MWANANCHI
Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe amekata rufaa Mahakama Kuu kupinga hukumu iliyotolewa dhidi yake Julai, mwaka huu, na kumtoza faini ya Sh1 milioni baada ya kupatikana na hatia katika kosa la jinai.
Mbowe alitozwa faini ya Sh1 milioni au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kosa la kumshambulia mwangalizi wa ndani wa Uchaguzi Mkuu wa 2010 katika Wilaya ya Hai, Nassir Yamin.
Hata hivyo, Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na Mbunge wa Hai, alilipa faini hiyo na kuachiwa huru na Mahakama ya Wilaya ya Hai.
Katika rufaa hiyo namba 33/2015, iliyofunguliwa na wakili Peter Kibatala, Mbowe anailalamikia mahakama iliyomtia hatiani kuwa ilishindwa kushughulikia hoja muhimu katika kufikia uamuzi huo.
Pia, Mbowe analalamika kuwa mahakama ilishindwa kupima ushahidi kwa usahihi na pia, ilishindwa kutilia maanani ushahidi wa mashahidi wa upande wa utetezi akiwamo yeye.
Mbowe analalamika kuwa mahakama ilishindwa kutumia msingi wa jukumu la kuthibitisha shitaka pale ilipoeleza kuwa mashahidi wa upande wa mashtaka walitoa ushahidi uliojitosheleza.
Kwa mujibu wa Mbowe, Mahakama hiyo ilitakiwa itumie dhana ya upande wa mashtaka kuwa unatakiwa uthibitishe shtaka bila kuacha mashaka, jambo ambalo halikufanyika.
Mkata rufaa huyo anailalamika pia mahakama hiyo ilishindwa kueleza sababu zilizoifanya ifikie uamuzi wake huo kama inavyoelekezwa katika sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (CPA) kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.
Kutokana na sababu hizo, Mbowe ameiomba Mahakama Kuu kuifuta hukumu iliyomtia hatiani, kurejeshewa Sh1 milioni alizolipa kama faini na apewe nafuu nyingine yoyote ambayo mahakama itaona inafaa.
Rufaa hiyo imepangwa kusikilizwa Septemba 2, mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Aishiel Sumari.
MWANANCHI
Kuongezeka kwa majeruhi wa ajali za bodaboda kumeifanya Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), kuzidiwa na wagonjwa hadi kulazimika kuwalaza wengine sakafuni.
Ofisa Uhusiano wa Moi, Patrick Mvungi alisema asilimia 53 ya majeruhi wote wanaopokewa na taasisi hiyo ni wa ajali za pikipiki.
Wajumbe wa Kamati ya Usalama Barabarani, Kanda ya Dar es Salaam jana walitembelea wodi namba 17 na 18 za Jengo la Sewahaji na Wodi namba Mbili ya Jengo la Mwaisela na kujionea idadi kubwa ya majeruhi.
Majeruhi wengi waliolazwa Sewahaji ni vijana ambao baadhi yao wamekatika miguu, mikono na wengine wakiwa na majeraha vichwani.
Mvungi alisema kila siku taasisi hiyo inapokea majeruhi kati ya 20 na 26 na kwamba wengi wao ni wa ajali za pikipiki. “Wodi za kulaza majeruhi zimezidiwa tunalazimika wengine kuwalaza chini lakini wote wanapata matibabu,” alisema.
Alisema Wodi Namba Mbili, ambayo ni ya majeruhi wanawake, ina vitanda 33 lakini hadi jana ilikuwa na wagonjwa 54 na kwamba waliozidi wanalala sakafuni.
Alisema tatizo la wagonjwa kulala sakafuni liko katika wodi tatu zinazolaza majeruhi… “Tatizo hilo litamalizika hivi karibuni mara baada ya kumalizika kwa jengo la taasisi.”
Katika wodi ya wanaume namba 17 na 18 ya Jengo la Sewahaji, mmoja wa majeruhi hao, Fikiri Omari aliyevunjika mguu wa kulia, alisema alipata ajali ya pikipiki tangu Juni 28 na kwamba mipango yake imeharibika.
Alisimulia kwamba alipata na mkasa huo wakati akisubiri kuruhusiwa kwenye taa za barabarani baada ya kugongwa na gari ambalo halikusimama.
“Nina mke na watoto wanaonitegemea lakini miezi inazidi kupita nikiwa hospitalini huku hali yangu ikiwa bado mbaya,” alisema. Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Kanda ya Dar es Salaam, Fadhili Mgonja alisema: “Ninasikitika kuwaona vijana wadogo wakiwa wamekatwa viungo kwa sababu ya ajali za barabarani.”
Alisema madereva, hasa wa bodaboda, wanatakiwa kuwa makini wanapokuwa barabarani kwa sababu wengi wao hawafuati sheria. “Madereva wa bodaboda hawafuati sheria na hata askari wa usalama barabarani wakiwasimamisha hawasimami matokeo yake ni ajali,”
MWANANCHI
Chadema Wilaya ya Bariadi kimedai kunasa kadi 36 za kupigia kura zilizokuwa zimetupwa kwenye gofu la nyumba moja mjini Bariadi.
Hata hivyo, Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Erika Musika alisema hana taarifa yoyote kuhusiana na kadi hizo… “Nimerudi leo kutoka kwenye Mbio za Mwenge.
Kama kuna tatizo hilo tutawataarifu NEC (Tume ya Taifa ya Uchaguzi) halafu watatoa majibu.” Chadema kimedai kuwa kadi hizo za kupigia kura (ambazo majina yake tunayo), zilionekana jana katika nyumba karibu na uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, mbili zilikuwa za mtu mmoja zenye picha na namba zinazofanana.
Kadi nyingine mbili ni za watu wawili tofauti na zina rangi ya pinki na kijani zenye nembo ya NEC, jambo linalodaiwa kuwa ni njama chafu zinazofanywa kwa lengo la kutaka kukibeba chama kimoja.
Katibu Mwenezi wa Chadema Wilaya ya Bariadi, Martin Mogan alidai kwamba kadi hizo zimetengenezwa kwa lengo la maalumu la kukibeba chama kimoja katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
“Mara ya kwanza jana asubuhi tulipata kadi 21 zikiwa zimetupwa kwenye hilo jumba bovu. Kadi nyingine 15 tulizipata maeneo ya karibu na Benki ya NMB mjini Bariadi zikiwa zimetupwa pia. Tutazipeleka polisi.”
Mogan aliitaka NEC itoe maelezo… kuhusu kadi hizo akisema hizo ni dalili za goli la mkono.
Mwanasheria wa Chadema Kanda ya Serengeti ambaye pia ni mgombea ubunge Jimbo la Bariadi, Godwin Ngwilimi alisema kupatikana kwa kadi hizo kunathibitisha kuwa kuna njama za kuiba kura Oktoba 25.
MWANANCHI
Vyama vya Chadema na CCM vimeingia katika mchuano wa kuwania nafasi ya kurusha matangazo ya moja kwa moja ya kampeni za wagombea urais katika televisheni Jumamosi hii.
Wakati Chadema ikitaka muda wa kurusha matangazo ya uzinduzi wa kampeni za mgombea wake, Edward Lowassa kutokea jijini Dar es Salaam, CCM inataka kurusha matangazo ya mkutano wa kampeni ya mgombea wake, Dk John Magufuli kutoka jijini Mbeya.
Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene alisema jana kuwa kumekuwa na njama za CCM kutaka kuzuia fursa ya Chadema kurusha kampeni za mgombea wake kwa kutaka siku hiyo irushe kampeni za Dk Magufuli.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikiri chama hicho kutaka kurusha matangazo ya mgombea wake na kuhoji; “tatizo liko wapi kama Chadema imechelewa kulipia?”
“Ni kweli mgombea wetu wa urais akiwa Mbeya tutarusha matangazo ya kampeni zake moja kwa moja kwenye runinga, sasa ni runinga ngapi siwezi kujua maana kuna watu wanalifanyika kazi suala hilo. Lakini kama Chadema walijua wana tukio lao kwa nini wasingewahi kulipia?” alihoji.
Chanzo cha habari kutoka kituo kimoja maarufu, kimeeleza kuwa kwa nyakati tofauti, CCM na Chadema waliomba muda wa kurusha vipindi vyao, lakini CCM ndiyo waliofanikiwa kupata.
“Ninachojua hao wote walikuja kwa nyakati tofauti kuomba muda na CCM ndiyo waliofanikiwa kupata,” alidokeza mmoja wa wafanyakazi wa telesheni hiyo ambaye hakutaka kutaja jina kwa maelezo kuwa siyo msemaji.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Azam TV, Tido Mhando alisema CCM na Chadema vilikuwa vimeomba kurushiwa matangazo yao na vyote vimelipia. Alisema kila moja kitapata fursa hiyo kwa kuwa kituo chake kina channel nyingi.
JAMBOLEO
Chama cha ACT – Wazalendo kitazindua kampeni zake za uchaguzi kwa kuwatambulisha wagombea wote wa ubunge waliosimamishwa kwenye majimbo ya Tanzania –Bara na Zanzibar. Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika Agosti 30 katika Uwanja vya Zakhem Mbagala, wilayani Temeke kuanzia saa nne asubuhi.
Katibu wa Mipango na Mikakati wa ACT – Wazalendo, Habibu Mchange aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba maandalizi ya uzinduzi huo yanaendelea vyema na kwamba hafla hiyo itahudhuriwa na viongozi wote wa kitaifa wa chama hicho wakiwamo Kiongozi wa Chama, Zitto Kabwe na Mwenyekiti wake, Anna Mghwira ambaye pia ni mgombea urais.
“Baada ya mwenyekiti wetu, Mama Mghwira kuchukua fomu ya kugombea urais, Watanzania wamekuwa na shauku ya kutaka kujua mustakabali wetu kuelekea Uchaguzi Mkuu,” alisema na kuongeza: “Hivyo basi tunawakaribisha wananchi wote siku hiyo waje kushuhudia kampeni za kisayansi.
Ndiyo maana tumeamua kuwaita wagombea ubunge wote kuhudhuria na kuwatambulisha rasmi kwa Watanzania.”
Alisema ACT – Wazalendo imejipanga kuchukua dola na kuleta siasa safi, tofauti na vyama vingine akisisitiza kuwa kina nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo ya Watanzania. Hivyo kuwataka wananchi kuhudhuria.
Alisema katika siku ya uzinduzi, kwa mara ya kwanza wabunge waliohama kutoka vyama vya CCM, CUF na Chadema watazungumza, pia wataendelea kuinadi ilani ya uchaguzi wa chama hicho. Alisisitiza kuinadi kaulimbiu ya chama hicho ya utu, uadilifu na uzalendo.
Katibu wa Fedha na Rasilimali ya chama hicho, Peter Mwambuja alisema pia kimejipanga kufanya siasa za malengo na masuala kwa maendeleo ya Watanzania siyo kupiga propaganda.
MTANZANIA
Siku moja baada ya mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edward Lowassa, kuzuiwa na polisi kutembelea wananchi mitaani, Manispaa ya Ilala imeuzuia umoja huo kutumia viwanja vya Jangwani kufungua kampeni zao keshokutwa kwa maelezo kuwa vimewahiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ukawa inayoundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD iliomba kufanya mkutano wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mkuu katika viwanja hivyo Agosti 29.
Awali Ukawa waliomba Uwanja wa Taifa, lakini walikataliwa kwa maelezo kuwa uwanja huo ni wa Serikali na hauruhusiwi kutumika kwa shughuli za kisiasa.
Jana Manisipaa ya Ilala ililieleza kwamba CCM, tayari waliomba kutumia viwanja vya Jangwani Agosti 23 kwa ajili ya uzinduzi wa kampeni zao na siku tatu zaidi kuanzia Agosti 28 hadi 30 kwa matumizi mengine ya kisiasa.
Ofisa Utamaduni wa Manispaa ya Ilala, Claud Mpelembwa alisema kuwa Ukawa walichelewa kuomba viwanja hivyo, kwani CCM licha ya kuvitumia Agosti 23, wameviomba tena Agosti 28, 29 na 30 kwa ajili ya shughuli zao za kisiasa.
“Hatujawanyima uwanja, hata barua tuliyowaandikia wanayo inajieleza. Unajua Jangwani ni mojawapo ya maeneo ya wazi, mtu yeyote anaweza kuomba. Ukawa wao waliomba Uwanja wa Taifa na baada ya kukataliwa hawakuleta maombi kwetu.
“CCM waliomba kutumia Agosti 21, 22 na 23 na kisha wakaomba tena kutumia Agosti 28, 29 na 30. Chadema wamekuja kuomba Agosti 24. Walipokuja tukasema basi tukae tuongee, tunaweza kuwapatia Septemba 3,” Mpelembwa.
Alisema kwa kuwa ndiyo kwanza kampeni zimeanza, bado wanaweza kuzungumza ili wapewe tarehe nyingine.
Hata alipoulizwa kuhusu ratiba ya kampeni inayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), inayoviongoza vyama vya siasa kufanya kampeni mkoa kwa mkoa, Mpelembwa alisema ratiba hizo huwa hazipelekwi kwenye manispaa.
Alipotafutwa kupitia simu yake ya kiganjani, Mkurugenzi wa NEC, Kailima Ramadhan Kombwey, alisema bado hawajapata taarifa kutoka Chadema kuhusu kunyimwa kufanya uzinduzi wa mkutano wa kampeni kwenye viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam.
Hivi karibuni Serikali ilikataa ombi la Chadema la kutumia Uwanja wa Taifa kuzindulia kampeni zake.
Akitoa majibu ya Serikali, Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Assa Mwambene, alisema kwa mazingira ya sasa hayaruhusu kutumika kwa uwanja huo kwa ajili ya mihadhara ya vyama vya siasa.
Awali kabla ya kutolewa kwa kauli ya Manispaa ya Ilala, Mwenyekiti mwenza wa Ukawa ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema mkutano huo uko palepale hata kama wamezuiwa.
Mbatia pia alilalamikia kitendo cha vyombo vya usalama na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuingilia harakati zao za siasa huku vikiipendelea CCM.
Mbali na kuzuiwa kutumia viwanja vya Jangwani kuzindulia kampeni zao, Mbatia alilalamikia upendeleo unaofanywa na viongozi wa Serikali na vyombo vya dola kwa CCM huku vikikandamiza vyama vya upinzani.
MTANZANIA
Mombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema akifanikiwa kushinda Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, atakuwa na baraza dogo la mawaziri litakalofanya kazi usiku na mchana.
Akihutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa kampeni mkoani Rukwa juzi, Dk. Mgufuli alisema mawaziri wake watahudumia wananchi kwa wakati na si kukaa ofisini na kusubiri kuletewa taarifa.
“Nitateua mawaziri wachache na wenye uadilifu, kama kuna waziri nitakayemteua na akaona hawezi kazi akae pembeni, kwa sasa Watanzania wanataka huduma kwa wakati.
“Haiwezekani mnatuchagua bure kisha na nyinyi mkose huduma, hili hapana ni lazima muhudumiwe bure na kwa wakati,” alisema Dk. Magufuli.
Alisema Serikali atakayoiunda itakuwa na watu waadilifu na haitakuwa na ngojangoja katika kuwahudumia wananchi.
“Ninajua hapa Laela kuna mradi wa maji unasuasu, najiuliza nikiwa Waziri wa Ujenzi nilifukuza wakandarasi 3,200, sasa kwa nini huyo wa maji yupo? Sasa naomba nafasi ya urais na hawa makandarasi wamaji wajiandae.
“Ninafahamu Watanzania wanataka mabadiliko, wamechoshwa na uonevu na wanataka maendeleo ya haki. Katika uongozi wangu sijawahi kukemewa wala kujiuzulu, siri kubwa ya hilo ni kwamba nilikuwa namtanguliza Mungu,” alisema.
Akizungumzia masilahi ya wafanyakazi na Polisi, alisema katika uongozi wake atahakikisha anaweka mazingira bora ya kazi.
“Katika utawala wangu polisi watapata masilahi bora ikiwa ni pamoja na vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi.
“Tunahitaji kuwa na Jeshi la Polisi bora na imara na hatuhitaji kuwa na jeshi la uonevu. Leo mtu anakamatwa na askari kwa kosa la kuwa na bodaboda kisha anabambikiwa kesi nyingine, hii hapana,”alisema.
Kwa upande wake Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema hana kinyongo na Dk. Magufuli na kwamba anashirikiana naye tofauti na baadhi ya watu wanavyodai.
Pinda ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu (CC), alisema licha ya yeye kuwa miongoni mwa makada 38 waliorudisha fomu kuomba kuteuliwa katika nafasi ya urais, ameridhika na mchakato wa ndani ya chama.
“Leo (jana) nipo hapa kwa ajili ya kushiriki kampeni za Magufuli, nimeridhika na moyo wangu mweupe kabisa sina kinyongo na mgombea wetu.
“Na nimekuja mwenyewe sitaki kusemewa maana kuna watu walishaanza ohooo mara hajaonekana katika uzinduzi wa kampeni … nimekuja sasa nilianza na ndugu Magufuli Katavi na sasa nipo Sumbawanga.
“Mmeona barabara zetu za lami pamoja na mimi kuwa kiranja wa Serikali mtendaji wa hizi barabara ni Magufuli, ujenzi huu alikuwa waziri je akiwa rais ni lazima atamaliza zote na zawadi yetu kubwa ni Oktoba 25 kura zote kwa Magufuli,” alisema Pinda .
Dk. Magufuli, alisema anaomba kura kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania na kuhakikisha anawaletea maendeleo ya kweli.
Alisema hakuamini kama CCM ingemteua ila ni uwezo wa Mungu ndio umemfikisha mahali hapo kutokana na dua za Watanzania na wana CCM.
“Ninajua hapa Sumbawanga kura zote mtanipa mimi lakini siwezi kufanyakazi peke yangu ninawaomba mnichagulie mbunge Aeshi Hilal, ninamuamini maana alikuwa kila siku ananisumbua ndani ya Bunge na ofisini kwangu kutaka pesa za kukamilisha barabara.
“Kubwa mkituchagua mimi na Aeshi mbunge wenu, nitahakikisha namaliza ujenzi wa barabara zote pamoja na Uwanja wa Ndege Sumbawanga kwa kuujenga kwa kiwango cha lami.
“…lakini pia Serikali yangu itakuwa na kazi ya kutoa huduma zenye staha kwa Watanzania nitahakikisha tunatoa elimu bure kwa wanafunzi wote kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne,” alisema Dk. Magufuli.
Akizungumzia tatizo la rushwa nchini alisema amejipanga kupambana kwa vitendo na watendaji wabovu ambao wamekuwa wakikwamisha juhudi za maendeleo.
Alisema kutokana na kukithiri kwa hali hiyo anajua wala rushwa na watendaji wanaomchukia kwa usimamizi wake hawatampa kura ila wananchi wengi ambao ndio watetezi wake ndio watamchagua kwa wingi.
Alisema anajua Tanzania ina rasilimali nyingi ikiwemo madini, hifadhi za Taifa lakini bado kuna watu wamekuwa wakwepa kodi za Serikali.
MTANZANIA
Mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Waziri wa zamani, Edward Lowassa, leo anatarajiwa kuzungumza na wanawake wa makundi mbalimbali nchini katika kongamano lililoandaliwa na Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha).
Mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee, aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa Lowassa atazungumza na wanawake hao kupitia televisheni mbalimbali zitakazorusha tukio hilo moja kwa moja.
Alisema katika mkutano huo mgombea huyo wa Ukawa atawaeleza mipango atakayoifanya akipata dhamana ya kuwa rais wa awamu ya tano baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
“Katika mkutano huo, Lowassa atazungumza na makundi ya watu wenye ulemavu, wachuuzi, mama lishe, wagonga kokoto, wauza baa, wafanyakazi wa saluni, waandishi wa habari, wasanii wa kike, wanaharakati, viongozi wa Bawacha, wabunge, mabalozi, wanawake wa nchi mbalimbali, walimu, wainjilisti, mahajati, wauguzi, wauza mitumba, wanavyuo wa kike, ‘madada poa’ na wengineo,”alisema Halima.
Mwenyekiti huyo wa Bawacha alielezea kuwa lengo la kongamano hilo ni kuwaunganisha wanawake wa makundi hayo waweze kushiriki kwa ukamilifu katika uchaguzi huo.
“Kama mnavyofahamu idadi ya wanawake nchini ni asilimia 52 kwa mujibu wa takwimu za sensa ya mwaka 2012 ya Watanzania wote, ambao ni zaidi ya nusu. Tunafahamu kundi hilo ndilo lenye zaidi ya asilimi 58 ya wapiga kura waaminifu, hivyo Bawacha ina wajibu wa kutumia haki yao ya katiba ya kupiga kura kwa maslahi mapana ya Taifa,” Halima.
Alisema kaulimbiu ya mkutano huo itakuwa “Lowassa na hatma ya changamoto za wanawake Tanzania” ikiwa na lengo la kuleta mageuzi makubwa katika maisha ya wanawake Tanzania.
Kongamano hilo ambalo Lowassa atafuatana na mkewe, Regina, ni mwanzo wa uzinduzi wa kampini pana zitakazofanywa na Bawacha nchi nzima zitakazojumuisha kanda 10 na kuongozwa na wajumbe wa Kamati Kuu, wabunge na kundi maarufu la 4U Movement.
HABARILEO
Polisi imesema inaandaa mipango ya kumtuma mtu nchini Kenya kwa ajili ya kupata taarifa kamili kuhusu, madai ya kukamatwa kwa Watanzania sita na kuhusishwa na ugaidi nchini Kenya.
Vyombo vya habari vya Kenya, viliripoti juzi kuwa Watanzania sita walikamatwa katika Mji wa Garissa nchini humo, wakiwa na bastola na mabomu saba.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, watanzania hao walikuwa wanakwenda Somalia kwa ajili ya kujiunga na kundi la wanamgambo la Al-Shabaab.
Akizungumza na gazeti hili, kuhusu taarifa hizo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Kamishna wa Polisi, Diwani Athumani, alisema hawajapata taarifa kamili kuhusu suala hilo, kutoka Kenya.
“Hatujapata taarifa kutoka Kenya kuhusu suala hilo, sisi tumelisikia kwenye vyombo vya habari. Lakini tunaandaa mipango ili tuweze kumtuma mtu Kenya ili kupata hali halisi kuhusu kukamatwa kwa watanzania hao,” alisema Athumani.
Juzi Mratibu wa Polisi wa Kanda ya Kaskazini Mashariki, Kenya, Mohamud Saleh, alipozungumza na waandishi wa habari katika mji wa Garissa, alisema wanaume wanaokadiriwa kuwa na umri wa miaka 20 hadi 40, walikamatwa katika mji wa Daddab wakijaribu kuvuka mpaka kuingia Somalia.
Alisema watu hao wanashikiliwa katika mji huo wa Garissa ambako watahojiwa kupata taarifa zaidi. Aidha, alisema mapema wiki hii, wanawake wawili mmoja raia wa Kenya na mwingine wa Tanzania, walikamatwa wakienda Somalia kwa ajili ya kuolewa na wanaume wa Al-Shabaab.
NIPASHE
Jumla ya watu 10 hadi kufikia jana walikuwa wameshapoteza maisha kutokana ugonjwa wa kipindupindu jijini Dar es Salaam huku 93 wakiwa wamelazwa kwenye kambi zilizotengewa kwa ajili ya walioathirika na ugonjwa huo.
Nipashe ilitembelea katika Kambi ya Mburahati wilayani Kinondoni jana na kushuhudia madaktari na wauguzi wakiendelea kutoa matibabu.
Msimamizi wa kambi hiyo, ambaye pia ni Mratibu wa Mafunzo Idara ya Afya Wilaya ya Kinondoni, Alfred Ngowi, alisema hadi kufikia jana wagonjwa 65 wa kipindupindu kati yao wakiwamo wanaume 36, wanawake 18 na watoto 11 walikuwa wamelazwa katika kambi hiyo.
Katika Wilaya Kinondoni hadi sasa watu watano wameshafariki wakiwamo wawili wakazi wa Alimaua, mtoto wa mwaka mmoja na nusu (Mwanyamala) na wengine wawili wa eneo hilo.
“Mpaka jana asubuhi kulikuwa na wagonjwa 52 lakini waliongezeka 13 na kufanya idadi kufikia 65 wakitokea majumbani na katika Kituo Cha Sinza,” alisema Ngowi.
Aidha, alisema wagonjwa wote wa kipindupindu hupokelewa katika kambi za Sinza na Mwanayamala na kupewa huduma ya kwanza kisha hupelekwa kwenye Kambi Kuu ya Mburahati kwa matibabu zaidi.
Ngowi alisema maeneo yaliyoathirika ni Manzese mtaa wa Mianzini, Tandale, Kijitonyama, Kinondoni, Ubungo, Wazo na Goba.
Aliongeza kuwa, kabla ya wagonjwa kuruhusiwa kurudi nyumbani, hupewa elimu ya afya na jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo huku wakipewa dawa za kuweka kwenye maji na kumwaga katika vyoo zikiwamo Waterguard na Chlorine kwa ajili kuzuia maambukizi.
Aliishukuru Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Msalaba Mwekundu na Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa misaada wanayoendelea kuitoa.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Mussa Natty, alisema manispaa hiyo ilianza kufanya mikakati ya kupambana na ugonjwa huo kabla wizara husika haijatoa agizo la kupiga marufuku ya uuzaji vyakula kiholela na maji ya kunywa maarufu kama ‘Kandoro’.
Alisema kwa kuzingatia madhara ya ugonjwa huo wananchi walipewa elimu ya jinsi ya kujikinga na kupeleka wataalamu wa afya katika mitaa na kata kutoa elimu.
Kwa upande wa Mganga Mkuu wa Wilaya Ilala, Dk. Victorina Ludovick, alisema wagaonjwa 25 wa kipindupindu walikuwa wamelazwa katika Kituo cha Afya cha Buguruni Mnyamani.
Dk. Ludovick alisema katika wilaya hiyo tangu ugonjwa huo uanze kimeshatokea kifo cha mtoto mmoja wa kike wa miaka mitatu mkazi wa Buguruni Kisiwani.
Aliyataja baadhi ya maeneo yaliyoathirika kuwa ni Buguruni, Vingunguti, Gongo la Mboto, Majohe na Tabata.
Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Dk. Sylivia Mamkwe, alisema katika Kambi ya Temeke watu watatu pekee ndio waliolazwa huku wanne wakiruhusiwa kwenda nyumbani. Maeneo yaliyoathirika katika wilaya hiyo ni Keko na Mtoni kwa Azizi Ali.
Jumanne wiki hii, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid alitoa agizo la kupiga marufuku biashara ya uuzaji chakula kiholela bila kuzingatia usafi na maji ya kunywa maarufu kama kandoro Jijini Dar es Salaam na mkoani Morogoro
PAPO KWA PAPO zipate habari zote zinazonifikia za siasa muziki, michezo, maisha, Breaking news na nyingine kwa kujiunga hapa na mimi >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos