HABARILEO
Makampuni 15 yaliyokwepa kodi baada ya kutorosha makontena yao, yamejisalimisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), lakini yameshindwa kulipa kodi ndani ya siku saba za msamaha wa Rais John Magufuli.
Kodi inayodaiwa kwa kampuni hizo ni Sh bilioni 3.75, hivyo watachukuliwa hatua za kisheria kwa kukwepa kulipa kodi, ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.
Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dk Philip Mpango alisema hayo jana wakati akielezea makusanyo ya kodi ya makontena yaliyoondolewa katika bandari kavu ya Azam, kinyume cha sheria pamoja na kumalizika kwa siku saba alizotoa Rais Magufuli kwa wafanyabiashara hao kulipa kodi waliyokwepa, bila kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria.
Dk Mpango alisema siku hizo saba zimefikia kikomo juzi, hivyo hatua kali za kisheria kwa wafanyabiashara ambao hawakulipa kodi katika kipindi hicho zinafuata hivyo wasubiri cha moto.
“Tumewasihi waje kulipa kwani huruma ya Rais sasa imeisha… tulifanya uhakiki na kuthibitisha kuwa kampuni hizo zipo. Wamekuja kulalamika lakini hakika hakuna atakayesamehewa kulipa na sasa tunafuata mkondo wa sheria ili kuwafikisha mahakamani,” alisisitiza.
Wadaiwa Alitaja kampuni hizo kuwa ni Ahmed Saleh Tawred anayedaiwa Sh milioni 59.23; Cla Tokyo Limited Sh milioni 77.52; Farida Abdullah Salem Sh milioni 75.33 na Juma Kassem Abdul Sh milioni 190.18.
Wengine ni Libas Fashion Sh milioni 52.94; Rushy Wheel Tyre Center Co Ltd, Sh bilioni 1.8; Said Ahmad Hamdan Sh milioni 68.36; Said Ahmed Said Sh milioni 68.73 na Salum Continental Co Ltd Sh milioni 151.17. Pia yumo Salum Link Tyres Sh milioni 343.44; Simbo Yonah Kimaro, Sh milioni 69.22; Snow Leopard Building Material Co Ltd Sh milioni 93.97; Swaleh Mohamed Swaleh Sh milioni 34.68; Tybat Trading Co Limited, Sh milioni 598.69 na Nasir Saleh Mazrui Sh milioni 70.10.
Alisema mpaka kufikia jana TRA walikuwa wamekusanya Sh bilioni 10,643.004,948.46 kutoka kwa kampuni 28 ambapo kampuni 13 zimelipa kodi yote iliyokadiriwa, ambayo ni Sh 4,167,130,173.89 na Sh 2,303,637,554.57 kutoka kampuni 15 zilizolipa sehemu ya kodi iliyokadiriwa.
Dk Mpango alisema Sh bilioni 4.17 zimelipwa na kampuni ya Azam ICD, ikiwa ni dhamana ya kodi iliyokwepwa, hivyo atatakiwa kumaliza kulipa kodi yote inayodaiwa kwa mujibu wa nafasi yake kama mwenye dhamana.
Alisema wakati utekelezaji huo ukiendelea, ili kurahisisha ukusanyaji wa kodi hiyo ya makontena yaliyoondolewa bandarini kinyume cha sheria na taratibu za forodha, TRA imefungua akaunti maalumu katika Benki Kuu yenye namba 9921169785 inayoitwa Commissioner for Customs and Excise – Container Account.
Kwa mujibu wa Dk Mpango, mpaka sasa watumishi 36 wa TRA wanaotuhumiwa kushiriki katika upotevu wa kodi kutokana na makontena hayo kuondoshwa bandarini.
Watumishi wachongewa Aidha, alisema TRA imepata taarifa zisizopungua 15 kutoka kwa wananchi kuhusu mali za kifisadi na mwenendo mbaya wa baadhi ya watumishi na walipakodi wanaokwepa kodi. Aliwashukuru wananchi waliotoa taarifa na kuwaomba wengine wajitokeze kutoa taarifa zaidi na mamlaka hiyo inawahakikishia kuwa itawalinda.
Dk Mpango alisema wanaendelea kutekeleza maagizo ya Rais katika ukusanyaji wa mapato, ikiwa ni pamoja na kupiga picha makontena yote badala ya sampuli ya kontena ilivyo sasa na wanafanya utaratibu wa kupata mashine za kupiga picha za nyongeza.
HABARILEO
Wakati wapinzani wakipinga uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, waziri huyo amewasihi wananchi kumvumilia kidogo, ili baada ya muda mfupi atoe mpango wa maendeleo ya wizara hiyo, ambao pamoja na mambo mengine, utaelezea bei ya nishati hiyo itakavyoshuka.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, Profesa Muhongo alisema mbali na mkakati wa kushusha bei ya umeme, kasi ya kusambaza umeme vijijini kupitia miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), itarejea palepale.
“Nimepokea uteuzi huo, kinachofuata ni kuwatumikia wananchi, niwaombe tu wanivumilie kidogo nitawapa mpango wangu wa maendeleo wa muda mfupi na mrefu, lakini nisisitize tu nishati sio siasa, ni suala la utaalamu, liachwe lifanywe kitaalamu,” alisema Profesa Muhongo.
Akizungumzia bei ya umeme na upatikanaji wake, Profesa Muhongo alisema kupunguza bei hiyo ni ajenda muhimu itakayozingatiwa na kusema ili umeme uwe wa uhakika, ni lazima kuwe na mipango ya kuwa na nishati hiyo ya uhakika ifikapo mwaka 2025.
“Umeme wa uhakika utapatikana na matarajio yetu ni Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 ambapo tunatarajia uzalishaji wa nishati hiyo ufike Megawati 10,000 hadi 15,000,” alisema Profesa Muhongo.
Alisisitiza kwamba wizara yake haitategemea chanzo kimoja cha nishati bali wataangalia vyanzo vingine ikiwemo nishati jadidifu, upepo, gesi, makaa ya mawe, maji huku akisema vyanzo hivyo vikitumika kuzalisha nishati, ni wazi bei ya umeme itashuka na kushusha gharama nyingine za maisha na za uwekezaji.
Aliongeza katika kuendeleza sekta ya nishati suala la uwekezaji ni muhimu hivyo wizara yake inakaribisha wawekezaji wenye sifa, watakaowekeza kwenye sekta hiyo ili kuja na matokeo bora zaidi, wananchi wanufaike na rasilimali za nchi yao.
Pamoja na nia yake hiyo kwa wananchi, Profesa Muhongo anakabiliwa na pingamizi kutoka kwa wanasiasa wa vyama vya upinzani, akiwemo Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) na aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba.
Lissu na Profesa Lipumba, wamekaririwa wakikosoa uteuzi wa Profesa Muhongo kwa madai kuwa wizara aliyopewa kuiongoza, ilikumbwa na kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow wakati wa uongozi wake, ikasababisha ajiuzulu.
Hata hivyo, Profesa Lipumba na Lissu katika kukosoa huko, hawakutaka kutumia kumbukumbu zilizo wazi kuwa uchunguzi dhidi ya Profesa Muhongo, ulibaini kuwa hakukiuka maadili yoyote katika sakata la utoaji wa karibu Sh bilioni 300 zilizokuwa katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu (BoT).
Matokeo ya uchunguzi huo yalitangazwa Mei mwaka huu na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ambapo alisema Tume ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ndiyo ilifanya uchunguzi kama Profesa Muhongo alistahili kwenda kwenye Baraza la Maadili kujibu mashitaka, lakini hawakuona tatizo lake na kufunga shauri lake.
Balozi Sefue aliweka wazi kuwa Profesa Muhongo alijiuzulu kwa sababu za kisiasa, lakini kimaadili hakuhusika kwa namna yoyote, kutokana na uchunguzi wa Sekretarieti ndiyo sababu hakufikishwa katika Baraza la Maadili.
HABARILEO
Wananchi katika majimbo ya Arusha Mjini na Handeni Mjini mkoani Tanga, watafanya uchaguzi wa wabunge wao leo.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva, jijini Dar es Salaam.
Pia alisema wananchi wa Kata ya Mvomero mkoani Morogoro, nao watamchagua diwani leo. Wananchi wa majimbo hayo mawili na kata hiyo, hawakupiga kura katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Siku hiyo, uchaguzi uliahirishwa katika majimbo saba nchini, ikiwemo Arusha Mjini na Handeni Mjini, kata ya Mvomero na nyinginezo 34 nchini.
Tangu wakati huo hadi sasa, uchaguzi umeshafanyika katika baadhi ya majimbo na kata nchini.
Lubuva aliwaomba wananchi waliojiandikisha kama wapigakura katika majimbo na kata husika, kujitokeza leo kwenye vituo walikojiandikisha ili kupiga kura na kuwachagua na viongozi wanaowataka.
“Kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, nawapongeza wananchi wote katika majimbo na kata zinazofanya uchaguzi kutokana na utulivu waliouonesha katika kipindi chote cha kusubiri siku ya kupiga kura kuchagua wabunge aumadiwani wao,” alisema Jaji Lubuva.
Alisisitiza kwamba taratibu zilizotumika katika uchaguzi mkuu tarehe 25 Oktoba mwaka huu, ndizo hizo hizo zitakazotumika.
“Vituo vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni. Iwapo wakati wa kufunga kituo watakuwepo wapiga kura katika mstari, ambao wamefika kabla ya wakati wa kufunga kituo na hawajapiga kura, hao wataruhusiwa kupiga kura. Mtu yeyote hataruhusiwa kujiunga katika mstari wa wapigakura baada ya saa kumi jioni”, alisema Jaji Lubuva.
HABARILEO
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amesema atafanya kazi kwa kasi ya Rais Magufuli katika kukabiliana na changamoto zilizopo katika wizara hiyo.
Amesema changamoto ziko nyingi kuanzia chini mpaka juu, katika Mahakama, magereza na kwingineko, hivyo aliomba apewe muda kuangalia hali ikoje ili abadilishe mifumo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
Akizungumzia suala la Katiba Mpya, alisema Rais alieleza vizuri kuwa litafanyiwa kazi, kwani halikuishia pabaya hivyo muda ukifika litakamilika.
Alisema watafanya kazi kubwa ili mfumo wa sheria usiwe pingamizi, bali uendeleze kasi aliyoanza nayo Rais Magufuli.
Nape Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye alisema atatengeneza utaratibu katika wizara hiyo, ili kuondoa utamaduni wa mtu mmoja kufanya mambo mengi peke yake na kuahidi kuwa msikivu na kutengeneza sheria, ili kila mmoja atimize wajibu.
Akizungumzia changamoto katika michezo, Nape alisema tatizo katika michezo ni usimamizi wa sheria na kutokuwa na nidhamu kwa kila mtu kufanya anavyotaka. Alisema zamani wanamichezo walikuwa wakifanikiwa kutokana na nidhamu, hivyo watasaidiana na wadau mbalimbali kurudisha nidhamu.
Manyanya na elimu ya juu Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Stella Manyanya, alisema kinachosubiriwa ni kasi ya kuleta mabadiliko kwa muda muafaka na jambo la msingi ni kazi na kila mtu ahakikishe anatimiza wajibu wake.
Alisema changomoto katika wizara hiyo ni nyingi, ikiwemo suala la mikopo ya elimu ya juu na kusisitiza kwamba wanafunzi wote wenye sifa ya kupata mikopo, wanapaswa kupewa kwa kuwa huo ni mkopo ambao wataurudisha.
Manyanya alisema wizara hiyo haitamvumilia mwalimu yeyote mzembe, atakayetumia muda wake vibaya kwa kutotimiza wajibu, kwa kuwa hatua zitakazochukuliwa ni kumfukuza kazi na sio kuhamishwa kituo cha kazi.
Mhagama, Kairuki Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama, alimshukuru Rais kutambua mchango wake katika Serikali iliyopita na kilichobaki ni kutimiza wajibu wao katika wadhifa huo.
“Rais katambua mchango wangu, nashukuru na sasa ni kuhakikisha nakwenda na kasi yake, ili tumsaidie kutimiza ndoto za wananchi na hasa kuondokana na tatizo la ajira,” alisema Mhagama.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki alisema anawiwa deni kubwa kuhakikisha anakwenda na kasi ya utendaji kazi ya Rais Magufuli.
MWANANCHI
Shirika la Umeme (TANESCO) wilayani Mwanga limepata hasara ya zaidi ya Sh151.2 milioni kwa kipindi cha miezi miwili kutokana na uharibifu wa miundombinu ya nishati hiyo.
Meneja wa Tanesco wa wilaya, Reinhild Malinjanga alisema jana kuwa hasara hiyo imetokana na matukio kumi na moja ya wizi yaliyotokea kati ya Novemba na Desemba.
Alisema mita 2,645 zimeibwa na kusababisha shirika hilo kupata hasara na kushindwa kutoa huduma bora kwa wateja. Mkuu wa wilaya, Shahib Ndemanga alisema hatawavumilia wala kuwafumbia macho watu watakaogundulika kujihusisha na wizi wa nyaya na nguzo za umeme.
Ndemanga alisema kwa kipindi alichofika wilayani hapo matukio hayo yamekuwa yakiongezeka ukilinganisha na miaka ya nyuma.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani alisema wanashikilia watu 28 wanaotuhumiwa kuhusika na wizi wa nyaya za umeme aina shaba wilayani Mwanga.
Kamanda Ngonyani alisema Desemba 8 walikamata mita 200 za nyaya za umeme zenye thamani ya Sh10.6 milioni na Desemba 9 walikamata mita 300 zenye thamani ya Sh 17.2 milioni.
MWANANCHI
Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza imeelezwa kukithiri kwa ukatili wa kijinsia, huku idadi kubwa ya watu wanaofanyiwa vitendo hivyo ni wanawake na watoto.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCu), Justin Bamanyisa alisema hayo jana wakati akitoa tathimini ya awali ya utafiti wa vitendo vya ukatili wilaya hapa.
Alisema utafiti huo unaonyesha kuwa asilimia 33 ya wanawake walio katika uhusiano wanafanyiwa vitendo hivyo.
“Nimefanya utafiti hasa vijijini na kubaini kwamba wanawake wanafanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia, lakini asilimia 21 ndiyo wanatoa taarifa katika vyombo vya dola, huku vitendo hivyo vikiwa vinatokea mara kwa mara,” alisema Bamanyisa.
Alisema kati ya watu waliowahojiwa wakati wa kufanya utafiti huo, asilimia 50 walisema wanaona ipo haja ya kuwasaidia waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia, huku asilimia 49 wakisema hakuna haja ya kuwasaidia watu hao.
“Kwa kweli hali ni mbaya, Misungwi kumekuwa na vitendo vya kikatili vingi ambavyo wanafanyiwa wanawake na watoto, tunaomba kila mmoja ajue ukatili ni dhambi,” alisema Bamanyisa.
Mratibu wa Afya wilayani hapa, Mery Joseph alisema wamekuwa wakipokea wasichana wa chini ya miaka 18 wakiwa na ujauzito. “Wanawake wenye zaidi ya miaka 20 ndiyo wanapaswa kuolewa, lakini sisi hapa tumekuwa tukipata changamoto ya kupata wasichana wa chini ya miaka 18 wakiwa na ujauzito,” alisema Joseph.
Katibu Tawala wa wilayani hapa, Elius Nyaka alisema vitendo hivyo havikubaliki na kwamba watalifuatilia suala hilo kuhakikisha wanatokomeza vitendo vya ukatili.
Mkurugenzi wa Shirika la kutetea haki za Wanawake (Kivulini), Yasin Ally alisema takwimu hizo zinatisha, kitaifa zinaonyesha utakili wa kijinsia Mwanza unafanyika kwa asilimia 43. “Hii hali inatisha, ipo haja ya kufunga mkanda na kupambana na vitendo vya ukatili.
MWANANCHI
Dalili za kufanyika kwa uchaguzi wa Rais wa Zanzibar na wawakilishi zinaonekana kuwa finyu kutokana na kutokuwapo maelekezo yoyote ya kuitaka Tume ya Uchaguzi (ZEC) kuanza kuuandaa.
Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum Jecha alitangaza kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo Oktoba 28, akisema kulikuwapo na ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za uchaguzi na kuahidi kuwa ungeitishwa uchaguzi mpya ndani ya siku 90.
Zikiwa zimepita siku 44 tangu atangaze uamuzi huo, hakuna maelekezo yoyote kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo kutoka ZEC, huku kukiwa hakuna taarifa rasmi za maendeleo ya vikao vinavyodaiwa kufanywa baina ya uongozi wa CCM na CUF, vyama vyenye upinzani mkali visiwani Zanzibar.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa ZEC, Salum Kassim Ali aliiambia Mwananchi jana kuwa hawajapata maagizo yoyote ya kutakiwa kuanza maandalizi ya uchaguzi.
Ingawa hakuwa tayati kuzungumzia suala hilo kwa kina, Kassim Ali alisema wakati akijibu maswali ya gazeti hili kuwa hakuna kinachoendelea hadi sasa.
“Wewe unauliza kununua pampasi wakati hujui mtoto atazaliwa lini? Badala ya kuuliza uchaguzi upo au haupo unauliza vitu vingine?” alihoji Kassim Ali alipoulizwa na gazeti hili uchaguzi wa marudio utafanyika lini”. alihoji.
Maalim Seif Sharrif Hamad alitangaza kuwa ameshinda uchaguzi huo na kuitaka ZEC imtangaze mshindi. Kitendo hicho pamoja na vurugu ambazo Jecha alidai zilifanyika ndani ya ZEC na wakati wa kuandikisha wapigakura, ndvyo vilivyomfanya atangaze kufuta uchaguzi, uamuzi ambao unapingwa na CUF inayodai kuwa mwenyekiti huyo hana mamlaka ya kufuta uchaguzi na kwamba alichukua uamuzi huo bila ya kushirikisha wajumbe wenzake.
Kuhusu taarifa kwamba Jecha amekuwa haonekani ofisini, mkurugenzi huyo wa uchaguzi wa ZEC alisema taarifa hizo si za kweli na kwamba kama kuna taarifa zimeenea kuhusu jambo hilo, ziandikwe hivyo hivyo. “Aliyekuambia hayupo ofisini ni nani? Andika hayo hayo ya mitaani,” alisema.
Akizungumzia suala hilo la tarehe ya uchaguzi wa marudio, ofisa uhusiano wa ZEC, Idrissa Jecha alisema kuwa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar haizungumzii uchaguzi wa marudio bali tarehe ya kupiga kura baada ya wagombea kuteuliwa na Tume.