Mfanyakazi aliyemtibu mgonjwa wa Ebola Thomas Eric Duncan nchini Marekani kabla hajafariki ameripotiwa kukutwa na virusi vya Ebola kutokana na utafiti wa afya aliofanyiwa ambapo kwa sasa amewekwa kwenye kitengo maalumu huku ikisemekana pamoja na kuvaa mavazi ya kumkinga kuambukizwa virusi, haikusaidia chochote.
Duncan ambaye alipata virusi hivyo vya Ebola alipokuwa mjini Liberia alifariki Jumatano ambapo mlipuko huu wa virusi vya Ebola kutoka nchi za Liberia, Guinea na Sierra Leone imethibitishwa kuwa na waathirika 8300 na vifo vya kukaribia 4033.
Hospitali imethibitisha kuwa njia za kujikinga na maambukizi hayo ya Ebola zinafatwa kwa uangalizi mkubwa na wafanyakazi wote ambao wanafanya kwenye kituo hicho cha afya cha Texas Health Presbyterian ambapo mkuu wa kituo hicho Dr. Tom Frieden amesema kuna uwezekano mfanyakazi huyo hakufata njia zote husika za kujikinga na ugonjwa huo.
Mkuu wa kituo hicho cha afya alikiambia chombo cha habari cha Marekani CBS kwamba watafanya uchunguzi ili kujua ni jinsi gani muhudumu huyo wa afya alipata virusi hivyo vya Ebola na kwamba wote ambao walimuhudumia Duncan watafanyiwa uchunguzi ili kujua kama na wao wamepata virusi hivyo vya Ebola.