MTANZANIA
Bomoabomoa ya nyumba na makazi zilizojengwa kinyume cha sheria iliendelea jana katika Wilaya ya Kinondoni, ambapo Kanisa la Anglikana pamoja na Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Mivumoni zimekumbwa na bomoabomoa hiyo.
Shughuli hiyo ya ubomoaji ilianza jana saa 12 asubuhi katika eneo la Mbezi Jogoo, ambapo nyumba 25, makanisa mawili, fremu mbili za biashara na sehemu ya kuoshea magari zilibomolewa.
Mbali na kanisa la Aglikana, kanisa jingine ni la Tanzania Assemblies of God (TAG) lililopo Bunju B, nyumba ya mwanajeshi ambaye amerejea kutoka kulinda amani Darfur Sudan nayo imebomolewa na kusababisha mke wa mwanajeshi huyo kuzirai.
Bomoabomoa ilifanyika karibu na kiwanda cha Interchick ambapo nyumba moja na eneo la kuoshea magari vilibomolewa.
Aidha bomoabomoa iliendelea eneo la Basihaya Bunju ambapo nyumba 19 zilibomolewa pamoja na fremu mbili za biashara ya mbao inayomilikiwa na Ally Khamis.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Basihaya, Kata ya Bunju, Malinus Ndule alisema nyumba hizo tayari wananchi wake walilipwa fidia ikiwemo viwanja katika eneo la Mabwepande.
Waumini wa Kanisa la Tanzania Assemmbles of God (TAG) walifika eneo la tukio wakiwa na Biblia wakiomba na kuangua kilio huku wakisema Mungu ana mpango nao.
Akizungumzia tathimini ya ubomoaji huo, Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni, Baraka Mkuya alisema shughuli hiyo inaendelea vyema na ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa kuwafichua vigogo waliojenga kinyume na sheria.
MTANZANIA
Wazanzibar wanaoishi nchini Uingereza jana wamefanya maandamano kutaka nchi hiyo iingilie kati na kutoa shindikizo kwa Serikali ya Tanzania ili kuhakikisha mshindi wa uchaguzi wa Rais wa Zanzibar anatangazwa na kuapishwa.
Hatua ya maandamano hayo yamekuja kutokana na hatua ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi huo huku akitoa sababu tisa ikiwemo uchaguzi kutoka huru na haki.
Katika maandamano hayo hayo yaliyofanyika nchini humo na kukusanya sehemu ya Wazanzibari wanaoishi nchini Uingereza, walifanya maandamano hayo ambayo yaliishia katika Mtaa wa Downing zilipo ofisi za Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron na kukabidhi barua yao.
“Tumefanya maandamano ambayo yameratibiwa na viongozi wa Zanzibar Welfare Association (ZAWA) na tumefikisha ujumbe wetu, ambapo tumekwenda hadi katika ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron katika namba 10 Downing Street na kukabidhi barua yatu,” alisema mmoja wa viongozi wa ZAWA
Tangu kufutwa kwa matokeo hayo ya uchaguzi mataifa kadhaa ya nje yamekuwa yakiingilia hatua hiyo ikiwemo Serikali ya Marekani na kutaka tamko hilo liondolewe.
Serikali ya Marekani imesema imeshtushwa sana na tamko la Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, kufuta matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar.
Katika tamko lililotolewa na ubalozi wa Marekani nchini, umesema hatua hii inasitisha mchakato wa uchaguzi uliofanyika vizuri na kwa amani, kama ilivyoelezwa na waangalizi wa uchaguzi kutoka Ubalozi wa Marekani, Jumuiya ya Ulaya, Jumuiya ya Madola na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika pamoja na kusitisha zoezi la majumuisho ya kura lililokuwa linakaribia kukamilika.
“Tunatoa wito wa kuondolewa kwa tamko hilo na kuzisihi pande zote kudhamiria kwa dhati kuukamilisha mchakato huu wa kidemokrasia kwa uwazi na kwa amani. Watu wa Zanzibar wanastahili jambo hilo,” ilieleza taarifa hiyo iliyotumwa na ubalozi wa Marekani nchini kwa vyombo vya habari.
Awali Mwenyekiti wa ZEC, Jecha, alisema kuwa wameamua kufuta uchaguzi huo baada ya kubaini kasoro tisa, ikiwamo kuchezewa kwa matokeo katika Kisiwa cha Pemba.
MWANANCHI
Wakati Rais John Magufuli akitarajiwa kuzindua na kulihutubia Bunge leo, ametahadharishwa kutoambatana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kwa maelezo kuwa si rais halali wa Zanzibar kikatiba.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Profesa Ibrahim Lipumba alisema Zanzibar haina Rais, hivyo kiongozi huyo kushiriki Bunge kwa nafasi hiyo ni kuvunja Katiba ya nchi.
Profesa Lipumba aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha CUF, ameungana na msimamo wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) walioutoa mjini Dodoma juzi wakidai kuwa Dk Shein hapaswi kuingia kwenye ukumbi wa Bunge wakati Rais Magufuli atakapohutubia.
Alishauri endapo kuna ulazima wa Rais wa Zanzibar kuhudhuria, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) itangaze matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa urais wa Zanzibar na rais aliyeshinda aapishwe.
Lipumba pia amemtaka Rais Magufuli kutumia nafasi yake ya Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama ya Tanzania kuishauri ZEC kurejea matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 na kumtangaza mshindi.
“Wazanzibari hawawezi kuruhusu uchaguzi kurudiwa, ” alisema Lipumba. Alisema anashangazwa na hatua ya Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete
MWANANCHI
Mbunge wa Ruangwa, Kassim Majaliwa amekuwa Waziri Mkuu wa Kumi na Moja baada ya Bunge kuidhinisha pendekezo la Rais John Magufuli jana, lakini akasema alipata taarifa za uteuzi wake kupitia runinga wakati akihamisha vifaa kutoka nyumba za Serikali.
Pamoja na ubashiri kumtaja kuwa mmoja wa watu waliokuwa wanapewa nafasi ya kuteuliwa kuwa mtendaji mkuu wa Serikali, Majaliwa, ambaye alikuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), alisema hakuwa na taarifa kuwa ameteuliwa.
“Kama binadamu nilipata mshtuko na kujikuta nikitoa machozi,” alisema Majaliwa nje ya ukumbi wa Bunge. “Sijui Rais aliona nini kwangu, alitumia vigezo gani kuona mimi nafaa.
Lakini namshukuru kwa kuona nafaa na kuniamini kunipa nafasi hii kubwa. “Sikuwa na taarifa yoyote. Juzi niliapishwa na kama ilivyo kawaida familia yangu, ndugu, jamaa na wapigakura wangu walikuja kushuhudia tukio hili muhimu.
Baada ya kuapishwa wengine walishaanza kuondoka tangu juzi na wengine walikuwa waondoke leo (jana) na taratibu zote za tiketi nilishakamilisha. “Kama ningekuwa na taarifa nisingeingia gharama zote hizo kwa kuwa wengine wameshaondoka.”
Uteuzi wa Waziri Mkuu ulitawaliwa na usiri mkubwa na hilo lilijionyesha jana wakati bahasha iliyokuwa na barua ya jina lake iliwasilishwa bungeni na mpambe wa Rais. Barua hiyo ilikuwa ndani ya bahasha tatu na iliandikwa kwa mkono wa Dk Magufuli, kwa mujibu wa Spika Job Ndugai.
Wakati Ndugai akifungua bahasha hizo, wabunge walionekana kuwa na tashwishi na kuangua kicheko baada ya katibu wa Bunge kufungua bahasha ya kwanza na kukuta nyingine ndani hadi ilipomalizika ya tatu.
“Na barua yenyewe imeandikwa kwa mkono wa Rais,” alisema Ndugai akimaanisha kuwa jukumu la kuandika barua hiyo hakupewa msaidizi wake huku wabunge wakishangilia. Akisoma barua hiyo, Ndugai alisita mara mbili kutaja jina na kusababisha ukumbi wa Bunge kulipuka kwa kelele kabla ya kutaja Majaliwa na wabunge kupokea kwa makofi na vifijo.
Wakati hayo yakitokea, Majaliwa hakuwapo ndani ya ukumbi wa Bunge. “Nilikuwa katika harakati za kuhamisha vyombo vyangu kutoka katika nyumba ya Serikali kwa kuwa nilipata nyingine ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) baada ya kipindi cha uwaziri kwisha,” alisema nje ya ukumbi wa Bunge.
Alisema wakati wanatoa vyombo katika nyumba hiyo, mmoja wa vijana waliokuwapo aliwasha runinga kwa ajili ya kuangalia Bunge na yeye akasogea karibu, ndipo akamuona Spika akitaja jina lake kuwa Waziri Mkuu.
Majaliwa, ambaye kitaaluma ni mwalimu, alithibitishwa na Bunge kwa kupata kura 258 ambazo ni sawa na asilimia 73.5 ya kura zote 351 zilizopigwa, huku kura 91 zikimkataa.
“Namshukuru Rais kuniamini na kulileta jina langu bungeni. Nawahakikishia kwamba nitawapa ushirikiano bila kujali vyama vyetu na nitafanya kazi pamoja kuwaletea wananchi maendeleo,” alisema Waziri Mkuu. Alisema kwa jukumu ambalo amepewa atashirikiana na wabunge wote ili waweze kuwasaidia wananchi waliowatuma bungeni kuwaletea maendeleo.
Alisema anaendelea kuwa Majaliwa yuleyule na ataendelea kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari kwa kuwa amekuwa akishirikiana nao wakati akiwa naibu waziri. Lakini akatahadharisha kuwa anavyoonekana kuwa ni mtu mpole na mnyenyekevu ni tofauti na alivyo kiutendaji.
“Unaweza kuwa mpole, lakini makini katika utendaji wa kazi. Upole ni tabia ambayo inaweza kumfanya mtu kuelewa jambo na kutekeleza kwa ufasaha,” alisema katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Azam Tv baadaye jana. “Lazima kama kiongozi upokee jambo, ulisikilize uchuje upate majibu na lazima usimamie ukweli wa jambo lenyewe.
Kwa hiyo suala la upole ni jambo moja na suala la usimamizi wa kazi ni jambo jingine.” Wabunge wachache waliopata nafasi ya kuchangia hoja ya kuliomba Bunge liidhinishe pendekezo la Rais la kumteua Majaliwa kuwa Waziri Mkuu ambalo liliwasilishwa na Mwanasheria Mkuu, George Masaju baada ya Bunge kusitisha shughuli zake kwa dakika 45, walimuelezea mbunge huyo wa Ruangwa kuwa ni mtu msikivu, mchapakazi, mpole na mwenye uwezo wa kujibu hoja za wizara yake.
Mbunge wa Isimani (CCM), William Lukuvi, ambaye pia alikuwa akitajwa kuwa angeweza kupewa nafasi hiyo, alikuwa wa kwanza kuchangia hoja akieleza kuwa Rais amependekeza mtu mwenye sifa. “Kwa wanaomfahamu, sisi tunamfahamu tumefanya naye kazi. Mimi nimefanya naye kazi nikiwa kwenye mwamvuli wa Waziri Mkuu. Lakini pia wabunge wengi wa zamani tunamjua.
Hawezi mtu hata mmoja kusema amegombana na Mheshimiwa Majaliwa,” alisema Lukuvi, ambaye alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri MkuuSera, Uratibu na Bunge kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Ardhi.
“Lakini na Watanzania kwa nafasi mbalimbali za kusikiliza mijadala au hoja mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa na Mheshimiwa Majaliwa hapa bungeni au waliopata fursa ya kumuona akitembelea miradi yake huko mikoani wanamjua Mheshimiwa Majaliwa kwamba ni mtu muadilifu, kwanza muadilifu sana.
Sifa kama hizo zilitolewa na mbunge wa Nzega Vijijini (CCM), Dk Hamis Kigwangallah aliyesema kuwa Majaliwa ni mwadilifu anayesikia na anayefaa katika nafasi hiyo. Mbunge wa mwisho kuchangia hoja hiyo kabla ya kupiga kura alikuwa Kangi Ligola wa Mwibara ambaye alimsifu Majaliwa kuwa ni jembe la pili baada ya Magufuli.
Lakini Ligola nusura avuruge halki ya hewa bungeni wakati alipodai kuwa mbunge wa Ubungo kwa tiketi ya Chadema, Saed Kubenea na wa Vunjo (NCCRMageuzi), James Mbatia walishangilia kwa kupiga makofi wakati Spika alipotangaza jina la Majaliwa.
Kubenea alikuwa wa kwanza kutoa taarifa kuwa Ligola alitumia jina lake vibaya na kumtaka afute kauli yake, lakini Ndugai alisema apuuze hayo na kumpa nafasi ya kuchangia hoja, akionekana kutaka kuendelea kusisitiza aombwe radhi, Spika alizima kipaza sauti chake na kumruhusu mbunge mwingiune Andrew Chenge achangie, .
NIPASHE
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imesema aliyekuwa Mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), David Mattaka na wenzake, wana kesi ya kujibu.
Mattaka na wenzake wanakabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya madaraka kwa kutangaza zabuni ya ununuzi wa magari 26 yaliyochakaa na kuisababishia Serikali hasara ya Dola 143,442.75 za Marekani.
Aidha, mahakama hiyo imesema kesi hiyo itaanza kusikiliza ushahidi wa upande wa utetezi Desemba 10 na 11, mwaka huu.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Emmilius Mchauru, baada ya kusikiliza mashahidi 13 wa upande wa Jamhuri dhidi ya washtakiwa.
Alisema washtakiwa hao wana haki ya kujitetea kupitia njia tatu.
“Washtakiwa mnaweza kuamua kujitetea kwa njia ya kiapo, bila kiapo ama kukaa kimya kuiachia mahakama kutoa hukumu,” alisema Hakimu Mchauru wakati akisoma uamuzi huo.
Hata hivyo, washtakiwa hao kwa nyakati tofauti walidai watajitetea kwa njia ya kiapo.
Upande wa utetezi ukiongozwa na Peter Swai na Alex Mgongolwa, ulidai kuwa katika ushahidi wao wa utetezi, wanatarajia kuita mashahidi saba wakiwamo washtakiwa.
Mbali na Mattaka, washtakiwa wengine ni Kaimu Ofisa Mkuu wa Kitengo cha Fedha, Elisaph Ikomba na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Ndani, William Haji, wa shirika hilo.
Katika kesi hiyo ya matumizi mabaya ya madaraka, Mattaka na wenzake Elisaph Ikomba na William Haji wanadaiwa pamoja na mambo mengine, wakiwa waajiriwa wa ATCL na wenzao ambao hawajulikani kati ya Machi na Julai, mwaka 2007, walikula njama ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya Dola 143,442.75 za Marekani.
NIPASHE
Kocha wa Timu ya Taifa, Taifa Stars Boniface Mkwasa ametupilia mbali hoja za kumtaka kujiuzulu nafasi hiyo kufuatia kipigo cha aibu ilichokipata Tanzania cha kufungwa mabao 7-0 na Algeria katika mechi ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Russia.
Badala yake, Mkwasa amewaomba radhi Watanzania kwa kipigo hicho kinachofanya jumla ya mabao yote kuwa 9-2 baada ya sare ya 2-2 katika mchezo wa kwanza uliopigwa Dar es Salaam.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkwasa alisema kwa miaka 25 aliyofundisha soka, hajawahi kuongoza timu na kufungwa idadi hiyo kubwa ya mabao.
“Matokeo haya yamenihuzunisha kupita maelezo,” alisema Mkwasa.
Alisema wachezaji wake walipambana vya kutosha kiasi cha kufika hatua ya mwisho kabisa ya uwezo wao dhidi ya timu bora Afrika.
“Kama ambavyo Mtanzania yeyote ameumizwa na matokeo haya, ndivyo mimi pia. Naomba radhi kwa matokeo haya.
“Hata kama tungefungwa, lakini siyo kwa idadi ile ya mabao, kweli hakuna anayefurahi matokeo kama haya,’ alisema Mkwasa.
Alisema kufungwa kwa Stars kunatokana na ubora wa timu waliyocheza nayo. “Wachezaji wao walikuwa bora kila idara kulinganisha na wachezaji wetu.
“Hatuna wachezaji wenye kariba kama ya wapinzani wetu…wenye usumbufu na wanaojua kukaba. Hili ni tatizo kwenye timu yetu.
“Wenzetu wana wachezaji wengi wazoefu na mechi za kimataifa na wote wanacheza soka la kulipwa nje ya nchi,” alisema.
“Pamoja na matokeo haya mabaya, sina mpango wa kujiuzulu kama watu wanavyoshauri. Nitaendelea kuifundisha Stars na nawaomba wananchi waiunge mkono timu.”
Stars sasa italazimika kusubiri harakati zingine za kucheza Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Qatar.
PAPO KWA PAPO zipate habari zote zinazonifikia za siasa muziki, michezo, maisha, Breaking news na nyingine kwa kujiunga hapa na mimi >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos