NIPASHE
Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini mkoani Mara, Esther Bulaya, anatarajiwa kutinga Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza leo baada ya kufunguliwa kesi ya madai ya kupinga matokeo yaliyompa ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Kesi hiyo ya madai iliyofunguliwa Novemba 19, mwaka huu na Magambo Masato na wenzake 30, inapinga matokeo yaliyompa ushindi Bulaya na wenzake 20 pamoja na mkurugenzi wa Wilaya ya Bunda ambaye alikuwa Msimamizi wa Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu.
Katika matangazo yaliyowekwa katika ubao wa matangazo ya Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, waomba maombi wanadai upatikanaji wa ubunge wa Bulaya haukuwa halali kutokana na kukiukwa kwa baadhi ya mambo.
Taarifa hiyo ilidai msimamizi wa uchaguzi hakutakiwa kumtangaza Bulaya kuwa mbunge halali wa jimbo hilo kutokana na kwenda kinyume cha sheria pamoja na kanuni za uchaguzi huo.
Kesi hiyo ya madai ni moja ya kesi zilizofunguliwa kupinga matokeo ya ushindi wa baadhi ya wabunge katika majimbo mbalimbali nchini tangu Uchaguzi Mkuu ufanyike Oktoba 25, mwaka huu.
NIPASHE
Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, imeingilia kati mgogoro wa Kiwanda cha Nguo cha Urafiki kwa kuwasimamisha kazi Meneja Mkuu wa kiwanda hicho, Nassoro Baraza na Naibu Meneja Mkuu, Samweli Swai ili kupisha uchunguzi dhidi yao ufanyike na endapo watabainika kuwa ni chanzo cha mgogoro huo watachukuliwa hatua za kisheria.
Aidha, serikali imetoa miezi sita kwa kiwanda hicho kiwe kimewalipa wafanyakazi madai yao mbalimbali sambamba na kuanza kulipa nyongeza ya mishahara wanayodai kama sehemu muhimu ya kumaliza kabisa mgogoro huo.
Akitoa agizo hilo jana, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Uledy Mussa, alisema serikali imeona ni vema kufanya maamuzi magumu kwa mtu mmoja au wawili ili kunusuru uwapo wa nguvu kazi nyingi hasa kwa watu wanaohitaji kutimiziwa haki zao za msingi.
Uledy pia alikitaka kiwanda hicho kuwalipa wafanyakazi wote kiwango kipya cha mishahara yao ya Sh. 150,000 ifikapo mwishoni mwa Desemba mwaka huu, kama wizara ya kazi na ajira inavyosema kupitia mwongozo wa mishahara ya wafanyakazi nchi.
Licha ya hayo, pia Uledy alisema serikali ipo katika hutua za mwisho kutafuta muwekazaji mpya katika kiwanda hicho ambaye atahakikisha analinda maslahi ya wafanyakazi na taifa kwa ujumla.
“Hatua hiyo ni muendelezo aliokuwa akifanya aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Marehemu Dk. Abdallah Kigoda,”alisema Uledy.
Pamoja na madai mengine, wafanyakazi hao pia wanahitaji kujua hatma ya wastaafu kulipwa Sh. 200,000 mara baada ya kustaafu, jambo ambalo Uledy alihitaji muda tena kabla ya kutoa jibu kamili kwa madai kwamba hakuwa na uwezo wa kulitolea ufafanuzi kwa wakati huo.
Katika hatua nyingine wafanyakazi wa kiwandani hicho wamemtaka Katibu wa Chama cha Wafanyakazi (TUICO), Florian Makero, kujihuzulu wadhifa huo kwa kile kunachodai kuwa ameshindwa kuwatetea katika kutafuta haki zao kuwa upande wa uongozi.
NIPASHE
Mbunge wa Jimbo la Kibamba, John Mnyika, ameomba ripoti za kamati za uchunguzi zilizoundwa na mawaziri wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe na Samuel Sitta, kuhusu Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ziwekwe hadharani.
Amesema kuwekwa hadharani kwa ripoti hizo kutaondoa usiri na kusaidia kubaini ufisadi uliokithiri katika mamlaka hiyo ili hatua za kuwasimamisha vigogo wa TPA na wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ziwe na mafanikio.
Mnyika ambaye amekua kimya kwa muda mrefu tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu Oktoba 25, mwaka huu, alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari, jijini la Dar es Salaam jana.
“Kama kweli serikali ya awamu ya tano ina lengo la kufichua mafisadi, inapaswa kuweka wazi ripoti mbalimbali za uchunguzi ili ziwe dira ya kujua kiini cha matatizo kujitokeza katika mamlaka hiyo,” alisema na kuongeza:
“Nafahamu yapo mambo mazuri kwa nchi yaliyonainishwa, lakini kutokana na ripoti hizo kuwa siri hakuna anayejua huku fedha za walipa kodi zikiwa zimetumika bila mafanikio. Dawa ya jipu siyo kulitumbua bali ni kulipasua ili kiini cha ndani kitoke, ukikiacha jipu linaanza kuvimba upya tena linakuwa hatari zaidi.”
Aidha, Mnyika alisema wakati wa kampeni, Rais Dk. John Magufuli, aliahidi kutatua tatizo la maji na kumtaka kutekeleza ahadi hiyo kwa kutembelea mradi wa maji wa Ruvu Juu ili apasuwe majipu yaliyoiva.
Alisema iwapo Rais atatembelea mtambo huo atabaini ufisadi unaokwamisha ulazaji wa mabomba ya Mchina yasitoe maji, pampu za maji kuharibika mara kwa mara na mradi wa maji kutoka Mlandizi hadi Kimara kukwama wakati fedha zimetolewa.
“Wizara ya maji ilisema bungeni kuwa ulazaji wa mabomba ya maji ulifikia asilimia 70 na ifikapo Agosti, mwaka huu mabomba yangetoa maji lakini bado wananchi wanaendelea kuteseka,” alisema.
Mnyika alisema serikali ya awamu ya tano ikishindwa kutoa ufumbuzi wa hoja hizo mbili, ataziwakilisha bungeni katika kikao cha Bunge kinachotarajia kufanyika Januari mwakani.
NIPASHE
Taharuki imetanda kwa wamiliki wa shule nchini baada ya kupokea waraka unaowakataza kuongeza ada kwa shule zisizo za serikali katika mwaka wa masomo unaoanza mwezi ujao.
Kwa mujibu wa tangazo hilo lililotolewa Desemba 3, mwaka huu na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Sifuni Mchome, shule zinatakiwa kutoongeza ada mwaka wa masomo 2016 hadi zitakapopata maelekezo kutoka kwa Kamishna wa Elimu.
Tangazo hilo pia lilieleza kuwa kwa shule ambazo zimeongeza ada bila kupata kibali cha Wizara, kamwe hazitatambuliwa kwani ni batili na kwamba zimefutwa kwavile hazina nguvu kisheria.
Kadhalika, tangazo hilo lilieleza kuwa ada zote kwa shule zisizo za serikali zitabaki kama zilivyoidhishwa na kamishna ambapo waraka wa Elimu Na. 4 wa mwaka 2008 umeelekeza ada zinazotozwa shule za msingi na sekondari pamoja na zisizo za serikali.
Ada iliyowekwa kwa shule za kutwa zisizo za serikali ni Sh. 150,000 na shule za bweni Sh. 380,000 kwa mwaka kila mwanafunzi.
Mkuu wa Shule ya Mtakatifu Florence ya Mikocheni, Willison Mwabwuke, alisema wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa hiyo kutoka kwa serikali.
Alisema wao hutumia gharama kubwa kuendesha shule hiyo ikiwamo kuwalipa mishahara walimu na kununua vitendea kazi.
Alisema hutoza ada Sh. 2,055,000 kwa wanafunzi wa kutwa na Sh. 2,970,000 kwa wanafunzi wa bweni.
“Tunagharamia usafiri, chakula, ulinzi, maji na usafi pia tunawalipa walimu mishahara mikubwa, sidhani kama serikali watakuwa wanatutendea haki,” alisema Mwabwuke.
Alisema serikali inatakiwa kuboresha huduma katika shule za umma na siyo kuzibana shule binafsi.
Aliongeza kuwa ni mapema kwa serikali kuanzisha utaratibu huo.
Naye mmiliki wa Shule za Green Acres, Julian Bujugo, alisema suala hilo haliwezekani kwa sababu wahusika waliopanga kiwango hicho hawakuangalia gharama wanazozitumia shule binafsi.
Alisema shule binafsi zina magari ambayo yanatumika kuwabeba wanafunzi kutoka majumbani hadi shuleni.
Alisema kama serikali inataka kuanzisha utaratibu huo, ni dhahiri watahamia katika hospitali kwa kuwa nako zinamilikiwa na watu binafsi na kuwapangia bei.
“Hili suala sisi wamiliki wa shule binafsi tunalipinga moja kwa moja na serikali inatakiwa kufanya utafiti kwanza kabla haijaanza kutekeleza,” alisema Bujugo.
Alisema shule za Green Acres hutoza Sh. 400,000 kwa wanafunzi wa kutwa na Sh. 550,000 kwa wanafunzi wa bweni.
Alisema endapo serikali wakiendelea kusisitiza kuwapo kwa bei hizo, Green Acres hawataweza kuendelea kutoa elimu.
Alisema walimu katika shule zake wanalipwa kuanzia Sh. 700,000 hadi Sh. milioni moja kwa mwalimu wa daraja la juu na Sh. 450,000 hadi Sh. 500,000 kwa walimu wa daraja la chini.
Mkuu wa Shule ya Sahara iliyopo Mabibo, Pili Odinga, alisema ni vyema serikali ikatoa mchanganuo wa gharama hizo walizozielekeza kwa wamiliki wa shule binafsi.
Alisema Shule ya Sahara inajiendesha na haipati ruzuku kutoka serikalini.
Alisema ada ya mwanafunzi kwa shule ya msingi ni Sh. milioni moja kwa kutwa na Sh. milioni 2.2 kwa wanafunzi wa bweni kwa mwaka na kwamba ina walimu 15 wanaolipwa mishahara.
Kwa upande wake, mmiliki wa shule ya sekondari na Chuo cha Ufundi Mong’are, Joseph Mong’are alisema suala hilo haliwezekani na litakuwa gumu kutekelezwa.
Alisema kwa mfano, darasa moja lenye wanafunzi 40 kila mwanafunzi akilipa Sh. 150,000, itakuwa Sh. milioni sita kwa mwaka.
Alisema Sh. milioni sita ikigawanywa kwa miezi 12 ya kuwapa mishahara walimu itapatikana Sh. 500,000, ambayo haitaajiri walimu wala kujenga majengo, vitendea kazi, maktaba, maabara, vitabu havitanunuliwa.
Ofisa Habari wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Oliva Kato, alisema serikali haijatoa waraka wa ada elekezi yoyote kwa shule zisizo za serikali kama ilivyoripotiwa, badala yake imetoa tangazo la katazo la kuongeza ada kwa mwaka masomo 2016 kwa shule hizo.
Alisema hadi sasa hakuna waraka uliotolewa na serikali ukizitaka shule hizo kutoza ada elekezi, badala yake limetoka tangazo linalozitaka kutotoza ada mpya bila kuwasiliana na Kamishna wa Elimu.
“Hakuna ada elekezi yoyote iliyotolewa na serikali kwa mwaka wa masomo 2016 limetolewa tangazo la kuzikataza shule kutotoza ada mpya mpaka zipate maelekezo kutoka kwa Kamishna wa Elimu,” alisisitiza Kato.
Alisema wamiliki wa shule hizo wamepewa wiki mbili kuwasilisha ada walizotoza mwaka huu na vibali vya kutoza pamoja na zitakazotozwa mwaka ujao wa masomo kwa ajili ya kupatiwa vibali na Kamishna.
Alisema kwa sasa bado wataalam wa wizara wanafanya utafiti za kuandaa mfumo wa kielektroniki wa kutambua gharama za kumsomesha mwanafunzi katika elimu ya awali, msingi na sekondari.
MWANANCHI
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema nchi haiwezi kuwa na mabadiliko ya kweli, kama miiko na maadili ya viongozi havitaingizwa kwenye Katiba Mpya.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo ya maisha ya utumishi wa umma uliotukuka juzi, Warioba alisema kwa miaka mingi akishirikiana na rafiki zake, walijaribu kuleta mabadiliko makubwa katika jamii, bila mafanikio.
“Huwezi kuwa na mabadiliko kama huna miiko na maadili kwenye Katiba, lazima kuwe na separation of power (kutenganishwa kwa madaraka), naamini kanuni hizi zitaingia kwenye Katiba Mpya,” alisema.
Mara kadhaa Jaji Warioba amekuwa akisisitiza umuhimu wa vipengele hivyo viwili kuingizwa kwenye Katiba Mpya. Katika rasimu ya pili ya Katiba, Tume ya Mabadiliko ya Katiba, aliyokuwa akiiongoza ilipendekeza miiko na kanuni za uongozi kama tunu za Taifa, lakini Bunge Maalumu la Katiba liliyaondoa na kuyaweka katika msingi wa utawala bora.
Jaji Warioba amekuwa akihoji kuwa uzalendo na uadilifu si mpaka mtu awe kiongozi na kwamba mambo hayo mawili si misingi ya utawala bora ni ya kitaifa na inamhusu kila Mtanzania. Azungumzia tuzo Akiizungumzia tuzo hiyo aliyopewa na Umoja wa Maofisa Watendaji wakuu wa Kampuni Binafsi (CEOrt), Warioba alisema anaamini alipewa heshima hiyo, kutokana na mchango wake alioutoa kwenye sekta binafsi alipokuwa Waziri Mkuu wakati wa Serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi.
Alisema kutokana mabadiliko ya mfumo wa maisha duniani wakati huo, Tanzania ilijikuta imeingia kwenye soko la uchumi bila kujiandaa, ndipo alipoomba msaada wa kitaalamu kutoka sekta binafsi. “Nikiwa Waziri Mkuu nikasema sekta binafsi wasaidie, nikaunda tume walikuwapo pia wasomi, mchango wao ulikuwa mkubwa sana,” alisema. Kuhusu rushwa Pia, alizungumzia ushiriki wake katika tume ya kuchunguza mianya ya rushwa aliyokuwa mwenyekiti wake.
Alisema ilifanya kazi kubwa ya kupambana na rushwa, lakini haikufanikiwa kiasi cha kutosha kwa kuwa bado vitendo hivyo vinaendelea mpaka sasa.
“Tangu mwaka 1996 hadi leo rushwa bado ni tatizo, tulisema kila kitu kiwe wazi, lakini bado sijaona uwazi na uwajibikaji. Tulisema rais amtake kila kiongozi baada ya miezi sita aonyeshe alivyofanya kupambana na rushwa kwa uwazi,” alisema.
HABARILEO
Rais John Magufuli ameendelea kutumbua majipu katika maeneo mbalimbali yenye harufu ya ufisadi, ambapo safari hii ametengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka kwa ajili ya kupisha uchunguzi dhidi ya matumizi mabaya ya kiasi cha Sh bilioni 13 katika Shirika la Reli Tanzania (TRL).
Pia kutokana na utendaji mbovu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa muda mrefu na hatua kutochukuliwa kudhibiti tatizo hilo, Dk Magufuli ameivunja Bodi yote ya Bandari na kutengua uteuzi wa Mwenyekiti wa bodi hiyo, Profesa Joseph Msambichaka na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Awadh Massawe.
Hii ni mara ya kwanza kwa Dk Magufuli kutengua uteuzi wa kiongozi wa juu wa serikali kama Katibu Mkuu, ikiwa ni mwezi mmoja tangu kuapishwa kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Mwinjaka aliteuliwa kushika wadhifa huo wa Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi na Rais mstaafu Jakaya Kikwete Agosti mwaka 2013, hivyo ameitumikia nafasi hiyo kwa takribani miaka mitatu sasa.
Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko. Mwinjaka atemwa Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema kutenguliwa kwa uteuzi wa Dk Mwinjaka, ulitokana na ziara ya ghafla ambayo aliifanya katika shirika hilo la reli.
“Nilifanya ziara ya ghafla TRL ambako katika uchunguzi wa awali nimegundua matumizi mabaya ya fedha Sh bilioni 13 nje ya utaratibu, na kwa sasa uchunguzi unakamilishwa kwa waliohusika. Ila Rais ametengua uteuzi wa Dk Mwinjaka kuanzia leo (jana) na atapangiwa kazi nyingine,” alisema Majaliwa.
Alisema pamoja na ubadhirifu huo, TRL na TPA ni mashirika ambayo yameshindwa kufanya vizuri kwa muda mrefu, ambapo kwa upande wa TRL limeshindwa kabisa kujiendesha.
Alisema Serikali inataka shirika hilo, lijiendeshe lenyewe kwa faida na kutoa huduma stahiki kwa wananchi. Wanane wasimamishwa Pamoja na hayo, Waziri Mkuu alisema amewasimamisha kazi wasimamizi wanane wa Bandari Kavu (ICD) ambao ni Happygod Naftali, Juma Zaar, Steven Naftali Mtui, Titi Ligalwike, Lydia Prosper Kimaro, Mkango Alli, John Elisante pamoja na James Kamwomwa.
Alisema wasimamizi hao, walitajwa kuhusika na upotevu wa makontena takribani 2,387 katika taarifa ya ukaguzi wa ndani ya Julai 30, mwaka huu, ambayo inaonesha TPA iligundua kuwepo kwa vitendo vinavyonesha kuwa bandari hiyo hupitisha makontena mengi bila ya kulipiwa kodi na hakuna hatua yoyote inayochukuliwa.
Aliwataja viongozi wengine ambao hawakutajwa na taarifa hiyo, lakini ni wahusika wakuu katika sekta zilizotoa ruhusa makontena kutoka ndani ya bandari kuwa ni Shaban Mngazija aliyekuwa Meneja Mapato, Rajab Mdoe Mkurugenzi wa Fedha na Mkuu wa Bandari Kavu, Ibin Masoud Kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Apolonia Mosha, Meneja wa Bandari Msaidizi (Fedha).
“Hawa wote nimeagiza wasimamishwe kazi na wawekwe chini ya ulinzi ili kuvisaidia vyombo vya dola wahusika wa makontena hayo waweze kupatikana na hivyo kufanikisha TRA kulipwa kodi yake,” alisisitiza Majaliwa. Mfumo mbovu wa malipo Alisema upotevu huo wa makontena, unaenda sambamba na mfumo usiokidhi wa kupokea malipo unaotoa mwanya mkubwa wa kupoteza mapato ya Serikali.
“Bandari ni eneo muhimu ambako kama itasimamiwa vizuri inaweza kukusanya fedha nyingi na kuchangia pato la taifa. Serikali haitavumilia kuona watu wachache au kikundi chochote kilichojipanga kuhujumu mifumo au kuiibia Serikali kwa namna yoyote ile kwa manufaa ya wachache,” alisema Waziri Mkuu huyo.
Mbali ya Profesa Msambichaka, wajumbe wa Bodi ya TPA iliyovunjwa ni Dk Tulia Ackson, Mhandisi wa Ujenzi, Musa Nyamsingwa, Mtaalamu wa Manunuzi na Mjumbe wa Bodi ya Posta, Donata Mugassa na Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Haruna Masebu.
Wengine ni Mhandisi wa Bodi ya Wahandisi Tanzania, Gema Modu, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Francis Michael, Mkurugenzi wa Mipango NSSF, Crescentius Magori na aliyekuwa Mkurugenzi wa Masoko wa TPA, Flavian Kinunda. Bodi hiyo iliteuliwa Juni mwaka huu na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta.
Hivi karibuni, Waziri Mkuu Majaliwa alifanya ziara za kushtukiza katika shirika la TRL na TPA, ambapo akiwa bandarini, alikagua mfumo wa upokeaji na utoaji mizigo na utozaji wa malipo baada ya kupewa taarifa kwamba kuna makontena 2,431 yametolewa bila kulipiwa ushuru.
Baada ya kuibua madudu hayo, alimtaka Kaimu Meneja wa Bandari, Hebel Mhanga ampelekee majina ya watumishi wote waliohusika na ukwepaji kodi huo na kutoa wiki moja kuhakikisha kuwa mamlaka hiyo, inabadilisha mfumo wa utozaji malipo na kuweka mfumo wa malipo wa kielektroniki.
Alipotembelea TRL, alikagua mabehewa na kuzungumza na baadhi ya wafanyakazi waliokuwepo kwenye stesheni hiyo, ambako alibaini madudu kwenye malipo ya mishahara na makato ya michango ya wafanyakazi.
Aidha alibainisha kuwa anazo taarifa za shirika hilo kupewa fedha na Serikali kiasi cha Sh bilioni 13.5 kwa ajili ya kuendeleza miundombinu ya reli, lakini halikufanya hivyo.
HABARILEO
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limesema limeanza kuchukua hatua kali kwa watu waliohusika na upigaji wa picha wa vifaa vya kijeshi na kusambaza kwenye mitandao ya kijamii, ambapo hadi sasa tayari watu wanne wapo chini ya ulinzi.
Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano wa JWTZ, Kanali Ngemela Lubinga alisema kumekuwa na tabia ya kusambaa kwa taarifa, zisizotakiwa kusambazwa na kusababisha usumbufu kwa taasisi za Serikali na hasa Jeshi.
“Desemba 3, mwaka huu saa 1:15 jioni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, lilitokea tukio lisilo la kawaida lililotendwa na wafanyakazi wa shirika la kupokea mizigo la Swiss Port wakishirikiana na wenzao wa Shirika la Ndege la KLM kwa kupiga picha vifaa vya kijeshi na kusambaza katika mitandao ya kijamii,” alisema Kanali Lubinga.
Alisema mizigo hiyo ni mali ya JWTZ na kuagizwa kwake, hakujaanza hivi karibuni kama baadhi ya watu katika mitandao ya kijamii wanavyoeleza, bali ni matokeo ya hatua zilizochukiliwa na JWTZ kupitia Wizara ya Ulinzi miaka sita iliyopita katika mpango wake wa kujenga uwezo wa JWTZ.
“Tunasikitika kwa tukio hili la watu kujichukulia maamuzi ya kupiga picha kitu ambacho hakikuwahusu na pia kusambaza picha hizo kwenye mitandao ya kijamii na kupelekea kujitokeza kwa maoni ya kupotosha jamii,” aliongeza Mkurugenzi huyo katika JWTZ.
Alisema tabia za kupotosha jamii, zimetokea mara kwa mara na hivyo kuvunja mshikamano uliopo kati ya Serikali na wananchi wake, jambo ambalo jeshi hilo halitalifumbia macho.
Alisema ni kwa msingi huo, wameanza kuwasaka wahusika wote, ambapo tayari watu wanne wapo chini ya ulinzi na watachukuliwa hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine, kutokana na upigaji wa picha hizo na usambazaji wake.
HABARILEO
Agizo la Rais John Magufuli la kutaka Sikukuu ya Uhuru itakayoadhimishwa kesho, inakuwa ya kufanya usafi, limeanza kutekelezwa kwa kasi kubwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Wakati Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick leo atatoa ratiba ya shughuli za usafi ambazo zitasimamiwa na ofisi za wilaya, baadhi ya taasisi na watu binafsi, wamekuwa wanajitolea kufanya usafi katika maeneo yao ya kazi au maeneo mengine yanayowazunguka.
“Kesho (leo) nitazungumza na waandishi wa habari kuhusu jambo hilo namna Dar es Salaam tutakavyofanya usafi,” alisema Sadick jana. Juzi eneo la Kipunguni, wananchi wa maeneo hayo walijitokeza kufanya usafi wa mazingira kwa kufyeka miti na kulima nyasi pamoja na kuhakikisha wanazibua mifereji ya majitaka.
Jana pia Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo alishiriki kufanya usafi wa Jiji la Mwanza kwa kushirikiana na wafanyabiashara wa soko kuu, ambako alitumia fursa hiyo pia kuwataka walipe kodi sahihi kwa serikali.
Mjini Songea, wafanyabiashara wa samaki katika soko kuu la Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wametakiwa kufanya biashara zao za kuzingatia usafi ili kuendelea kuvutia wateja wao kununua kitoweo hicho.
Mwito huo ulitolewa jana na Mkuu wa Masoko wa Manispaa hiyo, Salum Homela alipokuwa akikabidhi vifaa vya usafi kwa wafanyabiashara wa soko hilo ili wavitumie kwa ajili ya kufanya usafi wa mazingira kuzunguka maeneo wanayofanyia shughuli zao ikiwa ni utekelezaji wa agizola Rais John Magufuli.
Homela alisema usafi kwa wafanyabiashara ni jambo la muhimu kwani itasaidia kuepusha watumiaji wa bidhaa zao uwezekano wa kupata magonjwa, yanaosababishwa na uchafu, ikiwemo ugonjwa hatari wa kipindupindu.
Alisema kuna umuhimu kwa wafanya biashara wote wakiwemo wale wa matunda, nyama, na bidhaa nyingine sokoni hapo kuzingatia usafi kwa kuwa watu wengi hasa wageni wanaotembelea manispaa hiyo, jambo la kwanza wanalohitaji kuona ni namna ya wakazi wa Songea walivyoweza kuzingatia suala la usafi wa mazingira katika maeneo muhimu yanayotoa huduma mbalimbali za kijamii.
Mjinji Sumbawanga, mkutano wa kwanza wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga uliokuwa ufanyike leo, umeahirishwa kwa kuwa wakuu wa idara wana majukumu mengine ya kusimamia usafi.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Sumbawanga, Hamid Njovu alithibitisha kwa kusema kuwa shughuli kubwa inayofanyika sasa katika manispaa hiyo ni usafi kutimiza agizo la Rais Magufuli.
Tayari msemaji wa Serikali, Assah Mwambene amewaagiza watumishi wote wa umma, kushiriki katika sherehe za Uhuru kwa kufanya usafi katika maeneo yanayowazunguka na maeneo mengine watakayopangiwa katika kupambana na kipindupindu.
Kwa upande wao, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limesema litashirikiana na wananchi kufanya usafi katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Sikukuu ya Uhuru kesho Desemba 9.
Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano wa JWTZ, Kanali Ngemela Lubinga alisema jana kuwa usafi watakaoufanya pia ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli. “Mwaka huu, Serikali imeamua kubadilisha utaratibu wake wa kawaida na shamrashamra za gwaride badala yake imeagiza kufanyika kwa usafi nchi nzima, hivyo hata sisi tutashiriki kufanya hivyo,” alisema Kanali Lubinga.
Alisema, “Usafi kwa sisi wanajeshi siyo jambo la kufundishwa, ni jadi yetu na ni tabia yetu siku zote kwa hiyo kwa kuwa kambi zetu ni safi kila siku tutaungana na wananchi wote kufanya usafi katika maeneo mbalimbali nchini.”
Kutokana na agizo hilo la Rais, taasisi na mashirika mbalimbali yamekuwa yakijitokeza kushiriki juhudi hizo za kufanya usafi wa mazingira, lengo likiwa ni utekelezaji wa agizo hilo na kuepukana na ugonjwa wa kipindupindu.
Hata hivyo, tayari Serikali ilishatoa ufafanuzi kuhusu siku ya Uhuru kwa wafanyakazi wa umma, kwamba hawatakwenda kazini, bali watabaki majumbani mwao kusherehekea kwa kushiriki kufanya usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali kama alivyoagiza Dk Magufuli.
Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imeshatoa mwongozo kwa uongozi wa mikoa hadi mitaa wa jinsi ya kushiriki usafi kesho, ambapo tayari mikoa mbalimbali ilishaanza utekelezaji wa agizo hilo kwa vitendo. Habari hii imeandikwa na Shadrack Sagati na Hellen Mlacky, Dar; Muhidin Amri, Songea, Peti Siyame, Sumbawanga na Nashon Kennedy, Mwanza.
MTANZANIA
Serikali imetoa wiki mbili kwa wamiliki wa shule za binafsi kuhakikisha wanawasilisha vibali vya ada wanazotoza hivi sasa na watakaokiuka agizo hilo watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Pia imewataka wamiliki wa shule hizo kutoongeza ada kwa mwaka wa masomo unaoanzia Januari, 2016 hadi watakapopata maelekezo kutoka kwa Kamishna wa Elimu.
Ofisa Habari wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Oliver Kato alisema kibali hicho kiwe kimeidhinishwa na Kamishna wa Elimu kikielezea uhalisia wa viwango vya ada vinavyotakiwa kutozwa.
“Tumebaini kuna baadhi ya shule zisizo za Serikali zimekuwa zikiongeza ada kila mwaka pasipo kupata kibali cha Kamishna wa Elimu… utaratibu huu umekuwa ukifanywa na wamiliki hawa kila mwisho wa mwaka na kusababisha usumbufu kwa walimu,”alisema Oliver.
Alisema wamebaini baadhi ya shule, zimekuwa na tabia ya kuongeza ada bila kuwasiliana na Kamishna wa Elimu.
“Kutokana na tabia hii, tumeanza utaratibu wa kukagua vibali vyote kutoka shule moja hadi nyingine ili kukomesha vitendo hivi,”alisema Oliver.
Alisema wamiliki wote wanapaswa kuwasilisha vibali vyao tangu Desemba 3, mwaka huu ambapo Serikali imetoa wiki mbili kutekeleza agizo hilo.
Aliongeza kutokana na utaratibu wa awali Waraka wa Elimu Na 4 wa mwaka 2008, uliweka viwango vya ada vinavyotozwa shule za msingi na sekondari binafsi na za Serikali.
Alisema ada iliyowekwa kwa shule za kutwa zisizo za Serikali ni Sh 150,000 na za bweni ni Sh 380,000 kwa mwaka.
“ Waraka huo ulielekeza ongezeko lolote la ada lazima lipate kibali cha Kamishna wa Elimu kabla ya kuanza kutumika,”alisema Oliver.
Alisema ada zote kwa shule zisizo za Serikali zitabaki kama zilivyokuwa zimeidhinishwa na mamlaka husika.
Alizitaka pia kuwasilisha taarifa za Msajili wa Shule aliyeko Idara ya Ithibati ya Shule inayoeleza kiasi cha ada kinachotozwa kwa sasa na tarehe aliyopata kibali hicho.
Alisema serikali inatambua zipo shule ambazo zinatoa elimu kwa kufuata mitaala ya nje ya nchi na kueleza kuwa shule hizo haziguswi na agizo hilo.
Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo binafsi Tanzania (TAMONGSCO), Benjamin Nkonya alikaririwa na gazeti moja la kila siku akidai hawawezi kufungua shule zao ifikapo Januari, mwakani kupinga hatua ya Serikali kuwazuia kupandisha ada.
Unataka kutumiwa MSG za habari zote kubwa kutoka kwa Millard Ayo? ukiwa na line ya tiGO andika ‘AYO’ tuma kwenda 15510, msg utayotumiwa jibu OK ili uanze kupokea matukio yote kwa sms, pia ungana na Millard Ayokwenye Twitter, FB, Instagram naYouTUBE wa kubonyeza hapa>>>INSTAGRAM TWITTER FB YOUTUBE.