Leo March 14, 2018 Mwanajeshi MT 109795 Private Ramadhan Mlaku mwenye umri wa miaka 28 amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka la mauaji ya askari mwenzie, MT 79512 SGT Saimon Munyama.
Mshtakiwa huyo alifikishwa mahakama hapo akiwa kwenye gari la Jeshi la kubebea wagonjwa huku akiwa na majeraha miguuni.
Akisomewa shtaka lake na Wakili wa Serikali, Mosie Kaima mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,Thomas Simba amedai kuwa mshtakiwa anakabiliwa na kosa moja la mauaji.
Inadaiwa mshtakiwa huyo ambaye ni Mwanajeshi wa Kambi ya Jeshi Makongo ametenda kosa hilo October,30, 2017 akiwa Makao Mkuu ya JWTZ Upanga Ilala Dar es Salaam ambapo alimuua askari mwenzie MT 79512 SGT Munyama.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, Hakimu Simba amesema mshtakiwa haruhusiwi kukiri wala kukana kosa hilo kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.
Pia Hakimu Simba amesema kosa hilo halina dhamana kwa mujibu wa sheria. Wakili Mosie ameeleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, anaomba kesi iahirishwe hadi tarehe nyingine.
Hakimu Simba ameutaka upande wa mashtaka kuhakikisha unakamilisha upelelezi kwa wakati, ambapo ameahirisha kesi hiyo hadi March 28,2018.
Baada ya kusomewa shtaka hilo mshtakiwa alipandishwa tena katika Gari la Jeshi la kubebea Wagonjwa na kupelekwa mahabusu.