INSTAGRAM TWITTER FB YOUTUBE.