Siku moja baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe kuugua ghafla akiwa kwenye maandaamano na kuwahishwa hospitali ya Taifa Muhimbili, imebainika kuwa hali hiyo imesababishwa na kufanya kazi kwa muda mrefu bila kupumzika.
Daktari bingwa wa Moyo Kitengo alicholazwa kiongozi huyo, Dk Tulizo Sanga alieleza kuwa baada ya jopo la madaktari wanane kumfanyia uchunguzi waligundua kwamba tatizo kubwa lililokuwa likimsumbua Mbowe ni uchovu ambalo kitaalam linaitwa ‘Fatigue’.
“Jopo la madaktari lilimfanyia vipimo na tumegundua kuwa tatizo kubwa linalomsumbua ni uchovu unaosababishwa na kusafiri na kufanya kazi kwa muda mrefu bila kupumzika.
“Uamuzi uliochukuliwa ni kumuweka mapumziko kwa ajili ya uangalizi zaidi ndani ya saa 48 lakini hali yake inaendelea vizuri anaweza kuruhusiwa muda wowote,” alisema Dk Sanga
Dk Sanga alieleza kuwa Mbowe alipokelewa hospitalini hapo kwenye kitengo cha magonjwa ya dharura akitokea katika hospitalia ya Doctors Plaza iliyopo Kinondoni.
Mwananchi lilishuhudia viongozi kadhaa wa upinzani wakiwasili katika Jengo la Moyo kumjulia hali kiongozi huyo.
Baadhi ya viongozi walioonekana ni Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Juma Duni Haji, Godbless Lema, Joshua Nassari na Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia.
Kwa upande wake, Mbowe aliwatoa hofu watanzania na kuwahakikishia kwamba yupo salama na waondokane na hofu ambayo imeonekana kuenea kwenye mitandao na vyombo vya habari.
“Hakuna hali yoyote ya hofu na wasiwasi kama ambavyo imeshaanza kujengeka kwenye mitandao ya kijamii nipo hospitali kwa sababu za kitabibu na si vinginevyo.
“Ninachoweza kuwaambia Watanzania niko salama na hali yangu inaendelea vizuri, tatizo nililonalo limetokana na kufanya kazi usiku na mchana bila kupumzika,” alisema Mbowe.
Mbatia aliwata watanzania kuendelea kumuombea kiongozi huyo na kuwaunga mkono Ukawa ili waendeleze harakati zao katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu.
“Suala la kuugua ni kawaida kwa kila binadamu ninachoweza kusema tuondelee kumuombea ili arejee kwenye mapambano na wazidi kutuunga mkono kwenye harakati zetu”Mbatia
Kuhusiana na uwezekano wa ugonjwa wa Mbowe kusitisha ziara za Ukawa mikoani Mbatia alisema ratiba inaendelea kama kawaida na afya ya kiongozi huyo ikitengemaa ataungana na wenzake kwenye harakati hizo.
Mbowe aliugua ghafla juzi akiwa katika maandamano ya kumsindikiza mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Edward Lowassa baada ya kuchukua fomu za kugombea urais katika Tume ya Taifa Uchaguzi (NEC).
MWANANCHI
Wakati kukiwa na taarifa zinazosambaa mtandaoni zikimuhusisha Dk Willibrod Slaa na akaunti ambayo imekuwa ikitoa msimamo wake wa kujitenga na shughuli za siasa pamoja na Ukawa, katibu huyo mkuu wa Chadema amekanusha taarifa hizo akisema hajawahi kuwa na akaunti ya twitter.
Hii ni mara ya pili kwa Dk Slaa kuzungumza na gazeti hili, lakini akikatakaa kufafanua mambo mbalimbali yanayohusu sakata lake na Chadema, akiahidi kuwa kufanya hivyo baadaye, huku akiweka bayana kuwa hajawahi kuwa na akaunti ya twitter.
Dk Slaa, aliyekuwa anatajwa kuwa mgombea urais wa Chadema, hajaonekana hadharani katika matukio makubwa ya kichama tangu Chadema na Ukawa walipomkaribisha waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa na kumteua kuwa mgombea urais anayeungwa mkono na vyama vinne vinavyounda umoja huo.
Mara ya mwisho kuonekana kwenye shughuli za chama hicho ni katika kikao cha Kamati Kuu wakati Lowassa alikaribishwa kufanya majadiliano na kujibu hoja za wajumbe.
Lakini baada ya hapo Dk Slaa hakuonekana wakati wa kutambulishwa kwa Lowassa kwa waandishi wa habari, tukio la kuchukua na kurudisha fomu za urais ndani ya chama na tukio la juzi la kuchukua fomu za urais kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Wakati hayo yakiendelea, kuna akaunti ya twitter yenye jina la “Dr Willibrord Slaa” ambayo imekuwa ikitoa kauli mfululizo zikiwa na ujumbe mbalimbali unaoendana na mazingira aliyomo sasa mwanasiasa huyo.
Agosti 10, kulitumwa ujumbe zaidi mara 10, mmojawapo ukijaribu kuwaaminisha watu kuwa hiyo ni akaunti halisi ya Dk Slaa.
“Ndugu zangu Watanzania, hii ni akaunti yangu rasmi, bila shaka yoyote na naomba ninachoandika hapa kifikishwe kwa Watanzania popote walipo,” unasema ujumbe huo.
Taarifa nyingine zilizotumwa kwenye akaunti hiyo ya twitter ni pamoja na ile iliyoeleza kuwa Dk Slaa ameomba ulinzi kutoka nchi na mashirika ya kimataifa na atazungumza kupitia runinga na redio pindi atakapopata ulinzi.
Akizungumza na gazeti hili jana, Dk Slaa alisema hajawahi kutuma taarifa yoyote kwenye mitandao ya kijamii.
“Sijawahi ku-operate (kuendesha) kitu chochote kwenye akaunti ya twitter, sina akaunti kama hiyo,” alisema Dk Slaa.
Mbali na kukanusha kumiliki na kuendesha akaunti hiyo, Dk Slaa alirudia kauli yake ya wiki iliyopita kuwa atatoa msimamo wake muda muafaka utakapofika, baada ya kuulizwa swali kuhusu hatma yake ndani ya Chadema na kisiasa kwa ujumla.
“Subira yavuta heri, sasa ili uipate hiyo heri unatakiwa kuvumilia. Kwa hiyo wakati ukifika nitazungumza tu na Watanzania,” alisema.
Alipoulizwa ni wapi alipo kwa sasa, alisema yupo Dar es Salaam anapumzika, lakini akasisitiza kuwa ipo siku ataweka wazi mustakabali wake kisiasa.
Dk Slaa alisema yeye na mke wake Josephine Mushumbusi wanatarajia kusafiri kwenda nje ya nchi katika siku chache zijazo, ingawa hakuweka wazi nchi anayotarajia kuitembelea, lakini akasema atarejea baada ya wiki moja.
NIPASHE
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imemhukumu mfanyabiashara Erasmus Mrosso maarufu kama Mnyee (35), kulipa faini ya Sh. 700,000 au kwenda jela miaka miwili baada ya kupatina na hatia ya kosa la kukutwa na bastola isivyo halali.
Hukumu hiyo ilisomwa jana na Hakimu Mkazi, Thomas Simba, baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka kuthibitisha makosa bila kuacha shaka.
Hakimu Simba alisema ushahidi wa mashahidi watano wa Jamhuri uliotolewa mahakamani hapo ulieleza kwamba askari polisi walipofanya upekuzi nyumbani kwa mshtakiwa walikuta bastola, lakini hawakuona kibali cha umiliki wake.
Alisema mshtakiwa alipopata nafasi ya kujitetea dhidi ya tuhuma hizo, hakuileza mahakama kama alikuwa na kibali cha kumiliki bastola hiyo au la.
“Mshtakiwa ameshindwa kuieleza mahakama kuhusu umiliki wa bastola hiyo na imemtia hatiani kwa kosa la kukutwa na silaha kinyume cha sheria,” alisema Hakimu Simba.
Alipopewa nafasi ya kujitetea ili apunguziwe adhabu, mshtakiwa alidai kuwa amekaa mahabusu muda mrefu mahakama impunguzie adhabu.
Hakimu alisema mshtakiwa atalipa faini hiyo na akishindwa atatumikia kifungo cha miaka miwili jela.
Hadi NIPASHE inaondoka mahakamani hapo mshtakiwa alishindwa kulipa faini na alikwenda jela kutumikia kifungo hicho.
Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa kuwa Agosti 3, mwaka 2011 eneo la Magomeni Kagera, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alikutwa na bastola bila kibali.
NIPASHE
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma, imetoa hati ya kukamatwa kwa Mbunge wa Kigoma Kusini aliyemaliza muda wake, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), baada ya kushindwa kuhudhuria mahakamani kwa ajili ya kesi yake inayomkabili mahakamani hapo.
Kafulila anakabiliwa na shitaka la kutumia lugha ya matusi dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Khadija Nyembo, kwa kumwambia hana maadili, ana akili finyu na ni kiumbe dhaifu, kitendo ambacho kingeashiria uvunjifu wa amani.
Hakimu wa Mfawidhi wa mahakama hiyo, Sylvester Kainda, alitoa hati hiyo jana baada ya upande wa mashitaka kuomba hati ya kumkamata mshtakiwa kwa kutohudhuria mahakamani pamoja na wakili wake, Daniel Rumenyela.
Upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Shabani Masanja, ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na mshtakiwa.
Masanja aliiomba mahakama hiyo kutoa hati ya kumkamata mshtakiwa pamoja na hati ya kuwaita wadhamini wake.
Kutokana na hali hiyo, Masanja aliiomba Mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali.
Hakimu Kainda alikubaliana na ombi hilo na kutoa hati ya kumkamata mshtakiwa pamoja na ya kuwaita wadhamini wake.
Aidha, aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 10, mwaka huu mshtakiwa atakaposomewa mshtakiwa maelezo ya awali.
Awali, mshtakiwa huyo aliposomewa shitaka lake alikana kutenda kosa hilo na yuko nje kwa dhamana ya mdhamini mmoja na mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh. milioni mbili.
Mapema, akisoma hati ya mashitaka, Masanja alidai kuwa Agosti mosi, mwaka 2013, katika kata ya Nguruka eneo la Rest House Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, mshtakiwa alitoa lugha ya matusi kwa Nyembo kuwa hana maadili, ana akili finyu na ni kiumbe dhaifu, kitendo ambacho kingeashiria uvunjifu wa amani.
Kafulila alipotafutwa na Nipashe kuhusiana na amri hiyo ya mahakama, alisema kuwa hakwenda kortini kutokana na wakili wake kutompa taarifa za kuwapo shauri hilo kwa siku ya jana.
Aidha, Kafulia alisema alikuwa akimtafuta wakili huyo ili amweleze sababu za kutompatia taarifa hiyo.
NIPASHE
Kikosi cha Usalama Barabarani kimekusanya zaidi ya Sh. bilioni 40 katika kipindi cha mwaka 2013/14 zinazotokana na faini ya makosa mbalimbali ya usalama barabarani.
Hayo yalisemwa na Inspekta wa Polisi, Deus Sokoni, kwenye semina ya siku mbili ya waandishi wa habari, kuzungumzia ajali za barabarani na jinsi zinavyochangia kusababisha vifo na ulemavu na kupoteza nguvu kazi kubwa ya taifa.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pia yalihudhuriwa na maofisa wa wizara hiyo, wawakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), madaktari wanasheria na baadhi wa vyombo vya habari.
Sokoni ambaye pia mwenyekiti wa kamati ya mradi huo wa usalama barabarani alisema katika kipindi cha mwaka 2013 zaidi ya Sh. bilioni 19 kilikusanywa katika makosa mbalimbali ya usalama barabarani na mwaka 2014 kiasi hicho kiliongezeka hadi kufikia zaidi ya Sh. bilioni 29.
“Pamoja faini zilizotozwa kwa madereva na kuingiza kiasi hicho cha fedha, bado ajali za barabarani zinaongezeka nchini” alisema.
Sokoni alisema ajali nyingi zinasababishwa na uendeshaji mbaya wa vyombo vya moto, madereva kuendesha huku wakiwa wamelewa, madereva wa magari ya mikoani kuendesha kwa muda mrefu na kujikuta wakisinzia na barabara za vumbi pia zinachangia kusababisha ajali.
Alisema pia kuna uzembe unaofanywa na jamii yenyewe kwa kupuuzia mwendo wa kasi wa madereva wa magari ya abiria na kusababisha ajali.
Alisema tatizo la ajali za barabarani linaweza kupunguzwa kwa kiasi kikubwa kwa ushirikiano baina ya jamii na askari wa usalama barabarani.
MTANZANIA
Raia wa Burundi aliyetambulika kwa jina la Buchumi Joel (39), amefariki dunia baada ya kuugua ugonjwa wenye dalili sawa na Ebola, ikiwa ni pamoja na kutokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili wake.
Madaktari, wauguzi na ndugu waliomuhudumia mgonjwa huyo, wamewekwa chini ya uangalizi maalumu kwa siku 21 kama hatua ya tahadhari, huku wakisubiri kupokea majibu ya sampuli za vipimo ili kubaini iwapo kweli ni ugonjwa wa Ebola ama la.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, daktari wa Shirika la Kimataifa linaloshughulika na Wahamiaji (IOM), Dk. Laurian Beda, alisema Joel aliingia Kigoma mwaka 2012 na kuishi kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu, Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma kwa muda wa miaka mitatu akiwa pamoja na familia yake.
Alisema akiwa kambini hapo alikuwa akisumbuliwa na maradhi, hivyo Julai 28 mwaka alisafiri hadi Kigoma Mjini pamoja na familia yake kwa ajili ya kusafirishwa na IOM kwenda nchini Marekani.
“Akiwa Kigoma, alifikia katika hosteli za Hoteli ya Nzimano, lakini Julai 31 mwaka huu alianza kuugua akitokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili mdomoni, kwenye fizi na machoni, na ilipofika Agosti 8, mwaka huu hali yake ilizidi kuwa mbaya, ndipo uongozi wa shirika uliamua kumpeleka katika Hospitali ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni kwa ajili ya matibabu zaidi,” Beda.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Maweni, Dk Shija Ganai, alithibitisha kupokewa kwa mgonjwa huyo na kumlaza wodi namba nane, lakini wakati wakiendelea kumtibu, usiku wa kuamkia jana hali yake ilibadilika na kuwa mbaya, na alfajiri alifariki dunia.
“Kutokana na dalili hizo, tunadhani ugonjwa huo unaweza kuwa Ebola, hivyo tumechukua sampuli za vipimo vyake kwa ajili ya kufanya uchunguzi zaidi na kuvipeleka maabara kuu ya Taifa kwa ajili vipimo ili kubaini ugonjwa uliosababisha kifo chake,” alisema.
Dk. Ganai, jana aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), kwamba dalili za mgojwa huyo hazithibitishi moja kwa moja kwamba alikuwa akiugua Ebola.
Alisema alikuwa anatoka damu kwenye mdomo, macho mekundu sana, nesi aliyekuwa akimuhudumia alithibitisha kuwa alikuwa anatokwa damu kwenye macho, alikuwa anahangaika sana, lakini hakuwa na homa kali.
MTANZANIA
Katika kile kinachoweza kutafsiriwa kama njia ya kuwaokoa mawaziri waliobwagwa kwenye kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kamati Kuu (CC) imefuta matokeo ya awali na kutangazwa kufanyika upya kwa uchaguzi upya kwenye majimbo matano.
Kutokana na kufutwa kwa matokeo hayo, CC imeamuru kurudiwa kwa kura za maoni kesho, na matokeo yake kuwasilishwa haraka ngazi za juu kwa ajili ya uamuzi wa mwisho.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema uamuzi huo umefanyika kutokana na kubainika dosari mbalimbali wakati wa upigaji kura za maoni uliopita.
Alisema marudio ya uchaguzi wa kura za maoni yatafanyika katika majimbo ya Kilolo (Iringa), Rufiji (Pwani) ambalo lipo chini ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Makete (Njombe) analowania Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Busega (Simiyu) lililo chini ya Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk. Titus Kamani na Ukonga (Dar es Salaam).
“Upigaji wa kura utafanyika siku ya Alhamisi Julai 13, mwaka huu (kesho) na kisha matokeo yaletwe haraka kwenye vikao vya maamuzi kwa ajili ya kufanya uamuzi wa mwisho,’’ alisema Nape.
Alipoulizwa dosari zilizobainika, alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia suala hilo kwa ndani, huku akitaka utekelezwaji wa maagizo hayo kwa mujibu wa utaratibu.
Kurudia kwa kura za maoni kunatokana na utata ulioibuka ambapo katika Jimbo la Busega uliibuka mvutano mkali uliosababisha matokeo kutangazwa baada ya siku tatu.
Katika matokeo hayo yaliyotangazwa chini ya ulinzi mkali wa polisi, Msimamizi wa Uchaguzi huo ambaye pia ni Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Busega, William Bendeke, alimtangaza Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Dk. Raphael Chegeni kuwa mshindi kwa kumbwaga Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk. Titus Kamani.
Akitangaza matokeo ya kura hizo za maoni zilizozua utata miongoni mwa wana CCM, ikiwamo kuibuka kwa tuhuma za rushwa na hata kadi hewa za chama, Bendeke, alisema Dk. Chegeni alipata kura 13,048 dhidi ya 11,829 alizopata Dk. Kamani.
Katika Jimbo la Kilolo, licha ya Mbunge anayemaliza muda wake, Profesa Peter Msola kupinga matokeo na hata kurudiwa kwa uchaguzi katika kata tatu, bado uchaguzi huo umeonekana haukuwa huru na wa haki.
Pamoja na kujitokeza dosari katika kura za maoni na kurudiwa kwa uchaguzi, wana CCM wa maeneo husika walisusia, hali iliyomfanya mbunge wa zamani, Venance Mwamoto kuibuka mshindi.
Katika matokeo ya awali kwenye baadhi ya vituo, Profesa Msola aliongoza kwa kura nyingi zaidi ambapo yaliibuka madai ya udanganyifu.
Pia yaliibuka madai ya kuwapo wapigakura wasio na kadi za CCM waliosafirishwa kwenda kupiga kura na mmoja wa wagombea wa ubunge katika Tawi la Kipaduka.
Katika Jimbo la Makete, yaliibuka madai ya dosari kadhaa hali iliyomfanya Katibu wa CCM Mkoa wa Njombe, Hosea Mpagike, kusema kuwa changamoto za miundombinu katika jimbo hilo zimesababisha kuchelewa kwa matokeo.
Katika uchaguzi huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Binilith Mahenge alipata kura 8,534 huku mpinzani wake wa karibu, Profesa Norman Sigala akipata kura 8,211, Bonic Muhami 500, Fabianus Mkingwa 466 na Lufunyo Rafael 226.
Hata hivyo, Profesa Sigala alipinga matokeo hayo kwa kuwasilisha malalamiko yake kwa vikao vya juu ambavyo jana vimetoa uamuzi wa kurudiwa kwa uchaguzi huo.
Awali katika Jimbo la Ukonga, matokeo yalikuwa yakimpa ushindi kada wa chama hicho, Ramesh Patel aliyepata kura zaidi ya 10,000 lakini baada ya muda hali hiyo ilibadilika ambapo aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, alitangazwa mshindi kwa kura 10,000 huku Patel akipata kura 7,576 hali ambayo ilisababisha mvutano mkali.
Katika Jimbo la Rufiji, awali matokeo yalionyesha Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, anayemaliza muda wake, Dk. Seif Rashid alikuwa ameangushwa na mpinzani wake Mohamed Mchengerwa kwa tofauti ya kura zaidi ya 400.
HABARILEO
Rais amefanya uteuzi wa balozi mmoja na kubadilishia wengine wawili vituo vya kazi; mmoja akiwa ni Wilson Masilingi anayekwenda nchini Marekani.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, Dar es Salaam jana, imetaja aliyeuteuliwa kuwa ni Charles Makakala anayekwenda kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe.
Kabla ya uteuzi huo, kwa mujibu wa taarifa hiyo, Makakala alikuwa Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi.
Kwa upande wa Masilingi aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, amehamishiwa Marekani kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Liberata Mulamula aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi na Ushirikiano wa Kimataifa.
Balozi Masilingi pia atakuwa anaiwakilisha Tanzania nchini Mexico.
Aidha, Balozi Irene Kasyanju aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Sheria, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ameteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi kushika nafasi inayoachwa wazi na Masilingi.
Katika hatua nyingine, Rais Jakaya Kikwete amemteua rasmi Joseph Masikitiko kuwa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS). Kabla ya uteuzi huo Masikitiko alikuwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo.
PAPO KWA PAPO zipate habari zote zinazonifikia za siasa muziki, michezo, maisha, Breaking news na nyingine kwa kujiunga hapa na mimi >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos