MTANZANIA
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Bitun Msangi, ametangaza kufuta ziara za mafunzo kwa madiwani wa halmashauri hiyo na badala yake amewataka waende kujifunza vijijini.
Onyo hilo amelitoa juzi, wilayani hapa alipokuwa akizungumza na wananchi wa vijiji vya Mseta, Manhweta na Mseta Bondeni Kata ya Chamkoroma, wakati akikabidhi vyeti na kombe kwa wananchi waliofanya vizuri katika utunzaji wa mazingira ikiwamo ujengaji wa vyoo vya kisasa .
Alisema badala ya kufanya ziara hizo katika halmashauri nyingine, watatakiwa kwenda kujifunza katika vijiji vyao ambako kuna changamoto nyingi na watajadiliana jinsi ya kuzitatua.
“Mfano ulio hai ni hapa kwenye kata hii ambapo kama madiwani wakiamua kuja kujifunza wanaweza wakapata elimu ya kuwaelimisha wananchi wa kata nyingine ambazo mazingira ya usafi bado ni dhaifu,” alisema DC Msangi.
Alisema wananchi wa vijiji vya kata hiyo wameweza kunufaika na mpango wa vyoo vya kisasa kwa asilimia 100 kwa kila kaya kuwa na choo cha kisasa, ikiwemo kibuyu chirizi, shimo la taka na kichanja cha kuwekea vyombo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mipango wa Mradi kutoka shirika la UMATA, Nyomzobe Malimi, alisema vijiji hivyo vimefanikiwa katika ujenzi wa vyoo ikiwemo uwekaji wa vibuyu mchirizo kwa aslimia 100 tofauti na vijiji vingine vinavyofadhiliwa.
Alisema mradi huo umewekewa mikakati ya miaka mitano kuhakikisha unawawezesha zaidi ya watu milioni moja katika wilaya tatu wanafikiwa.
MTANZANIA
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa amelitaka Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es salaam (DAWASCO), kufikisha maji kwa wateja milioni moja hadi kufikia Juni mwaka ujao.
Mbarawa alimtaka Mkurugenzi wa Dawasco, Cyprian Luhemeja kuongeza makadirio waliyokuwa wamejiwekea kwa kuongeza wateja kutoka 148,000 waliopo kwenye bili hadi kufikia milioni moja.
Profesa Mbarawa aliyasema hayo jana katika ziara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo mwishoni mwa wiki ambapo alisema uzalishaji wa maji katika Jiji la Dar es salaam unategemea mitambo ya Ruvu Juu, Ruvu Chini pamoja na ule wa Mtoni.
“Naamini pindi tutakapofanya mazungumzo ya kina tutafikisha kiasi hicho cha wateja hiyo Juni mwakani na hilo mtalipima kwenye tathimini tutakapokutana Februari,” alisema Profesa Mbarawa.
Katika hatua nyingine waziri huyo alitoa wito kwa Dawasco kuanza mchakato wa kutumia mita za mfumo wa kulipia kabla kama inavyofanyika kwa simu na umeme.
“Njia hii naamini itasaidia kuwabana wakwepaji wa kulipa na hivyo kusaidia Dawasco kujipatia mapato ya kutosha,” alisema Mbarawa.
Alitoa wito kwa Mkurugenzi wa Dawasa, Archard Mutalemwa kuhakikisha wanaweka miundombinu bora ili kuokoa upotevu wa maji ili kuboresha huduma ya kuongezeka kwa wateja walio kwenye mfumo wa bili watakaofikia milioni moja.
MTANZANIA
Mwanamke mmoja mkazi wa Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Kulwa Shasumuni, amemwunguza mkono wa kushoto mtoto wake Hassani Faustino mwenye miaka 9 kwa kile alichodai ameshindwa kuanika shuka zake alizokojolea kitandani.
Taarifa za kuunguzwa mkono kwa mtoto huyo zilitolewa na majirani, ambao hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini kwa kuhofia usalama wao.
“Mama huyo amekuwa akimfanyia vitendo vya kikatili mwanae mara nyingi hata tunapomzuia amekuwa akitukaripia na kutuambia hayatuhusu masuala ya mtoto wake,” alisema mmoja wa majirani hao.
Alisema katika tukio la juzi, walisikia sauti ya mtoto Hassan akilalamika huku akisema. “mama nakufa” ndipo walipochungulia dirishani na kumwona mama huyo akiwa amemweka mtoto wake kwenye moto wa kuni hali iliyowafanya wapige kelele na hatimaye kumwachia.
Kutokana na tukio hilo mwanamke huyo baada ya kumfanyia ukatili mtoto huyo alimpeleka katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga, ambapo alilazwa wodi namba 8 huku akiendelea kupatiwa matibabu kutokana na majeraha ya moto.
Akizungumza na mwanadishi wa habari hizi, mtoto Hassan Faustino, akiwa wodini alisema alikojoa kitandani kwa bahati mbaya, lakini mama yake alipogundua kuwa amekojoa alimtaka aanike shuka jambo ambalo alisahau kulifanya.
“Nilikojoa kitandani kwa bahati mbaya na mama aliniambia nianike shuka lakini nilisahau ilipofika mchana aliniita ndani na kuanza kuniadhibu na baada ya muda aliniunguza mkono wa kushoto kwa moto,” alisema mtoto huyo.
Mtoto huyo alisema baada ya kuhisi maumivu makali ya moto alipiga kelele ndipo alipomwachia ingawa alikuwa amepoteza fahamu.
Kutokana na tukio hilo, mwandishi wa habari hizi, alimtafuta mama mzazi wa mtoto huyo, Kulwa Shasumuni, ambaye alikiri kufanya kitendo hicho.
“Ni kweli nilimwunguza mtoto wangu na sikutarajia kuwa hali ingeweza kuwa hivi ila ni hasira tu zilipanda, awali nilimwambia achukue majivu lakini kumbe yalikuwa na moto,” alisema mama huyo.
Akizungumzia hali ya mtoto huyo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Igunga, Abdallah Ombeni, alithibitisha kumpokea mtoto huyo akiwa na jeraha la moto katika mkono wake wa kushoto.
Hata hivyo alisema pamoja na kuendelea na matibabu bado hali ya mtoto huyo si nzuri.
Kutokana na ukatili huo, Diwani wa Kata ya Igunga, Charles Bomani (CCM), amelaani kitendo hicho na kuuomba uongozi wa Serikali ya Wilaya kufanya juhudi za kuokoa maisha ya mtoto huyo ambaye bado amelazwa hospitalini hapo.
Boman, alisema anashangazwa na hatua ya Jeshi la Polisi kushindwa kumchukulia hatua za kisheria mwanamke huyo hadi sasa.
MWANANCHI
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema tatizo la uzalishaji umeme kwenye mabwawa ni uchakavu wa mitambo baada ya kufanya ziara na naibu wake, Dk Menard Kalemani kwenye vituo vya New Pangani na Hale mkoani Tanga.
Profesa Muhongo, ambaye amerejeshwa kwenye wizara hiyo baada ya kulazimika kujiuzulu mapema mwaka jana kutokana na kashfa ya uchotwaji fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow, alitoa kauli hiyo baada ya kukutana na wakuu wa Shirika la Umeme (TANESCO) na baadaye kutembelea vituo hivyo vinavyozalisha umeme wa maji.
“Tumejigawa,” alisema Profesa Muhongo akizungumzia mpango kazi wake na Dk Kalemani jana. “Naibu wangu yeye kesho (leo) atatembelea mtambo wa Kinyerezi jijini Dar es Salaam.
Mimi natembelea vituo sanjari na kuangalia hali ya mabwawa.” Alisema ameamua kufanya ziara hiyo ya wiki moja katika vituo vyote vinavyozalisha umeme na kujua hali ya umeme nchini.
Alisema hataki kuingiza siasa katika masuala ya umeme na kwamba akisema mtambo fulani utazalisha megawati kadhaa, kuwe na kweli na si kuwadanganya Watanzania. Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, Rais John Magufuli aliituhumu Tanesco kuwa inamuhujumu kwa kukata umeme, na kutaka viongozi wajiandae kuondoka.
Na katika hotuba yake ya kuzindua Bunge mwezi uliopita, Dk Magufuli alisema kuna njama za kuruhusu maji kutoka Bwawa la Mtera ili wasingizie mitambo haiwezi kuzalisha umeme kwa kuwa hakuna maji, na hivyo kutengeneza soko wafanyabiashara kuuza jenereta.
Lakini jana, Profesa Muhongo alisema matatizo ya umeme yanasababishwa na mambo mawili.
Alisema sababu ya kwanza ni uchakavu mitambo na ya pili ni wananchi kuchepusha mkondo wa maji unaoelekea kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme.
“Tumekuwa tukishikana mashati, tukigombana na kutuhumiana huko nje, lakini ukweli ni huu; baadhi ya mitambo imechakaa na inahitaji kufanyiwa ukarabati,” alisema Profesa Muhongo akitofautiana na tuhuma za Rais Magufuli.
Alisema ni wakati mwafaka kwa Taifa kuacha kutegemea vyanzo vya umeme wa maji, badala yake lijaribu kutumia vyanzo vingine kama umeme wa makaa ya mawe.
Alisema mwezi ujao watafufua mashine ya pili ya kituo cha Hale, baada ya kupata mkopo kutoka Serikali ya Sweden, hatua ambayo itawezesha kituo hicho kuzalisha umeme kwa ufanisi.
Mramba alisema mashine hiyo ya pili ikianza kufanya kazi, itazalisha jumla ya megawati 21 zitakazoingizwa gridi ya taifa.
Kuhusu kuchepusha maji ya mabwawa ya uzalishaji umeme, Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Esterina Kilasi alimuahidi Profesa Muhongo kulishughulikia jambo hilo ili kuhakikisha maji hayo yanatumika kama yalivyokusudiwa.
MWANANCHI
Mbunge wa jimbo la Kibamba, John Mnyika amekosoa uamuzi wa Rais John Magufuli wa kuhamishia wizara inayohusu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) chini ya ofisi yake, akidai kitendo hicho kimelenga kuvibana vyama vya upinzani ambavyo vimeshinda halmashauri nyingi nchini.
Mnyika aliyasema hayo jana wakati akitoa shukrani zake kwa wananchi wa Kata ya Salanga iliyopo Kimara kwa kumchagua kuwa mbunge wao.
Alieleza kushangazwa na mabadiliko yanayofanywa na Dk Magufuli tangu alipoingia madarakani. Mbunge huyo alisema Chadema na vyama vingine vya upinzani vimeshinda katika uchaguzi wa nafasi za umeya na uenyekiti katika halmashauri mbalimbali nchini, jambo hilo limemfanya Rais kuiweka Tamisemi chini yake ili kupunguza uhuru wa halmashauri zinazoongozwa na upinzani katika kuleta maendeleo.
“Katika halmashauri za Dar es Salaam bado tunavutana, wanaleta madiwani wa viti maalumu kutoka Zanzibar kuja kupiga kura huku bara. Tunawaambia hatutakubali kwa sababu Chadema na Ukawa inaongoza kwa viti vingi vya udiwani, lazima tuongoze jiji hili,” alisema.
Myika aliongeza kuwa “Rais Magufuli amefanya kama alivyofanya Benjamini Mkapa wakati wa utawala wake kwa kutaka kutawala kibabe.
Hatafika mbali kwa sababu ameshindwa kujenga mifumo thabiti, badala yake amebaki kuhimiza usafi wa siku moja,” alisema.
Kiongozi huyo ambaye pia ni naibu katibu mkuu wa Chadema, alimtaka Rais Magufuli kujenga misingi ambayo itajiendesha yenyewe bila uwepo wake.
Alimtaka pia kuweka msimamo thabiti wa kutengeneza Katiba mpya kwa kufanyia kazi maoni ya wananchi.
MWANANCHI
Wamiliki wa viwanja katika mji wa Moshi waliokuwa wamevihodhi kwa miaka mingi bila kuviendeleza, wameanza kuviuza kwa kasi baada ya Serikali kuanza mchakato wa kuvitwaa.
Hata hivyo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imewaonya wanaouza viwanja hivyo kuhakikisha wanalipa kodi kwa mujibu wa sheria vinginevyo watashtakiwa.
Meneja wa TRA Mkoa Kilimanjaro, Abdul Mapembe alitia taarifa hiyo juzi kuwa akisema baadhi ya wamiliki wanauza viwanja hivyo ili kukwepa mchakato unaoendelea wa kuwanyang’anya.
Kwa mujibu wa meneja huyo, wiki ijayo watamwandikia barua mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi ili awape orodha ya viwanja na wamiliki wake, wafuatilie kama kodi stahiki zililipwa baada ya mauzo.
Viwanja vya pembezoni ya mji vimekuwa vikiuzwa kati ya Sh15 milioni hadi Sh50 milioni, huku vilivyopo maeneo ya kibiashara vikiuzwa kati ya Sh100 milioni na Sh200 milioni.
Hata hivyo, imebainika baadhi ya wauzaji na wanunuzi wamekuwa wakila njama na baadhi ya mawakili wasio waaminifu ambao huandika mikataba miwili, moja ukionyesha mauzo halisi na mwingine ukionyesha bei ndogo ili kukwepa kodi.
Gazeti hili limefanikiwa kupata mkataba wa ununuzi wa kiwanja kimoja cha katikati ya mji ukionyesha kilinunuliwa chini ya Sh10 milioni lakini taarifa nyingine zinadai kiwanja hicho kiliuzwa kwa zaidi ya bei hiyo.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini kuwa baadhi ya viwanja havijaendelezwa kwa zaidi ya miaka 20 na vinamilikiwa na vigogo wa kisiasa na wafanyabiashara wazito.
Wiki iliyopita, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, ilitangaza kuanza kufanya tathmini upya ili kubaini idadi ya viwanja vya makazi na biashara vinavyotakiwa kufutwa baada ya wamiliki wake kushindwa kuviendeleza.
Manispaa ya Moshi ina viwanja zaidi ya 200 ambavyo orodha yake ilipelekwa kwa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete ili vifutwe na kugawiwa upya lakini hadi anastaafu hakuvifuta viwanja hivyo.
Kaimu mkurugenzi wa manispaa hiyo, Jeshi Lupembe, alisema baada ya kukamilika kwa tathmini hiyo mpya,orodha ya viwanja hivyo itapelekwa kwa Rais John Magufuli ili wamiliki wanyang’anywe.
Kauli ya Lupembe imekuja siku chache baada ya Rais Magufuli kulihutubia Bunge na kueleza namna viwanja vingi vilivyohodhiwa bila kuendelezwa na kusisitiza kuwa Serikali itavitwa na kuvigawa upya.
MWANANCHI
Hatua ya Rais John Magufuli kuteua na kuwaapisha mawaziri watatu kabla ya kuapishwa kuwa wabunge, imeibua utata huku wanasheria wakihoji jinsi gani watafanya kazi za Kamati za Bunge kabla ya Februari wakati chombo hicho cha kutunga sheria kitakapoanza shughuli zake.
Kwa mujibu wa ibara ya 66 (1) ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano, Rais ana mamlaka ya kuteua wabunge wasiozidi kumi ambao anaamini wanaweza kumsaidia katika utekelezaji wa majukumu yake. Na ibara ya 55 (4) inamuelekeza Rais kuteua mawaziri kutoka miongoni mwa wabunge.
Kwa kutumia mamlaka hayo, Alhamisi iliyopita Rais Magufuli aliwateua makada watatu kuwa wabunge na hapo hapo kutangaza kuwateua kuwa mawaziri na kisha kuwaapisha juzi kutumikia wadhifa huo.
Mawaziri hao ni Profesa Makame Mbarawa ambaye ameteuliwa kuwa Wazira wa Maji na Umwagiliaji, Dk Abdallah Possi (Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri MkuuSera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), na Balozi Augustine Mahiga ambaye anakuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.
Kuteuliwa kwao kunafanya jumla ya wabunge walioteuliwa na Rais hadi sasa kuwa wanne baada ya kumteua Dk Tulia Ackson mwezi uliopita kabla ya naibu mwanasheria mkuu huyo wa zamani kugombea nafasi ya Naibu Spika wa Bunge.
Hata hivyo, Dk Tulia aliapishwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai kabla ya kugombea nafasi ya unaibu spika na kushinda na kuapishwa kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yake.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema hapo kuna tatizo la kisheria kwa kuwa mawaziri wote huteuliwa kutokana na nafasi zao za ubunge na kwamba kiapo cha ubunge ndiyo kinamtambulisha mbunge kabla ya kutambuliwa kuwa waziri.
Lissu alisema endapo shughuli za Kamati za Bunge za Kudumu zitaanza vikao vyake siku chache zijazo kabla ya mkutano wa Bunge, waziri anayehusika kwenye kamati yake hatatambuliwa licha ya kuwa kiongozi wa Serikali anayetakiwa kujibu hoja za wizara yake.
“Kwa mfano, Balozi Mahiga atahitajika kuwa mjumbe wa Wizara ya Mambo ya Nje, sasa ataingiaje bila kuwa na kiapo cha kuwa mbunge? Je, hawataenda kushiriki? Kama hawataenda, itakuwaje kwa sababu hata kanuni zinasema huwezi kutambuliwa wala kufanya kazi za kibunge bila kula kiapo,” alisema Lissu.
Kauli ya Lissu iliungwa mkono na mwenyekiti wa zamani wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji Amir Manento kuwa waziri aliyeapishwa bila kula kiapo cha Bunge hawezi kutambuliwa na Bunge hilo. Jaji Manento alisema Spika hatakuwa na uwezo wa kumpangia kazi zozote za kibunge hadi atakapokula kiapo.
Kwa hiyo alisema mawaziri walioapishwa kabla ya kiapo hicho hawatambuliwi na Bunge.
“Inawezekana Rais alishawateua mapema katika kipindi cha ukimya wake wa mwezi mmoja na kuwasiliana na ofisi za Bunge, bila kupata taarifa hiyo, yaani ofisi ya Bunge ikawatambua tu licha ya kutotambuliwa kwa kiapo, lakini bado kuna utata katika suala hilo la kiapo, sawa na mchezo wa yai na kifaranga nani aliyeanza,” alisema Jaji Manento.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema mawaziri hao hawawezi kujihusisha na shughuli zozote za Bunge bila kula kiapo. Alisema mawaziri hao watakuwa na nafasi ya kufanya shughuli zote zinazowahusu kama mawaziri, lakini hawatakuwa na nafasi ya kupewa majukumu ya kibunge kabla ya kula kiapo.
“Jambo la pili, mawaziri hao wanaweza kuwa na nafasi ya kushiriki kwenye Kamati za Bunge lakini hawatakuwa na nafasi ya kupiga kura kama kanuni za Bunge zinavyobainisha.
Anaweza kuingia na kusikiliza au kufuatilia mjadala tu kwenye kamati hizo,” alisema huku akitoa mfano kuwa jambo hilo si mara ya kwanza kutokea.
” Katika ufafanuzi huo, Dk Kashililah alisema mawaziri hao hawataweza kushiriki mjadala ya miswada au hoja zilizowasilishwa ndani ya kamati hizo. “Na ndiyo maana Bunge litakapoanza tu, wanaanza kula kiapo kwanza kwa sababu kanuni za Bunge zinaagiza hivyo,” alisema.
HABARILEO
Wazazi wa wakazi wa Kijiji cha Kamsisi wilayani Mlele katika Mkoa wa Katavi wamekubali kuuzika mwili wa mtoto wao Moshi Salehe mwenye miaka 17 anayedaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi za moto na askari wa wanyamapori wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).
Mwili wa marehemu huyo ulilazimika kuhifadhiwa katika chumba cha maiti katika Hospitali ya Mkoa wa Katavi kwa siku tano baada ya jamii wa wafugaji wakiwemo wazazi wa marehemu kukataa kuufanyia maziko mwili huo.
Jamii hiyo ya wafugaji na wazazi wa marehemu walidai kuwa watakuwa tayari kuufanyia maziko mwili wa marehemu huyo iwapo watuhumiwa wote watatiwa nguvuni ili sheria ichukue mkondo wake.
Akisimulia mkasa huo, baba mzazi wa marehemu, Samweli Daki alisema mtoto wake huyo aliuawa Desemba 6, mwaka huu saa kumi jioni katika eneo la Hifadhi la Kanono wilayani Mlele.
“Nakumbuka siku hiyo ya tukio Moshi akiwa na watoto wangu watano walikuwa wakiswaga kundi la ng’ombe zetu kutoka Kata ya Mpanda ndogo wilayani Mpanda wakizihamishia kijijini Kamsisi wilayani Mlele ambako niko tunakoishi,” alieleza baba wa marehemu.
Alieleza kuwa watoto wake hao walipofika eneo hilo la Kanono wakiwa wanasagwa ng’ombe ndipo walipokutana uso kwa ana kwa ana askari wa wanyamapori waliokuwa katika gari lao la doria.
“Ndipo askari hao wakiwa na silaha walifyatua risasi na kumjeruhi vibaya mwanangu pajani ….. watoto wangu wengine walitimua mbio kusalimisha maisha yao wote ni wazima hakuna aliyejeruhiwa,” alieleza.
Akifafanua aliongeza kuwa baada ya askari hao wa wanyamapori kumpiga risasi kijana huyo waliondoka wakimwacha pekee yake porini bila msaada wowote ule ambapo alipoteza damu nyingi hadi wao walipopata taarifa na kwenda kumchukua.
Naye Mwenyekiti wa Wafugaji Mkoa wa Katavi, Musa Kabuja na Mwenyekiti wa Wafugaji Wilaya ya Mlele, Zezengela Ruhagaje walisisitiza kuwa wahusika wote wasakwe na kutiwa nguvuni ili sheria ichukue mkondo wake kwa unyama waliomfanyia mtoto huo.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Rashid Mohamed alikiri mauaji hayo, akisema mtoto huyo aliuawa kwa kupigwa risasi na askari wa wanyamapori waliokuwa wakifanya doria katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi. Bila kutaja majina, alisema wanawashikilia askari wa wanyamapori wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji hayo.
HABARILEO
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imefafanua kwamba geti namba tano katika Bandari ya Dar es Salaam ni maalumu kupitisha kontena zinazokwenda katika bandari kavu na si eneo la kutoza au kukagua kodi.
Meneja Mawasiliano wa TPA, Janeth Ruzangi alisema hayo kupitia taarifa kwa vyombo vya habari aliyoitoa jana.
Alisema, kwa mujibu wa utaratibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kontena zote za waagizaji wa ndani ndizo hutozwa kodi na ni lazima zipelekwe bandari kavu moja kwa moja kutoka bandarini. Kodi na tathmini zote hufanywa baada ya kontena hizo kufika bandari kavu.
“Kwa mujibu wa taratibu za forodha, kontena zote zinazokwenda kwenye bandari kavu zinapotoka bandarini huwa hazijalipiwa hata kodi ya custom escort,” Runzagi alisema na kuongeza kwamba kontena za waagizaji wa nchi jirani hazitozwi kodi.
“Makontena haya hutozwa tozo za bandari kama ushuru kwa huduma na kazi za bandari wakati wa kuupokea mzigo huo,” alisisitiza Taarifa hiyo imetolewa baada ya baadhi ya vyombo vya habari kudai geti hilo linatumiwa na wakwepa kodi.
“Kwa hiyo, si sahihi kusema kuwa geti namba tano ni maalum kwa makontena yanayokwepa kodi. Kwa utaratibu, geti hilo ni maalumu kupitisha makontena yanayokwenda bandari kavu,” alisema.
HABARILEO
Wizara ya Elimu, Sayansi na Ufundi imetoa waraka wa elimu kuhusu elimumsingi bila malipo na kutoa orodha ya shule za msingi 11 za Serikali ambazo hazihusiki na utoaji wa elimu bure uliotangazwa na Rais John Magufuli. Elimumsingi inajumuisha elimu ya awali, ya msingi na sekondari ambayo itaanza Januari mwakani.
Katika Waraka Elimu Namba 6 wa Mwaka 2015 kuhusu utekelezaji wa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari, wizara hiyo imetaja shule hizo kuwa ni Shule ya Msingi Olympio (Dar es Salaam); Shule ya Msingi Diamond (Dar es Salaam); Shule ya Msingi Oysterbay (Dar es Salaam); Shule ya Msingi Iringa (Iringa) na Shule ya Msingi Mkapa (Mbeya).
Nyingine ni Shule ya Msingi Angaza (Mbeya); Shule ya Msingi Nuru (Mbeya); Shule ya Msingi Lupilisi (Ruvuma); Shule ya Msingi Tanga (Tanga); Shule ya Msingi Arusha (Arusha) na Shule ya Msingi Kisimani iliyoko mkoani Arusha.
Wizara hiyo pia imesema waraka huo hauzihusu shule zinazomilikiwa na mashirika ya umma ama taasisi za umma ambazo zinaendeshwa kwa taratibu sawa na shule za binafsi. Katika waraka huo, wizara hiyo imetoa majukumu yanayotakiwa kufanywa na Wizara hiyo, Tamisemi, wakurugenzi wa manispaa na halmashauri ya wilaya, wakuu wa shule, bodi za shule, wazazi na wananchi.
Majukumu ya wazazi na walezi Kuanzia Januari, wazazi wanatakiwa tu kununua sare za shule na michezo, vifaa vya kujifunzia vikiwemo madaftari na kalamu, na chakula kwa wanafunzi wa kutwa na kugharimia matibabu kwa watoto wao.
Wanatakiwa pia kulipia nauli ya kwenda shule na kurudi kwa wanafunzi wa kutwa na wanafunzi wa bweni wakati wa likizo; kununua magodoro, shuka, vifaa vya usafi binafsi kwa wanafunzi wanaosoma shule za bweni na wanaoishi katika hosteli zinazotumiwa na serikali; na kukemea na kutoa taarifa kuhusu mienendo inayokwenda kinyume na elimumsingi bila malipo.
Wazazi na wananchi wengine pia wanatakiwa kuendelea kujitolea nguvukazi na mali ili kuleta ustawi na maendeleo ya shule zilizoko ndani ya jamii.
Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Katika waraka huo, Wizara ina jukumu la kutenga fedha za kugharimia utayarishaji na uendeshaji wa mitihani ya kitaifa kulingana na idadi ya wanafunzi; kutenga fedha kwa ajili ya Uthibiti Ubora wa Shule na kutenga fedha za kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utoaji wa elimumsingi bila malipo na kuchukua hatua stahiki pale inapobidi.
Inachotakiwa kufanya Tamisemi Kwa upande wa Tamisemi, waraka huo unaielekeza wizara hiyo kutoa miongozo ya matumizi ya fedha za umma kwa wakuu wa shule, kuratibu uandaaji wa mipango na bajeti ili kupata mipango na bajeti ya taifa kila mwaka inayozingatia mahitaji halisi ya elimumsingi bila malipo.
Pia Tamisemi inatakiwa kufanya ukaguzi wa ndani, ufuatiliaji na tathmini za mara kwa mara ili kuhakikisha elimumsingi bila malipo inatolewa kwa ufanisi na viwango vya ubora inavyostahili.
Kuratibu utoaji mipango na bajeti za ruzuku ya uendeshaji wa shule ikiwemo ulinzi, umeme, maji na ununuzi wa chaki na karatasi pamoja na vifaa vingine vya kufundishia na kujifunzia.
Kutenga na kutuma fedha shuleni kwa ajili ya uendeshaji na usimamizi wa mitihani na majaribio mbalimbali shuleni ikiwemo tathmini endelezi, kununua vitabu, kemikali na vifaa vya maabara, samani yakiwemo madawati, vifaa vya michezo, matengenezo ya mashine na mitambo pamoja na kujenga na kukarabati miundombinu ya shule.
Kutenga na kutuma fedha shuleni za kugharimia wanafunzi wenye mahitaji maalumu waliopo kwenye shule na vitengo vya elimu maalumu kwa kuwapatia chakula yaani mlo mmoja kwa wanafunzi wa kutwa na milo mitatu kwa wanafunzi wa bweni pamoja na vifaa na visaidizi.
Wakuu wa shule Waraka huo unawataka wakuu wa shule kuwapa maelekezo wazazi kuhusu aina ya vifaa vinavyohitajika mfano rangi ya kitambaa cha sare ya shule, sare za michezo, idadi na aina ya madaftari watakayotumia wanafunzi ili wazazi wanunue wenyewe.
Pia wanatakiwa kusimamia na kuhakikisha fedha inayotolewa na Serikali inatumika kama ilivyokusudiwa kulingana na taratibu za fedha za Serikali na kutoa takwimu na taarifa sahihi za idadi ya wanafunzi na mahitaji mengine ya shule.
Unataka kutumiwa MSG za habari zote kubwa kutoka kwa Millard Ayo? ukiwa na line ya tiGO andika ‘AYO’ tuma kwenda 15510, msg utayotumiwa jibu OK ili uanze kupokea matukio yote kwa sms, pia ungana na Millard Ayo kwenyeTwitter,FB, Instagram na YouTUBE kwa kubonyeza hapa >>>INSTAGRAM TWITTER FB YOUTUBE